Ayubu 31:1-12
Ayubu 31:1-12 NEN
“Nimefanya agano na macho yangu yasimtazame msichana kwa kumtamani. Kwa kuwa fungu la mwanadamu ni gani kutoka kwa Mungu juu, urithi wake kutoka kwa Mungu Mwenye Nguvu Aliye juu? Je, si uharibifu kwa watu waovu, maangamizi kwa wale watendao mabaya? Je, yeye hazioni njia zangu na kuihesabu kila hatua yangu? “Kama nimeishi katika uongo au mguu wangu umekimbilia udanganyifu, Mungu na anipime katika mizani za uaminifu, naye atajua kwamba sina hatia: kama hatua zangu zimepotoka kutoka kwenye njia, kama moyo wangu umeongozwa na macho yangu, au kama mikono yangu imetiwa unajisi, basi wengine na wale nilichokipanda, nayo yale yote niliyootesha na yangʼolewe. “Kama moyo wangu umeshawishiwa na mwanamke, au kama nimevizia mlangoni mwa jirani yangu, basi mke wangu na asage nafaka ya mwanaume mwingine, nao wanaume wengine walale naye. Kwa kuwa hilo lingekuwa aibu, naam, dhambi ya kuhukumiwa. Ni moto uwakao kwa Uharibifu; ungekuwa umengʼoa mavuno yangu.