Maombolezo 3
3
# 3 Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22. 1Mimi ndiye mtu aliyeona mateso
kwa fimbo ya ghadhabu yake.
2Amenifukuzia mbali na kunifanya nitembee
gizani wala si katika nuru;
3hakika, amegeuza mkono wake dhidi yangu
tena na tena, mchana kutwa.
4Amefanya ngozi yangu na nyama yangu kuchakaa
na ameivunja mifupa yangu.
5Amenizingira na kunizunguka
kwa uchungu na taabu.
6Amenifanya niishi gizani
kama wale waliokufa.
7Amenizungushia ukuta ili nisiweze kutoroka,
amenifunga kwa minyororo mizito.
8Hata ninapoita au kulia ili kuomba msaada,
anakataa kupokea maombi yangu.
9Ameizuia njia yangu kwa mapande ya mawe,
amepotosha njia zangu.
10Kama dubu aviziaye,
kama simba mafichoni,
11ameniburuta kutoka njiani,
akanirarua na kuniacha bila msaada.
12Amevuta upinde wake
na kunifanya mimi niwe lengo kwa ajili ya mishale yake.
13Alinichoma moyo wangu kwa mishale
iliyotoka kwenye podo lake.
14Nimekuwa kichekesho kwa watu wangu wote,
wananidhihaki kwa wimbo mchana kutwa.
15Amenijaza kwa majani machungu
na kunishibisha kwa nyongo.
16Amevunja meno yangu kwa changarawe,
amenikanyagia mavumbini.
17Amani yangu imeondolewa,
nimesahau kufanikiwa ni nini.
18Kwa hiyo nasema, “Fahari yangu imeondoka
na yale yote niliyokuwa nimetarajia kutoka kwa Mwenyezi Mungu.”
19Nayakumbuka mateso yangu na kutangatanga kwangu,
uchungu na nyongo.
20Ninayakumbuka vyema,
nayo nafsi yangu imezimia ndani yangu.
21Hata hivyo najikumbusha neno hili
na kwa hiyo ninalo tumaini.
22Kwa sababu ya upendo mkuu wa Mwenyezi Mungu, hatuangamii,
kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe.
23Ni mpya kila asubuhi,
uaminifu wako ni mkuu.
24Nimeiambia nafsi yangu, “Mwenyezi Mungu ni fungu langu,
kwa hiyo nitamngojea.”
25Mwenyezi Mungu ni mwema kwa wale wanaomtumaini,
na kwa yule anayemtafuta;
26ni vyema kungojea kwa utulivu
kwa ajili ya wokovu wa Mwenyezi Mungu.
27Ni vyema mtu kuchukua nira
bado angali kijana.
28Na akae peke yake awe kimya,
kwa maana Mwenyezi Mungu ameiweka juu yake.
29Hata azike uso wake mavumbini
bado tumaini litakuwepo.
30Na atoe shavu lake kwa yule ampigaye,
na ajazwe na aibu.
31Kwa kuwa watu hawakatiliwi mbali
na Bwana milele.
32Ingawa huleta huzuni, ataonesha huruma,
kwa kuwa upendo wake usiokoma ni mkuu.
33Kwa maana hapendi kuwaletea mateso
au huzuni watoto wa wanadamu.
34Kuwaponda chini ya nyayo
wafungwa wote katika nchi,
35Kumnyima mtu haki zake
mbele za Aliye Juu Sana,
36kumnyima mtu haki:
Je, Bwana asione mambo kama haya?
37Nani awezaye kusema nalo likatendeka
kama Bwana hajaamuru?
38Je, si ni kwenye kinywa cha Aliye Juu Sana
ndiko yatokako maafa na mambo mema?
39Je, mwanadamu yeyote aliye hai aweza kulalamika
wakati anapoadhibiwa kwa ajili ya dhambi zake?
40Tuzichunguze njia zetu na kuzijaribu,
na tumrudie Mwenyezi Mungu.
41Tuinue mioyo yetu pamoja na mikono yetu
kwa Mungu mbinguni, na tuseme:
42“Tumetenda dhambi na kuasi
nawe hujasamehe.
43“Umejifunika mwenyewe kwa hasira na kutufuatilia;
umetuchinja bila huruma.
44Unajifunika mwenyewe kwa wingu,
ili pasiwe na ombi
litakaloweza kupenya.
45Umetufanya takataka na uchafu
miongoni mwa mataifa.
46“Adui zetu wote wamefumbua vinywa vyao
wazi dhidi yetu.
47Tumeteseka kwa hofu kuu na shida ya ghafula,
uharibifu na maangamizi.”
48Vijito vya machozi vinatiririka kutoka machoni mwangu,
kwa sababu watu wangu wameangamizwa.
49Macho yangu yatatiririka machozi bila kukoma,
bila kupata nafuu,
50hadi Mwenyezi Mungu atazame chini
kutoka mbinguni na kuona.
51Lile ninaloliona huniletea huzuni nafsini
kwa sababu ya wanawake wote wa mji wangu.
52Wale waliokuwa adui zangu bila sababu
wameniwinda kama ndege.
53Walijaribu kukomesha maisha yangu ndani ya shimo
na kunitupia mawe;
54maji yalifunika juu ya kichwa changu,
nami nikafikiri nilikuwa karibu
kukatiliwa mbali.
55Nililiitia jina lako, Ee Mwenyezi Mungu,
kutoka vina vya shimo.
56Ulisikia ombi langu: “Usikizibie masikio yako
kilio changu nikuombapo msaada.”
57Ulikuja karibu nilipokuita,
nawe ukasema, “Usiogope.”
58Ee Bwana, ulichukua shauri langu,
ukaukomboa uhai wangu.
59Umeona, Ee Mwenyezi Mungu, ubaya niliotendewa.
Tetea shauri langu!
60Umeona kina cha kisasi chao,
mashauri yao yote mabaya dhidi yangu.
61Ee Mwenyezi Mungu, umesikia matukano yao,
mashauri yao yote mabaya dhidi yangu:
62kile adui zangu wanachonong’ona na kunung’unikia
dhidi yangu mchana kutwa.
63Watazame! Wakiwa wameketi au wamesimama,
wananidhihaki katika nyimbo zao.
64Uwalipe kile wanachostahili, Ee Mwenyezi Mungu,
kwa yale ambayo mikono yao imetenda.
65Weka pazia juu ya mioyo yao,
laana yako na iwe juu yao!
66Wafuatilie katika hasira na uwaangamize
chini ya mbingu za Mwenyezi Mungu.
Iliyochaguliwa sasa
Maombolezo 3: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.