Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 23:23-39

Mathayo 23:23-39 Biblia Habari Njema (BHN)

Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnatoza watu sehemu moja ya kumi, hata juu ya majani yenye harufu nzuri, bizari na jira, na huku mnaacha mambo muhimu ya sheria kama vile haki, huruma na imani. Haya ndio hasa mliyopaswa kuyazingatia bila kusahau yale mengine. Viongozi vipofu! Mnatoa nzi katika kinywaji, lakini mnameza ngamia! “Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafisha kikombe na bakuli kwa nje, lakini ndani mnaacha kumejaa vitu mlivyopata kwa unyanganyi na uchoyo. Mfarisayo kipofu! Kisafishe kikombe ndani kwanza na nje kutakuwa safi pia. “Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mko kama makaburi yaliyopakwa chokaa ambayo kwa nje yanaonekana kuwa mazuri, lakini ndani yamejaa mifupa ya maiti na kila namna ya uchafu. Hali kadhalika nyinyi mnaonekana na watu kwa nje kuwa wema, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu. “Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya watu wema. Mwasema: ‘Kama sisi tungaliishi nyakati za wazee wetu hatungalishirikiana nao katika mauaji ya manabii!’ Hivyo mnathibitisha nyinyi wenyewe kwamba nyinyi ni watoto wa watu waliowaua manabii. Haya, kamilisheni ile kazi wazee wenu waliyoianza! Enyi kizazi cha nyoka wenye sumu! Mnawezaje kuiepa hukumu ya moto wa Jehanamu? Ndio maana mimi ninawapelekea nyinyi manabii, watu wenye hekima na waalimu; mtawaua na kuwasulubisha baadhi yao, na wengine mtawapiga viboko katika masunagogi yenu na kuwasaka katika kila mji. Hivyo lawama yote itawapateni kwa ajili ya damu yote ya watu wema iliyomwagwa juu ya ardhi. Naam, tangu kumwagwa damu ya Abeli ambaye hakuwa na hatia, mpaka ile ya Zakaria, mwana wa Barakia, ambaye mlimuua hekaluni kati ya patakatifu na madhabahu. Nawaambieni kweli, kizazi hiki kitapata adhabu kwa sababu ya mambo haya. “Yerusalemu! Ee Yerusalemu! Unawaua manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako. Mara ngapi nimejaribu kuwakusanya watoto wako kwangu, kama vile kuku anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka. Haya basi, nyumba yako itaachwa mahame. Nakuambia, hutaniona tena mpaka wakati utakaposema: ‘Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana.’”

Shirikisha
Soma Mathayo 23

Mathayo 23:23-39 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ole wenu Waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa, bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache. Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia. Ole wenu Waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang'anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nako kupate kuwa safi. Ole wenu, Waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi. Ole wenu, Waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnayajenga makaburi ya manabii, na kuyapamba maziara ya wenye haki, na kusema, Kama sisi tungalikuwako zamani za baba zetu, hatungalishirikiana nao katika damu ya manabii. Hivi mwajishuhudia wenyewe, ya kwamba ninyi ni wana wao waliowaua manabii. Kijazeni basi kipimo cha baba zenu. Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya Jehanamu? Kwa sababu hiyo, angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima na waandishi; na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulubisha, na wengine wao mtawapiga katika masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji; hivyo ije juu yenu damu yote ya haki iliyomwagika juu ya nchi, tangu damu ya Habili, yule mwenye haki, hata damu ya Zakaria mwana wa Barakia, mliyemwua kati ya patakatifu na madhabahu. Amin, nawaambieni, Mambo hayo yote yatakuja juu ya kizazi hiki. Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii, na kuwapiga kwa mawe wale waliotumwa kwako! Ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako, kama vile kuku awakusanyavyo pamoja vifaranga wake chini ya mabawa yake, lakini hamkutaka! Angalieni, nyumba yenu mmeachiwa hali ya ukiwa. Kwa maana nawaambia, Hamtaniona kamwe tangu sasa, hadi mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.

Shirikisha
Soma Mathayo 23

Mathayo 23:23-39 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache. Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang’anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi. Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi. Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnayajenga makaburi ya manabii, na kuyapamba maziara ya wenye haki, na kusema, Kama sisi tungalikuwako zamani za baba zetu, hatungalishirikiana nao katika damu ya manabii. Hivi mwajishuhudia wenyewe, ya kwamba ninyi ni wana wao waliowaua manabii. Kijazeni basi kipimo cha baba zenu. Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehanum? Kwa sababu hiyo, angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima na waandishi; na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulibisha, na wengine wao mtawapiga katika masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji; hivyo ije juu yenu damu yote ya haki iliyomwagika juu ya nchi, tangu damu ya Habili, yule mwenye haki, hata damu ya Zakaria bin Barakia, mliyemwua kati ya patakatifu na madhabahu. Amin, nawaambieni, Mambo hayo yote yatakuja juu ya kizazi hiki. Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii, na kuwapiga kwa mawe wale waliotumwa kwako! Ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako, kama vile kuku avikusanyavyo pamoja vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hamkutaka! Angalieni, nyumba yenu mmeachiwa hali ya ukiwa. Kwa maana nawaambia, Hamtaniona kamwe tangu sasa, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.

Shirikisha
Soma Mathayo 23

Mathayo 23:23-39 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

“Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnatoa zaka ya mnanaa, bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu zaidi ya sheria, yaani haki, huruma na uaminifu. Iliwapasa kufanya haya makuu ya sheria bila kupuuza hayo matoleo. Ninyi viongozi vipofu, mnachuja kiroboto lakini mnameza ngamia! “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa unyangʼanyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu! Safisha ndani ya kikombe na sahani kwanza, ndipo nje itakuwa safi pia. “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnafanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, ambayo yanapendeza kwa nje, lakini ndani yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu. Vivyo hivyo, kwa nje ninyi mnaonekana kwa watu kuwa wenye haki, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu. “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya wenye haki. Nanyi mwasema, ‘Kama tungeishi wakati wa baba zetu, hatungeshiriki katika kumwaga damu ya manabii!’ Hivyo mnajishuhudia wenyewe kwamba ninyi ni wana wa wale waliowaua manabii. Haya basi, kijazeni kipimo cha dhambi ya baba zenu! “Ninyi nyoka, ninyi uzao wa nyoka wenye sumu! Mtaiepukaje hukumu ya Jehanamu? Kwa sababu hii, tazameni, natuma kwenu manabii na wenye hekima na walimu. Baadhi yao mtawaua na kuwasulubisha, na wengine wao mtawapiga mijeledi katika masinagogi yenu na kuwafuatia kutoka mji mmoja hadi mji mwingine. Hivyo ile damu ya wenye haki wote iliyomwagwa hapa duniani, tangu damu ya Abeli, aliyekuwa mwenye haki, hadi damu ya Zakaria mwana wa Barakia, mliyemuua kati ya patakatifu na madhabahu, itawajia juu yenu. Amin, nawaambia, haya yote yatakuja kwa kizazi hiki. “Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako pamoja, kama vile kuku akusanyavyo vifaranga wake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka! Tazama nyumba yenu imeachwa ukiwa. Kwa maana nawaambia, hamtaniona tena tangu sasa hadi mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana.’”

Shirikisha
Soma Mathayo 23