Ayubu 26:5-14
Ayubu 26:5-14 NEN
“Wafu wako katika maumivu makuu, wale walio chini ya maji na wale waishio ndani yake. Mauti iko wazi mbele za Mungu; Uharibifu haukufunikwa. Hutandaza anga la kaskazini mahali patupu; naye huiningʼiniza dunia mahali pasipo na kitu. Huyafungia maji kwenye mawingu yake, hata hivyo mawingu hayapasuki kwa uzito wake. Huufunika uso wa mwezi mpevu, akitandaza mawingu juu yake. Amechora mstari wa upeo juu ya uso wa maji, ameweka mpaka wa nuru na giza. Nguzo za mbingu nazo zatetemeka, zinatishika anapozikemea. Kwa nguvu zake aliisukasuka bahari; kwa hekima yake alimkata Rahabu vipande vipande. Aliisafisha anga kwa pumzi yake; kwa mkono wake alimchoma joka aendaye mbio. Haya ni mambo madogo tu katika matendo yake; tazama jinsi ulivyo mdogo mnongʼono tunaousikia kumhusu! Ni nani basi awezaye kuelewa ngurumo za nguvu zake?”