Yobu 31:13-23
Yobu 31:13-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kama nimeidharau kesi ya mtumishi wangu, au ya kijakazi changu, Waliposhindana nami; Basi Mungu atakapoinuka nitafanya nini? Naye atakapozuru, nitamjibuje? Je! Huyo aliyenifanya mimi ndani ya tumbo, siye aliyemfanya na yeye? Si yeye mmoja aliyetufinyanga tumboni? Ikiwa nimewanyima maskini haja zao, Au kama nimeyatia kiwi macho ya mwanamke mjane; Au kama nimekula tonge langu peke yangu, Mayatima wasipate kulila; (La, tangu ujana wangu alikuwa pamoja nami kama kwa baba; Nami nimekuwa ni kiongozi wa mjane tangu tumbo la mamangu); Ikiwa nimemwona mtu kuangamia kwa kukosa nguo, Au wahitaji kukosa mavazi; Ikiwa viuno vyake havikunibariki, Au kama hakupata moto kwa manyoya ya kondoo wangu; Ikiwa nimewainulia mayatima mkono, Nilipoona msaada wangu langoni; Basi bega langu na lianguke kutoka mahali pake, Na mkono wangu uvunjike mfupani mwake. Kwani msiba utokao kwa Mungu ulikuwa na kitisho kwangu, Na kwa sababu ya ukuu wake sikuweza kufanya neno.
Yobu 31:13-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Kama ningewanyima haki watumishi wangu wanaume au vijakazi wangu, walipokuwa na manungʼuniko dhidi yangu, nitafanya nini Mungu atakaponikabili? Nitamjibu nini nitakapoitwa kutoa hesabu? Je, yeye aliyeniumba tumboni mwa mama yangu, si ndiye aliwaumba? Je, si ni yeye huyo mmoja aliyetuumba sote ndani ya mama zetu? “Ikiwa nimewanyima maskini haja zao, au kuyaacha macho ya wajane yadhoofike, kama nimekula chakula changu mwenyewe, bila kuwashirikisha yatima; lakini tangu ujana wangu nimemlea yatima kama ambavyo baba angefanya, nami tangu kuzaliwa kwangu nimewaongoza wajane: kama nilimwona yeyote akiteseka kwa kukosa nguo, au mtu mhitaji asiye na mavazi ambaye wala moyo wake haukunibariki kwa kumpatia joto kwa mavazi ya manyoya ya kondoo zangu, na kama nimeinua mkono wangu dhidi ya yatima, nikijua kuwa nina ushawishi mahakamani, basi mkono wangu na unyofoke toka begani mwangu, nao na uvunjike kutoka kiungio chake. Kwa kuwa niliogopa uharibifu kutoka kwa Mungu, nami kwa kuuogopa utukufu wake sikuweza kufanya mambo kama hayo.
Yobu 31:13-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Kama nimekataa kesi ya mtumishi wangu wa kiume au wa kike, waliponiletea malalamiko yao, nitafanya nini basi Mungu atakaponikabili? Je, akinichunguza nitamjibu nini? Maana Mungu ndiye aliyeniumba mimi na mtumishi wangu; yeye ndiye aliyetuumba sisi wote. “Je, nimepata kumnyima maskini mahitaji yake au kuwafanya wajane watumaini bure? Je, nimekula chakula changu peke yangu, bila kuwaachia yatima nao wapate chochote? La! Tangu ujana wangu nimekuwa mlezi wao, tangu utoto wangu nimewaongoza wajane. Je, nilimwona mtu anakufa kwa kukosa nguo, au maskini ambaye hana nguo ya kuvaa, bila kumpa joto kwa mavazi ya manyoya ya kondoo wangu naye akanitakia baraka za shukrani ya moyo? Kama nimenyosha mkono mahakamani dhidi ya yatima, nikijua nitapendelewa na mahakimu, basi, bega langu na lingoke, mkono wangu na ukwanyuke kiwikoni mwake. Maana maafa kutoka kwa Mungu ni kitisho kwangu; mimi siwezi kuukabili ukuu wake.
Yobu 31:13-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kama nimeidharau daawa ya mtumishi wangu, au ya kijakazi changu, Waliposhindana nami; Basi Mungu atakapoinuka nitafanya nini? Naye atakapozuru, nitamjibuje? Je! Huyo aliyenifanya mimi ndani ya tumbo, siye aliyemfanya na yeye? Si yeye mmoja aliyetufinyanga tumboni? Ikiwa nimewanyima maskini haja zao, Au kama nimeyatia kiwi macho ya mwanamke mjane; Au kama nimekula tonge langu peke yangu, Mayatima wasipate kulila; (La, tangu ujana wangu alikua pamoja nami kama kwa baba; Nami nimekuwa ni kiongozi cha mjane tangu tumbo la mamangu); Ikiwa nimemwona mtu kuangamia kwa kukosa nguo, Au wahitaji kukosa mavazi; Ikiwa viuno vyake havikunibarikia, Au kama hakupata moto kwa manyoya ya kondoo zangu; Ikiwa nimewainulia mayatima mkono, Nilipoona msaada wangu langoni; Basi bega langu na lianguke kutoka mahali pake, Na mkono wangu uvunjike mfupani mwake. Kwani msiba utokao kwa Mungu ulikuwa na kitisho kwangu, Na kwa sababu ya ukuu wake sikuweza kufanya neno.