Mathayo 13:34-58
Mathayo 13:34-58 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu aliwaambia watu hayo yote kwa mifano. Hakuwaambia chochote bila kutumia mifano, ili jambo lililonenwa na nabii litimie: “Nitasema nao kwa mifano; nitafichua yaliyofichika tangu kuumbwa ulimwengu.” Kisha Yesu aliwaaga wale watu, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, “Tufafanulie ule mfano wa magugu shambani.” Yesu akawaambia, “Mpanzi wa zile mbegu nzuri ni Mwana wa Mtu. Lile shamba ni ulimwengu. Zile mbegu nzuri ni watu wale ambao ufalme ni wao. Lakini yale magugu ni wale watu wa yule Mwovu. Adui aliyepanda yale magugu ni Ibilisi. Mavuno ni mwisho wa nyakati na wavunaji ni malaika. Kama vile magugu yanavyokusanywa na kuchomwa moto, ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati; Mwana wa Mtu atawatuma malaika wake wawakusanye kutoka katika ufalme wake wale wote wenye kusababisha dhambi, na wote wenye kutenda maovu, na kuwatupa katika tanuri ya moto, na huko watalia na kusaga meno. Kisha, wale wema watangara kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio na asikie! “Ufalme wa mbinguni unafanana na hazina iliyofichika shambani. Mtu mmoja aliigundua, akaificha tena. Alifurahi sana hata akaenda kuuza yote aliyokuwa nayo, akalinunua shamba lile. “Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na mfanyabiashara mmoja mwenye kutafuta lulu nzuri. Alipopata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda, akauza yote aliyokuwa nayo, akainunua lulu ile. “Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na wavu uliotupwa baharini, ukanasa samaki wa kila aina. Ulipojaa, watu waliuvuta pwani, wakaketi, wakachagua samaki wazuri wakawaweka ndani ya vikapu vyao, na wabaya wakawatupa. Ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati: Malaika watatokea, watawatenganisha watu wabaya na watu wema, na kuwatupa hao wabaya katika tanuri ya moto. Huko watalia na kusaga meno.” Yesu akawauliza, “Je, mmeelewa mambo haya yote?” Wakamjibu, “Naam.” Naye akawaambia, “Hivyo basi, kila mwalimu wa sheria anayekuwa mwanafunzi wa ufalme wa mbinguni anafanana na mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.” Yesu alipomaliza kusema mifano hiyo alitoka mahali hapo, akaenda kijijini kwake. Huko akawa anawafundisha watu katika sunagogi lao hata wakashangaa, wakasema, “Huyu amepata wapi hekima hii na maajabu? Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi, amepata wapi haya yote?” Basi, wakawa na mashaka naye. Lakini Yesu akawaambia, “Nabii hakosi kuheshimiwa, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani mwake!” Kwa hiyo, hakutenda miujiza mingi pale kwa sababu ya kutoamini kwao.
Mathayo 13:34-58 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno; ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Nitafumbua kinywa changu kwa mifano, Nitayatamka yaliyositirika tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Kisha Yesu akawaaga makutano, akaingia katika nyumba; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa magugu ya shambani. Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu; lile shamba ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu; yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika. Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika wake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuri ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong'aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna; hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa. Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuri ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam. Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale. Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake. Na alipofika mji wa kwao, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? Na dada zake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe. Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutoamini kwao.
Mathayo 13:34-58 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno; ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Nitafumbua kinywa changu kwa mifano, Nitayatamka yaliyositirika tangu awali. Kisha Yesu akawaaga makutano, akaingia nyumbani; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa magugu ya kondeni. Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu; lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu; yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika. Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna; hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa. Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam. Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale. Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake. Na alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe. Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutokuamini kwao.
Mathayo 13:34-58 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Isa alinena mambo haya yote kwa umati wa watu kwa mifano, wala hakuwaambia lolote pasipo mfano. Hii ilikuwa ili kutimiza neno lililonenwa na nabii, aliposema: “Nitafungua kinywa changu niseme nao kwa mifano; nitahubiri mambo yaliyofichika tangu kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.” Kisha Isa akaagana na ule umati, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamjia wakamwambia, “Tueleze maana ya ule mfano wa magugu shambani.” Akawaambia, “Aliyepanda mbegu nzuri ni Mwana wa Adamu. Shamba ni ulimwengu na mbegu nzuri ni wana wa ufalme. Magugu ni wana wa yule mwovu. Yule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika. “Kama vile magugu yang’olewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika wake, nao watakusanya kutoka ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote. Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watang’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Yeye aliye na masikio, na asikie. “Ufalme wa mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba. “Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na mfanyabiashara aliyekuwa akitafuta lulu safi. Alipoipata lulu moja ya thamani kubwa, alienda akauza vyote alivyokuwa navyo akainunua. “Tena, ufalme wa mbinguni ni kama wavu wa kuvua samaki uliotupwa baharini ukavua samaki wa kila aina. Ulipojaa, wavuvi wakauvuta ufuoni, wakaketi na kukusanya samaki wazuri kuwaweka kwenye vyombo safi, lakini wale samaki wabaya wakawatupa. Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki. Nao watawatupa hao waovu katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.” Isa akauliza, “Je, mmeyaelewa haya yote?” Wakamjibu, “Ndiyo.” Akawaambia, “Basi kila mwalimu wa Torati aliyefundishwa elimu ya ufalme wa mbinguni ni kama mwenye nyumba anayetoa kutoka ghala yake mali mpya na mali ya zamani.” Isa alipomaliza kutoa mifano hii, akaondoka. Alipofika mji wa kwao, akawafundisha watu katika sinagogi lao. Nao wakastaajabu, wakauliza, “Mtu huyu amepata wapi hekima hii na uwezo huu wa kufanya miujiza? Huyu si yule mwana wa seremala? Mama yake si yeye aitwaye Mariamu, nao ndugu zake si Yakobo, Yusufu, Simoni na Yuda? Nao dada zake wote, hawako hapa pamoja nasi? Mtu huyu amepata wapi basi mambo haya yote?” Wakachukizwa naye. Lakini Isa akawaambia, “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani mwake.” Naye hakufanya miujiza mingi huko kwa sababu ya kutokuamini kwao.