Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Maombolezo 4

4
# 4 Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22. 1Jinsi dhahabu ilivyopoteza mng’ao wake,
dhahabu iliyo safi haing’ai!
Vito vya thamani vimetawanywa
kwenye mwanzo wa kila barabara.
2Wana wa Sayuni wenye thamani,
ambao mwanzo uzito wa thamani yao
ulikuwa wa dhahabu,
sasa wanaangaliwa kama vyungu vya udongo,
kazi ya mikono ya mfinyanzi!
3Hata mbweha hutoa matiti yao
kunyonyesha watoto wao,
lakini watu wangu wamekuwa wasio na huruma
kama mbuni jangwani.
4Kwa sababu ya kiu ulimi wa mtoto mchanga
umegandamana na kaakaa la kinywa chake,
watoto huomba mkate,
lakini hakuna yeyote awapaye.
5Wale waliokula vyakula vya kifahari
ni maskini barabarani.
Wale waliokuzwa wakivaa nguo za zambarau
sasa wanalalia majivu.
6Adhabu ya watu wangu
ni kubwa kuliko ile ya Sodoma,
ambayo ilipinduliwa ghafula
wala hapakuwa na mkono wa msaada.
7Wakuu wao walikuwa wameng’aa kuliko theluji
na weupe kuliko maziwa,
miili yao ilikuwa myekundu kuliko marijani,
kuonekana kwao kama yakuti samawi.
8Lakini sasa ni weusi kuliko masizi;
hawatambulikani barabarani.
Ngozi yao imeshikamana juu ya mifupa yao,
imekuwa mikavu kama fimbo.
9Wale waliouawa kwa upanga ni bora
kuliko wale wanaokufa njaa;
wanateseka kwa njaa, wanatokomea
kwa kukosa chakula kutoka shambani.
10Kwa mikono yao wenyewe wanawake wenye huruma
wanapika watoto wao wenyewe,
waliokuwa chakula chao
watu wangu walipoangamizwa.
11Mwenyezi Mungu ametoa nafasi kamilifu ya ghadhabu yake;
ameimwaga hasira yake kali.
Amewasha moto katika Sayuni
ambao umeteketeza misingi yake.
12Wafalme wa dunia hawakuamini,
wala mtu yeyote wa duniani,
kwamba adui na watesi wangeweza kuingia
kwenye malango ya Yerusalemu.
13Lakini hili lilitokea kwa sababu ya dhambi za manabii wake,
na maovu ya makuhani wake,
waliomwaga ndani yake
damu ya wenye haki.
14Sasa wanapapasa papasa barabarani
kama watu ambao ni vipofu.
Wamenajisiwa kabisa kwa damu,
hata hakuna anayethubutu kugusa mavazi yao.
15Watu wanawapigia kelele, “Ondokeni! Ninyi ni najisi!
Ondokeni! Ondokeni! Msituguse!”
Wanapokimbia na kutangatanga,
watu miongoni mwa mataifa wanasema,
“Hawawezi kukaa hapa zaidi.”
16Mwenyezi Mungu mwenyewe amewatawanya;
hawaangalii tena.
Makuhani hawaoneshwi heshima,
wazee hawakubaliki.
17Zaidi ya hayo, macho yetu yalichoka,
kwa kutazamia bure msaada;
tuliangalia kutoka minara yetu
kwa taifa lisiloweza kutuokoa.
18Watu walituvizia katika kila hatua
hata hatukuweza kutembea katika barabara zetu.
Mwisho wetu ulikuwa karibu, siku zetu zilikuwa zimetimia,
kwa maana mwisho wetu ulikuwa umefika.
19Waliotufuatia walikuwa wepesi
kuliko tai angani;
walitusaka juu milimani
na kutuvizia jangwani.
20Mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu, pumzi ya uhai wetu hasa,
alinaswa katika mitego yao.
Tulifikiri kwamba chini ya kivuli chake
tungeishi miongoni mwa mataifa.
21Shangilia na ufurahi, ee Binti Edomu,
wewe unayeishi nchi ya Usi.
Lakini kwako pia kikombe kitapitishwa,
Utalewa na kuvuliwa nguo ubaki uchi.
22Ee Binti Sayuni, adhabu yako itaisha,
hatarefusha muda wako wa kukaa uhamishoni.
Lakini, ee Binti Edomu, ataadhibu dhambi yako,
na atafunua uovu wako.

Iliyochaguliwa sasa

Maombolezo 4: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia