Ayubu 27:1-12
Ayubu 27:1-12 NEN
Ndipo Ayubu akaendelea na hoja yake, akasema: “Hakika kama Mungu aishivyo, aliyeninyima haki yangu, Mwenyezi ambaye amenifanya nionje uchungu wa nafsi, kwa muda wote nitakaokuwa na uhai ndani yangu, nayo pumzi ya Mungu ikiwa puani mwangu, midomo yangu haitanena uovu, wala ulimi wangu hautatamka udanganyifu. Sitakubaliana nanyi kabisa kuwa mko sahihi; hadi nife, sitakana uadilifu wangu. Nitadumisha haki yangu wala sitaiacha; dhamiri yangu haitanisuta muda wote ninaoishi. “Watesi wangu wawe kama waovu, nao adui zangu wawe kama wasio haki! Kwa maana mtu asiyemcha Mungu analo tegemeo gani anapokatiliwa mbali, Mungu anapouondoa uhai wake? Je, Mungu husikiliza kilio chake, shida zimjiapo? Je, anaweza kumfurahia Mwenyezi? Je, atamwita Mungu nyakati zote? “Nitawafundisha juu ya uweza wa Mungu; njia za Mwenyezi sitazificha. Ninyi nyote mmeona hili wenyewe. Ni ya nini basi mazungumzo haya yasiyo na maana?