Yuda 1:5-16
Yuda 1:5-16 NENO
Ingawa mmekwisha kujua haya yote, nataka niwakumbushe kuwa Mwenyezi Mungu, akiisha kuwaokoa watu wake kutoka nchi ya Misri, baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini. Nao malaika ambao hawakulinda nafasi zao, lakini wakayaacha makao yao, hawa amewaweka katika giza, wakiwa wamefungwa kwa minyororo ya milele kwa ajili ya hukumu Siku ile kuu. Vivyo hivyo, Sodoma na Gomora na pia ile miji iliyokuwa kandokando, ambayo kwa jinsi moja na hao, walijifurahisha kwa uasherati na kufuata tamaa za mwili zisizo za asili, waliwekwa wawe mfano kwa kuadhibiwa katika moto wa milele. Vivyo hivyo, hawa waotao ndoto huutia mwili unajisi, hukataa kuwa chini ya mamlaka na kunena mabaya juu ya wenye mamlaka. Lakini hata malaika mkuu Mikaeli alipokuwa anashindana na ibilisi kuhusu mwili wa Musa, hakuthubutu kumlaumu, bali alimwambia, “Mwenyezi Mungu na akukemee!” Lakini watu hawa hunena mabaya dhidi ya mambo wasiyoyafahamu. Na katika mambo yale wanayoyafahamu kwa hisia kama wanyama wasio na akili, hayo ndiyo hasa yatakayowaangamiza. Ole wao! Kwa kuwa wanaifuata njia ya Kaini, wamekimbilia faida katika kosa la Balaamu na kuangamia katika uasi wa Kora. Watu hawa ni dosari katika karamu zenu za upendo, wakila pamoja nanyi bila hofu, wakijilisha wenyewe tu. Wao ni mawingu yasiyokuwa na maji, yakichukuliwa na upepo, miti isiyo na matunda wakati wa mapukutiko, ambayo hunyauka, iliyokufa mara mbili na kung’olewa kabisa. Wao ni mawimbi makali ya bahari, yakitoa povu la aibu yao wenyewe, ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba waliowekewa milele. Idrisi, mtu wa saba kuanzia Adamu, alitoa unabii kuhusu watu hawa, akisema: “Tazama, Mwenyezi Mungu anakuja pamoja na maelfu kwa maelfu ya watakatifu wake, ili kumhukumu kila mmoja na kuwapatiliza wote wasiomcha Mungu kwa matendo yao yote ya uasi waliyoyatenda, pamoja na maneno yote ya kuchukiza ambayo wenye dhambi wamesema dhidi yake.” Watu hawa ni wenye kunung’unika na wenye kutafuta makosa; wao hufuata tamaa zao mbovu; hujisifu kwa maneno makuu, na kuwasifu mno watu wengine kwa faida yao wenyewe.