Mathayo 13:34-58
Mathayo 13:34-58 NENO
Isa alinena mambo haya yote kwa umati wa watu kwa mifano, wala hakuwaambia lolote pasipo mfano. Hii ilikuwa ili kutimiza neno lililonenwa na nabii, aliposema: “Nitafungua kinywa changu niseme nao kwa mifano; nitahubiri mambo yaliyofichika tangu kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.” Kisha Isa akaagana na ule umati, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamjia wakamwambia, “Tueleze maana ya ule mfano wa magugu shambani.” Akawaambia, “Aliyepanda mbegu nzuri ni Mwana wa Adamu. Shamba ni ulimwengu na mbegu nzuri ni wana wa ufalme. Magugu ni wana wa yule mwovu. Yule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika. “Kama vile magugu yang’olewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika wake, nao watakusanya kutoka ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote. Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watang’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Yeye aliye na masikio, na asikie. “Ufalme wa mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba. “Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na mfanyabiashara aliyekuwa akitafuta lulu safi. Alipoipata lulu moja ya thamani kubwa, alienda akauza vyote alivyokuwa navyo akainunua. “Tena, ufalme wa mbinguni ni kama wavu wa kuvua samaki uliotupwa baharini ukavua samaki wa kila aina. Ulipojaa, wavuvi wakauvuta ufuoni, wakaketi na kukusanya samaki wazuri kuwaweka kwenye vyombo safi, lakini wale samaki wabaya wakawatupa. Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki. Nao watawatupa hao waovu katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.” Isa akauliza, “Je, mmeyaelewa haya yote?” Wakamjibu, “Ndiyo.” Akawaambia, “Basi kila mwalimu wa Torati aliyefundishwa elimu ya ufalme wa mbinguni ni kama mwenye nyumba anayetoa kutoka ghala yake mali mpya na mali ya zamani.” Isa alipomaliza kutoa mifano hii, akaondoka. Alipofika mji wa kwao, akawafundisha watu katika sinagogi lao. Nao wakastaajabu, wakauliza, “Mtu huyu amepata wapi hekima hii na uwezo huu wa kufanya miujiza? Huyu si yule mwana wa seremala? Mama yake si yeye aitwaye Mariamu, nao ndugu zake si Yakobo, Yusufu, Simoni na Yuda? Nao dada zake wote, hawako hapa pamoja nasi? Mtu huyu amepata wapi basi mambo haya yote?” Wakachukizwa naye. Lakini Isa akawaambia, “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani mwake.” Naye hakufanya miujiza mingi huko kwa sababu ya kutokuamini kwao.