Maombolezo 1:12-22
Maombolezo 1:12-22 NEN
“Je, si kitu kwenu, ninyi nyote mpitao kando? Angalieni kote mwone. Je, kuna maumivu kama maumivu yangu yale yaliyotiwa juu yangu, yale BWANA aliyoyaleta juu yangu katika siku ya hasira yake kali? “Kutoka juu alipeleka moto, akaushusha katika mifupa yangu. Aliitandia wavu miguu yangu na akanirudisha nyuma. Akanifanya mkiwa, na mdhaifu mchana kutwa. “Dhambi zangu zimefungwa kwenye nira, kwa mikono yake zilifumwa pamoja. Zimefika shingoni mwangu na Bwana ameziondoa nguvu zangu. Amenitia mikononi mwa wale ambao siwezi kushindana nao. “Bwana amewakataa wapiganaji wa vita wote walio kati yangu, ameagiza jeshi dhidi yangu kuwaponda vijana wangu wa kiume. Katika shinikizo lake la divai Bwana amemkanyaga Bikira Binti Yuda. “Hii ndiyo sababu ninalia na macho yangu yanafurika machozi. Hakuna yeyote aliye karibu kunifariji, hakuna yeyote wa kuhuisha roho yangu. Watoto wangu ni wakiwa kwa sababu adui ameshinda.” Sayuni ananyoosha mikono yake, lakini hakuna yeyote wa kumfariji. BWANA ametoa amri kwa ajili ya Yakobo kwamba majirani zake wawe adui zake; Yerusalemu umekuwa kitu najisi miongoni mwao. “BWANA ni mwenye haki, hata hivyo niliasi dhidi ya amri yake. Sikilizeni, enyi mataifa yote, tazameni maumivu yangu. Wavulana wangu na wasichana wangu wamekwenda uhamishoni. “Niliita washirika wangu lakini walinisaliti. Makuhani wangu na wazee wangu waliangamia mjini walipokuwa wakitafuta chakula ili waweze kuishi. “Angalia, Ee BWANA, jinsi nilivyo katika dhiki! Nina maumivu makali ndani yangu, nami ninahangaika moyoni mwangu, kwa kuwa nimekuwa mwasi sana. Huko nje, upanga unaua watu, ndani, kipo kifo tu. “Watu wamesikia ninavyolia kwa uchungu, lakini hakuna yeyote wa kunifariji. Adui zangu wote wamesikia juu ya dhiki yangu, wanafurahia lile ulilolitenda. Naomba uilete siku uliyoitangaza ili wawe kama mimi. “Uovu wao wote na uje mbele zako; uwashughulikie wao kama vile ulivyonishughulikia mimi kwa sababu ya dhambi zangu zote. Kulia kwangu kwa uchungu ni kwingi na moyo wangu umedhoofika.”