Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 8:31-51

Yohana 8:31-51 NEN

Kisha Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkidumu katika maneno yangu, mtakuwa wanafunzi wangu kweli kweli. Ndipo mtaijua kweli nayo kweli itawaweka huru.” Wao wakamjibu, “Sisi tu wazao wa Abrahamu, nasi hatujawa watumwa wa mtu yeyote. Wawezaje kusema kwamba tutawekwa huru?” Yesu akajibu, “Amin, amin nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Mtumwa hakai nyumbani anakotumika siku zote, lakini mwana hukaa nyumbani daima. Hivyo Mwana akiwaweka huru mtakuwa huru kweli kweli. Ninajua ya kuwa ninyi ni wazao wa Abrahamu, lakini mnatafuta wasaa wa kuniua kwa sababu ndani yenu hamna nafasi ya neno langu. Ninasema yale niliyoyaona mbele za Baba yangu, nanyi inawapa kufanya yale mliyosikia kutoka kwa baba yenu.” Wakajibu, “Baba yetu ni Abrahamu.” Yesu akawaambia, “Kama mngekuwa wazao wa Abrahamu mngefanya mambo yale aliyofanya Abrahamu. Lakini sasa ninyi mnatafuta kuniua, mtu ambaye nimewaambia kweli ile niliyosikia kutoka kwa Mungu, Abrahamu hakufanya jambo la namna hii. Ninyi mnafanya mambo afanyayo baba yenu.” Wakamjibu, “Sisi hatukuzaliwa kwa uzinzi. Tunaye Baba mmoja, Mungu pekee.” Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda, kwa maana nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, ila yeye alinituma. Kwa nini hamwelewi ninayowaambia? Ni kwa sababu hamwezi kusikia nisemacho. Ninyi ni watoto wa baba yenu ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli maana hamna kweli ndani yake. Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo. Lakini kwa sababu nimewaambia kweli hamkuniamini! Je, kuna yeyote miongoni mwenu awezaye kunithibitisha kuwa mwenye dhambi? Kama nawaambia yaliyo kweli, mbona hamniamini? Yeye atokaye kwa Mungu husikia kile Mungu asemacho. Sababu ya ninyi kutosikia ni kwa kuwa hamtokani na Mungu.” Wayahudi wakamjibu Yesu, “Je, hatuko sahihi tunaposema ya kwamba wewe ni Msamaria na ya kwamba una pepo mchafu?” Yesu akawajibu, “Mimi sina pepo mchafu, bali ninamheshimu Baba yangu, nanyi mnanidharau. Lakini mimi sitafuti utukufu wangu mwenyewe, bali yuko anayetaka kunitukuza, naye ndiye mwamuzi. Amin, amin nawaambia, mtu yeyote akilitii neno langu hataona mauti milele.”