Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yuda 1

1
Salamu
1Yuda, mtumwa wa Isa Al-Masihi, na nduguye Yakobo.
Kwa wale walioitwa, waliopendwa katika Mungu Baba#1:1 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. Mwenyezi na kuhifadhiwa salama ndani ya Isa Al-Masihi.
2Rehema, amani na upendo ziwe kwenu kwa wingi.
Dhambi na hukumu ya watu wasiomcha Mwenyezi Mungu
3Wapendwa, ingawa nilikuwa ninatamani sana kuwaandikia kuhusu wokovu ambao tunaushiriki sisi sote, niliona imenipasa kuwaandikia na kuwasihi kwamba mwitetee imani iliyokabidhiwa watakatifu kwa nafasi moja itoshayo. 4Kwa kuwa kuna watu waliojipenyeza kwa siri kati yenu, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, waovu, wanaopotosha neema ya Mungu, na kuifanya kuwa ruhusa ya kutenda maovu, wakimkana Isa Al-Masihi, ambaye pekee ni Mtawala wetu mkuu na Bwana wetu.
Hukumu kwa walimu wa uongo
5Ingawa mmekwisha kujua haya yote, nataka niwakumbushe kuwa Mwenyezi Mungu, akiisha kuwaokoa watu wake kutoka nchi ya Misri, baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini. 6Nao malaika ambao hawakulinda nafasi zao, lakini wakayaacha makao yao, hawa amewaweka katika giza, wakiwa wamefungwa kwa minyororo ya milele kwa ajili ya hukumu Siku ile kuu. 7Vivyo hivyo, Sodoma na Gomora na pia ile miji iliyokuwa kandokando, ambayo kwa jinsi moja na hao, walijifurahisha kwa uasherati na kufuata tamaa za mwili zisizo za asili, waliwekwa wawe mfano kwa kuadhibiwa katika moto wa milele.
8Vivyo hivyo, hawa waotao ndoto huutia mwili unajisi, hukataa kuwa chini ya mamlaka na kunena mabaya juu ya wenye mamlaka. 9Lakini hata malaika mkuu Mikaeli alipokuwa anashindana na ibilisi kuhusu mwili wa Musa, hakuthubutu kumlaumu, bali alimwambia, “Mwenyezi Mungu na akukemee!” 10Lakini watu hawa hunena mabaya dhidi ya mambo wasiyoyafahamu. Na katika mambo yale wanayoyafahamu kwa hisia kama wanyama wasio na akili, hayo ndiyo hasa yatakayowaangamiza.
11Ole wao! Kwa kuwa wanaifuata njia ya Kaini, wamekimbilia faida katika kosa la Balaamu na kuangamia katika uasi wa Kora.
12Watu hawa ni dosari katika karamu zenu za upendo, wakila pamoja nanyi bila hofu, wakijilisha wenyewe tu. Wao ni mawingu yasiyokuwa na maji, yakichukuliwa na upepo, miti isiyo na matunda wakati wa mapukutiko, ambayo hunyauka, iliyokufa mara mbili na kung’olewa kabisa. 13Wao ni mawimbi makali ya bahari, yakitoa povu la aibu yao wenyewe, ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba waliowekewa milele.
14Idrisi, mtu wa saba kuanzia Adamu, alitoa unabii kuhusu watu hawa, akisema: “Tazama, Mwenyezi Mungu anakuja pamoja na maelfu kwa maelfu ya watakatifu wake, 15ili kumhukumu kila mmoja na kuwapatiliza wote wasiomcha Mungu kwa matendo yao yote ya uasi waliyoyatenda, pamoja na maneno yote ya kuchukiza ambayo wenye dhambi wamesema dhidi yake.” 16Watu hawa ni wenye kunung’unika na wenye kutafuta makosa; wao hufuata tamaa zao mbovu; hujisifu kwa maneno makuu, na kuwasifu mno watu wengine kwa faida yao wenyewe.
Maonyo na mausia
17Lakini ninyi wapendwa, kumbukeni yale mitume wa Bwana wetu Isa Al-Masihi waliyotabiri awali. 18Kwa kuwa waliwaambia, “Siku za mwisho kutakuwa na watu wenye kudhihaki, watakaofuata tamaa zao wenyewe za upotovu.” 19Hawa ndio watu wanaowagawanya ninyi, wanaofuata tamaa zao za asili, wala hawana Roho wa Mungu.
20Lakini ninyi wapendwa, jijengeni katika imani yenu iliyo takatifu sana tena ombeni katika Roho wa Mungu. 21Jilindeni katika upendo wa Mungu mkitazamia rehema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi, inayowapeleka katika uzima wa milele.
22Wahurumieni walio na mashaka; 23okoeni wengine kwa kuwanyakua kutoka motoni; nao wengine wahurumieni mkiwa na hofu, mkichukia hata vazi lenye mawaa na kutiwa unajisi na mwili.
Dua la kutakia heri
24Kwake yeye awezaye kuwalinda ninyi msianguke na kuwaleta mbele za utukufu wake mkuu bila dosari na kwa furaha ipitayo kiasi: 25kwake yeye Mungu pekee Mwokozi wetu, kwa Isa Al-Masihi Bwana wetu, utukufu, ukuu, uweza na mamlaka ni vyake tangu milele, sasa na hata milele! Amen.

Iliyochaguliwa sasa

Yuda 1: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia