Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 2

2
Wataalamu wa nyota waenda kumwona mtoto Isa
1Baada ya Isa kuzaliwa katika mji wa Bethlehemu huko Yudea, wakati wa utawala wa Mfalme Herode, wataalamu wa mambo ya nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu 2wakiuliza, “Yuko wapi huyo aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tumeona nyota yake ikitokea mashariki, nasi tumekuja kumwabudu.”
3Mfalme Herode aliposikia jambo hili aliingiwa na hofu sana pamoja na watu wote wa Yerusalemu. 4Herode akawaita pamoja viongozi wa makuhani na walimu wa Torati, akawauliza ni wapi ambapo Al-Masihi#2:4 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta. angezaliwa. 5Nao wakamwambia, “Katika Bethlehemu ya Yudea, kwa maana hivyo ndivyo ilivyoandikwa na nabii:
6“ ‘Nawe, Bethlehemu, katika nchi ya Yuda,
wewe si mdogo miongoni
mwa watawala wa Yuda;
kwa maana kutoka kwako atakuja mtawala
atakayekuwa mchungaji
wa watu wangu Israeli.’#2:6 Mika 5:2
7Ndipo Herode akawaita wale wataalamu wa nyota kwa siri na kutaka kujua kutoka kwao uhakika kamili wa wakati ile nyota ilionekana. 8Kisha akawatuma Bethlehemu na kuwaambia, “Nendeni mkamtafute mtoto huyo kwa makini. Mara tu mtakapompata, nileteeni taarifa ili nami niende kumwabudu.”
9Baada ya kumsikia mfalme, wale wataalamu wa nyota wakaenda zao, nayo ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, nao wakaifuata hadi iliposimama mahali alipokuwa mtoto. 10Walipoiona ile nyota wakajawa na furaha kubwa mno. 11Walipoingia ndani ya ile nyumba, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mama yake, wakamsujudia na kumwabudu yule mtoto Isa. Ndipo wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane. 12Kwa kuwa walikuwa wameonywa katika ndoto wasirudi kwa Herode, wakarudi nchi yao kwa njia nyingine.
Yusufu, Mariamu na mtoto Isa wakimbilia Misri
13Walipokwisha kwenda zao, malaika wa Mwenyezi Mungu akamtokea Yusufu katika ndoto akamwambia, “Amka, umchukue mtoto na mama yake, mkimbilie Misri. Kaeni huko hadi nitakapowaambia, kwa maana Herode anataka kumtafuta huyu mtoto ili amuue.”
14Kisha Yusufu akaamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake wakati wa usiku, nao wakaenda Misri, 15ambako walikaa hadi Herode alipofariki. Hili lilifanyika ili litimie lile neno Mwenyezi Mungu alilosema kupitia kwa nabii: “Nilimwita mwanangu kutoka Misri.”#2:15 Hosea 11:1
16Herode alipogundua kwamba alikuwa amedanganywa na wale wataalamu wa nyota, alikasirika sana, naye akatoa amri ya kuwaua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili kurudi chini katika mji wa Bethlehemu na sehemu zote za jirani, kwa mujibu wa ule muda alioambiwa na wale wataalamu wa nyota. 17Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, aliposema:
18“Sauti ilisikika huko Rama,
maombolezo na kilio kikubwa,
Raheli akilia kwa ajili ya wanawe,
akikataa kufarijiwa,
kwa sababu hawako tena.”#2:18 Yeremia 31:15
Kurudi Nasiri kutoka Misri
19Baada ya Herode kufa, malaika wa Mwenyezi Mungu akamtokea Yusufu katika ndoto huko Misri 20na kusema, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mwende, mrudi katika nchi ya Israeli kwa sababu wale waliokuwa wakijaribu kumuua mtoto wamekufa.”
21Basi Yusufu, akainuka, akamchukua mtoto na mama yake wakaenda hadi nchi ya Israeli. 22Lakini aliposikia kwamba Arkelao alikuwa anatawala huko Yudea baada ya Herode baba yake, aliogopa kwenda huko. Kwa kuwa alikuwa ameonywa katika ndoto, akaenda zake sehemu za Galilaya, 23akaenda kuishi katika mji ulioitwa Nasiri. Hivyo likawa limetimia neno lililonenwa na manabii waliposema, “Ataitwa Mnasiri.”

Iliyochaguliwa sasa

Mathayo 2: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia