Ayubu 29:11-25
Ayubu 29:11-25 NEN
Yeyote aliyenisikia alinena mema juu yangu, nao walioniona walinisifu, kwa sababu nilimwokoa maskini aliyeomba msaada, naye yatima aliyekuwa hana wa kumsaidia. Mtu aliyekuwa karibu kufa alinibariki, nami niliufanya moyo wa mjane kuimba. Niliivaa haki kama vazi langu; uadilifu ulikuwa joho langu na kilemba changu. Nilikuwa macho ya kipofu na miguu kwa kiwete. Nilikuwa baba kwa mhitaji; nilimtetea mgeni. Niliyavunja meno makali ya waovu, na kuwapokonya wahanga kwenye meno yao. “Nikafikiri, ‘Nitafia katika nyumba yangu mwenyewe, nazo siku zangu zitakuwa nyingi kama chembechembe za mchanga. Mizizi yangu itafika mpaka kwenye maji, nao umande utakaa juu ya matawi yangu usiku kucha. Utukufu wangu utabakia kuwa mpya ndani yangu, upinde wangu daima utaendelea kuwa mpya mkononi mwangu.’ “Watu walinisikiliza kwa tumaini, wakingojea ushauri wangu kwa utulivu. Baada ya mimi kuzungumza, hawakusema zaidi; maneno yangu yaliingia masikioni mwao kwa makini. Waliningojea kama manyunyu ya mvua na kuyapokea maneno yangu kama ardhi inyonyavyo mvua ya vuli. Walipokata tamaa niliwaonyesha uso wa furaha; nuru ya uso wangu ilikuwa ya thamani kwao. Niliwachagulia njia na kukaa kama mkuu wao; niliishi kama mfalme katikati ya majeshi yake; nikawa kama yeye anayewafariji waombolezaji.