Luka 11:1-13
Luka 11:1-13 NEN
Siku moja, Yesu alikuwa mahali fulani akiomba. Alipomaliza kuomba, mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, tufundishe kuomba, kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake.” Akawaambia, “Mnapoomba, semeni: “ ‘Baba yetu (uliye mbinguni), jina lako litukuzwe, ufalme wako uje. (Mapenzi yako yafanyike hapa duniani kama huko mbinguni.) Utupatie kila siku riziki yetu. Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa na sisi huwasamehe wote wanaotukosea. Wala usitutie majaribuni (bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu).’ ” Kisha akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu mwenye rafiki yake, naye akamwendea usiku wa manane na kumwambia, ‘Rafiki, nikopeshe mikate mitatu. Kwa sababu rafiki yangu amekuja kutoka safarini, nami sina kitu cha kumpa.’ “Kisha yule aliyeko ndani amjibu, ‘Usinisumbue. Mlango umefungwa, nami na watoto wangu tumelala. Siwezi kuamka nikupe chochote.’ Nawaambia, ingawa huyo mtu hataamka na kumpa hiyo mikate kwa sababu ni rafiki yake, lakini kwa sababu ya kuendelea kwake kuomba, ataamka na kumpa kiasi anachohitaji. “Kwa hiyo nawaambia: Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango. Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango. “Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba samaki, atampa nyoka badala yake? Au mtoto akimwomba yai atampa nge? Basi ikiwa ninyi mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wale wamwombao!”