Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yuda 1:5-16

Yuda 1:5-16 Biblia Habari Njema (BHN)

Sasa nataka kuwakumbusheni mambo fulani, ingawaje haya mlikwisha fahamishwa kikamilifu mara moja: Kumbukeni jinsi Bwana alivyowaokoa watu wa Israeli na kuwatoa katika nchi ya Misri, lakini baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini. Na, malaika ambao hawakuridhika na cheo chao, wakayaacha makao yao ya asili, Mungu amewafunga gizani kwa minyororo ya milele wahukumiwe siku ile kuu. Kumbukeni pia Sodoma na Gomora, na miji ya kandokando yake; wenyeji wake walifanya kama wale malaika; walifanya uzinzi na mambo yaliyo kinyume cha maumbile, wakapewa hukumu ya moto wa milele, iwe onyo kwa watu wote. Hivyo ndivyo pia walivyo watu hawa. Ndoto zao huwaongoza katika kuichafua miili yao wenyewe, kuyadharau mamlaka ya Mungu na kuvitukana viumbe vitukufu vya huko juu. Hata Mikaeli, malaika mkuu, hakufanya hivyo. Katika ule ubishi kati yake na Ibilisi juu ya mwili wa Mose, Mikaeli hakuthubutu kumhukumu Ibilisi kwa matusi, ila alisema: “Bwana mwenyewe na akukaripie.” Lakini watu hawa hutukana chochote wasichokielewa; wataangamizwa kwa mambo yaleyale wanayoyajua kwa silika kama wajuavyo wanyama wasio na akili. Ole wao! Watu hao wamefuata mwenendo uleule wa Kaini. Kwa ajili ya fedha, wamejiingiza katika mkosi uleule wa Balaamu. Wameasi kama Kora alivyoasi na wameangamizwa kama yeye alivyoangamizwa. Kwa makelele yao yasiyo na adabu, na kwa kujipendelea wao wenyewe, watu hao ni kama madoa machafu kwenye karamu mnazoshiriki kwa upendo. Wako kama mawingu yasiyo na mvua yanayopeperushwa na upepo. Wao ni kama miti iliyopukutika isiyozaa matunda, iliyokufa kabisa, iliyong'olewa. Watu hao ni kama mawimbi makali ya bahari, na matendo yao ya aibu yanatoka kama povu. Wao ni kama nyota zinazotangatanga ambazo zimewekewa milele mahali pa giza kuu. Naye Henoki, ambaye ni babu wa saba tangu Adamu, alibashiri hivi juu ya watu hao: “Sikilizeni! Bwana anakuja pamoja na maelfu ya malaika wake watakatifu kuwahukumu watu wote, na kuwaadhibu wote wasiomcha Mungu kwa ajili ya matendo yao yote maovu waliyotenda bila kumjali Mungu, na kwa ajili ya maneno yote mabaya ambayo watu waovu walimkashifu nayo.” Watu hawa hunung'unika daima, hulalamika, hufuata tamaa zao mbaya, hujigamba na kuwasifu watu wengine mno kwa faida yao wenyewe.

Shirikisha
Soma Yuda 1

Yuda 1:5-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Tena napenda kuwakumbusha, ijapokuwa mmekwisha kujua haya yote, ya kwamba Bwana, akiisha kuwaokoa watu katika nchi ya Misri, aliwaangamiza baadaye wale wasioamini. Na malaika wasioilinda enzi yao wenyewe, lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu, amewaweka katika vifungo vya milele chini ya giza kwa hukumu ya siku ile kuu. Kama vile Sodoma na Gomora na miji iliyokuwa kandokando, waliofuata uasherati kwa jinsi moja na hawa, wakaenda kufuata mambo ya mwili yasiyo ya asili, imewekwa kuwa dalili, wakiadhibiwa katika moto wa milele. Kadhalika na hawa, katika kuota kwao, huutia mwili uchafu, hukataa kutawaliwa, na kuyatukana matukufu. Lakini Mikaeli, malaika mkuu, aliposhindana na Ibilisi, na kuhojiana naye kwa ajili ya mwili wa Musa, hakuthubutu kumshitaki kwa kumlaumu, bali alisema, Bwana na akukemee. Lakini watu hawa huyatukana mambo wasiyoyajua, na mambo wayatambuayo kwa asili wajiharibu kwayo kama wanyama wasio na akili. Ole wao! Kwa sababu walikwenda katika njia ya Kaini, na kulifuata kosa la Balaamu pasipo kujizuia, kwa ajili ya malipo, nao wameangamia katika maasi ya Kora. Watu hawa ni miamba yenye hatari katika karamu zenu za upendo walapo karamu pamoja nanyi, wakijilisha pasipo hofu; ni mawingu yasiyo na maji, yachukuliwayo na upepo; ni miti iliyopukutika, isiyo na matunda, iliyokufa mara mbili, na kung'olewa kabisa; ni mawimbi ya bahari yasiyozuilika, yakitoa aibu yao wenyewe kama povu; ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba yao waliowekewa milele. Na Henoko, mtu wa kizazi cha saba toka kwa Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana yuaja na watakatifu wake, maelfu kwa maelfu, ili afanye hukumu juu ya watu wote, na kuwaadhibu wote wasiomcha Mungu, kwa ajili ya kazi zao zote za upotevu walizozitenda bila kumcha Mungu, na kwa ajili ya maneno yote maovu ambayo hao wenye dhambi wasiomcha Mungu wameyanena juu yake. Watu hawa ni wenye kunung'unika, wenye kulalamika, waendao kwa tamaa zao, na vinywa vyao vyanena maneno makuu mno ya kiburi, wakipendelea watu wenye cheo kwa ajili ya faida.

Shirikisha
Soma Yuda 1

Yuda 1:5-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Tena napenda kuwakumbusha, ijapokuwa mmekwisha kujua haya yote, ya kwamba Bwana, akiisha kuwaokoa watu katika nchi ya Misri, aliwaangamiza baadaye wale wasioamini. Na malaika wasioilinda enzi yao wenyewe, lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu, amewaweka katika vifungo vya milele chini ya giza kwa hukumu ya siku ile kuu. Kama vile Sodoma na Gomora na miji iliyokuwa kando-kando, waliofuata uasherati kwa jinsi moja na hawa, wakaenda kufuata mambo ya mwili yasiyo ya asili, imewekwa kuwa dalili, wakiadhibiwa katika moto wa milele. Kadhalika na hawa, katika kuota kwao, huutia mwili uchafu, hukataa kutawaliwa, na kuyatukana matukufu. Lakini Mikaeli, malaika mkuu, aliposhindana na Ibilisi, na kuhojiana naye kwa ajili ya mwili wa Musa, hakuthubutu kumshitaki kwa kumlaumu, bali alisema, Bwana na akukemee. Lakini watu hawa huyatukana mambo wasiyoyajua, na mambo wayatambuayo kwa asili wajiharibu kwayo kama wanyama wasio na akili. Ole wao! Kwa sababu walikwenda katika njia ya Kaini, na kulifuata kosa la Balaamu pasipo kujizuia, kwa ajili ya ujira, nao wameangamia katika maasi ya Kora. Watu hawa ni miamba yenye hatari katika karamu zenu za upendo walapo karamu pamoja nanyi, wakijilisha pasipo hofu; ni mawingu yasiyo na maji, yachukuliwayo na upepo; ni miti iliyopukutika, isiyo na matunda, iliyokufa mara mbili, na kung’olewa kabisa; ni mawimbi ya bahari yasiyozuilika, yakitoa aibu yao wenyewe kama povu; ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba yao waliowekewa milele. Na Henoko, mtu wa saba baada ya Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu, ili afanye hukumu juu ya watu wote, na kuwaadhibisha wote wasiomcha Mungu, kwa ajili ya kazi zao zote za upotevu walizozitenda bila kumcha Mungu, na kwa ajili ya maneno magumu yote ambayo hao wenye dhambi wasiomcha Mungu wameyanena juu yake. Watu hawa ni wenye kunung’unika, wenye kulalamika, waendao kwa tamaa zao, na vinywa vyao vyanena maneno makuu mno ya kiburi, wakipendelea watu wenye cheo kwa ajili ya faida.

Shirikisha
Soma Yuda 1

Yuda 1:5-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ingawa mmekwisha kujua haya yote, nataka niwakumbushe kuwa Bwana akiisha kuwaokoa watu wake kutoka nchi ya Misri, baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini. Nao malaika ambao hawakulinda nafasi zao, lakini wakayaacha makao yao, hawa amewaweka katika giza, wakiwa wamefungwa kwa minyororo ya milele kwa ajili ya hukumu Siku ile kuu. Vivyo hivyo, Sodoma na Gomora na pia ile miji iliyokuwa kandokando, ambayo kwa jinsi moja na hao, walijifurahisha kwa uasherati na kufuata tamaa za mwili zisizo za asili, waliwekwa wawe mfano kwa kuadhibiwa katika moto wa milele. Vivyo hivyo, hawa waotao ndoto huutia mwili unajisi, hukataa kuwa chini ya mamlaka na kunena mabaya juu ya wenye mamlaka. Lakini hata malaika mkuu Mikaeli alipokuwa anashindana na ibilisi juu ya mwili wa Mose, hakuthubutu kumlaumu, bali alimwambia, “Bwana na akukemee!” Lakini watu hawa hunena mabaya dhidi ya mambo wasiyoyafahamu. Na katika mambo yale wanayoyafahamu kwa hisia kama wanyama wasio na akili, hayo ndiyo hasa yanayowaharibu. Ole wao! Kwa kuwa wanaifuata njia ya Kaini, wamekimbilia faida katika kosa la Balaamu na kuangamia katika uasi wa Kora. Watu hawa ni dosari katika karamu zenu za upendo, wakila pamoja nanyi bila hofu, wakijilisha pasipo hofu. Wao ni mawingu yasiyokuwa na maji, yakichukuliwa na upepo, miti isiyo na matunda wakati wa mapukutiko, ambayo hunyauka, iliyokufa mara mbili na kungʼolewa kabisa. Wao ni mawimbi makali ya bahari, yakitoa povu la aibu yao wenyewe, ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba waliowekewa milele. Enoki, mtu wa saba kuanzia Adamu alitoa unabii kuhusu watu hawa, akisema: “Tazama, Bwana anakuja pamoja na maelfu kwa maelfu ya watakatifu wake, ili kumhukumu kila mmoja na kuwapatiliza wote wasiomcha Mungu kwa matendo yao yote ya uasi waliyoyatenda, pamoja na maneno yote ya kuchukiza ambayo wenye dhambi wamesema dhidi yake.” Watu hawa ni wenye kunungʼunika na wenye kutafuta makosa; wao hufuata tamaa zao mbaya, hujisifu kwa maneno makuu kuhusu wao wenyewe na kuwasifu mno watu wenye vyeo kwa ajili ya kujipatia faida.

Shirikisha
Soma Yuda 1