Walawi 10:1-7
Walawi 10:1-7 NEN
Nadabu na Abihu, wana wa Aroni, wakachukua vyetezo vyao, wakaweka moto ndani yake na kuongeza uvumba; kisha wakamtolea BWANA moto usio halali, kinyume na agizo la Mungu. Hivyo moto ukaja kutoka kwa uwepo wa BWANA na kuwaramba, nao wakafa mbele za BWANA. Kisha Mose akamwambia Aroni, “Hili ndilo alilonena BWANA wakati aliposema: “ ‘Miongoni mwa wale watakaonikaribia nitajionyesha kuwa mtakatifu; machoni pa watu wote nitaheshimiwa.’ ” Aroni akanyamaza. Mose akawaita Mishaeli na Elisafani, wana wa Uzieli mjomba wake Aroni, akawaambia, “Njooni hapa. Ondoeni miili ya binamu zenu mbele ya mahali patakatifu, mkaipeleke nje ya kambi.” Hivyo wakaja na kuwaondoa, wakiwa bado wamevalia makoti yao ya ibada, wakawapeleka nje ya kambi, kama Mose alivyoamuru. Ndipo Mose akamwambia Aroni pamoja na wanawe, Eleazari na Ithamari, “Msifunue vichwa vyenu wala msirarue mavazi yenu, la sivyo mtakufa na BWANA ataikasirikia jumuiya nzima. Lakini ndugu zenu, nyumba yote ya Israeli, wanaweza kuwaombolezea wale ambao BWANA amewaangamiza kwa moto. Msitoke nje ya ingilio la Hema la Kukutania, la sivyo mtakufa, kwa sababu mafuta ya BWANA ya upako yako juu yenu.” Hivyo wakafanya kama vile Mose alivyosema.