Ayubu 31:13-23
Ayubu 31:13-23 NEN
“Kama ningewanyima haki watumishi wangu wanaume au vijakazi wangu, walipokuwa na manungʼuniko dhidi yangu, nitafanya nini Mungu atakaponikabili? Nitamjibu nini nitakapoitwa kutoa hesabu? Je, yeye aliyeniumba tumboni mwa mama yangu, si ndiye aliwaumba? Je, si ni yeye huyo mmoja aliyetuumba sote ndani ya mama zetu? “Ikiwa nimewanyima maskini haja zao, au kuyaacha macho ya wajane yadhoofike, kama nimekula chakula changu mwenyewe, bila kuwashirikisha yatima; lakini tangu ujana wangu nimemlea yatima kama ambavyo baba angefanya, nami tangu kuzaliwa kwangu nimewaongoza wajane: kama nilimwona yeyote akiteseka kwa kukosa nguo, au mtu mhitaji asiye na mavazi ambaye wala moyo wake haukunibariki kwa kumpatia joto kwa mavazi ya manyoya ya kondoo zangu, na kama nimeinua mkono wangu dhidi ya yatima, nikijua kuwa nina ushawishi mahakamani, basi mkono wangu na unyofoke toka begani mwangu, nao na uvunjike kutoka kiungio chake. Kwa kuwa niliogopa uharibifu kutoka kwa Mungu, nami kwa kuuogopa utukufu wake sikuweza kufanya mambo kama hayo.