Yohane 8:31-51
Yohane 8:31-51 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkiyazingatia mafundisho yangu mtakuwa kweli wanafunzi wangu. Mtaujua ukweli, nao ukweli utawapeni uhuru.” Nao wakamjibu, “Sisi ni wazawa wa Abrahamu, na hatujapata kamwe kuwa watumwa wa mtu yeyote yule. Una maana gani unaposema: ‘Mtakuwa huru?’” Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, kila mtu anayetenda dhambi ni mtumwa wa dhambi. Mtumwa hana makao ya kudumu nyumbani, lakini mwana anayo makao ya kudumu. Mwana akiwapeni uhuru mtakuwa huru kweli. Najua kwamba nyinyi ni wazawa wa Abrahamu. Hata hivyo, mnataka kuniua kwa sababu hamyakubali mafundisho yangu. Mimi nasema yale aliyonionesha Baba, lakini nyinyi mwafanya yale aliyowaambieni baba yenu.” Wao wakamjibu, “Sisi ni watoto wa Abrahamu!” Yesu akawaambia, “Kama nyinyi mngekuwa watoto wa Abrahamu, mngefanya kama alivyofanya Abrahamu. Mimi nimewaambieni ukweli niliousikia kwa Mungu; hata hivyo, nyinyi mwataka kuniua. Abrahamu hakufanya hivyo! Nyinyi mnafanya mambo yaleyale aliyofanya baba yenu.” Wao wakamwambia, “Sisi si watoto haramu! Tunaye baba mmoja tu, yaani Mungu.” Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi, maana mimi nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila yeye alinituma. Kwa nini hamuelewi hayo ninayosema? Ni kwa kuwa hamwezi kuusikiliza ujumbe wangu. Nyinyi ni watoto wa baba yenu Ibilisi na mnataka tu kutekeleza tamaa za baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; hana msimamo katika ukweli, kwani ukweli haumo ndani yake. Kila asemapo uongo, husema kutokana na hali yake ya maumbile, maana yeye ni mwongo na baba wa uongo. Mimi nasema ukweli, na ndiyo maana nyinyi hamniamini. Nani kati yenu awezaye kuthibitisha kuwa mimi nina dhambi? Ikiwa basi nasema ukweli, kwa nini hamniamini? Aliye wa Mungu husikiliza maneno ya Mungu. Lakini nyinyi hamsikilizi kwa sababu nyinyi si watu wa Mungu.” Wayahudi wakamwambia, “Je, hatukusema kweli kwamba wewe ni Msamaria, na tena una pepo?” Yesu akajibu, “Mimi sina pepo; mimi namheshimu Baba yangu, lakini nyinyi hamniheshimu. Mimi sijitafutii utukufu wangu mwenyewe; yuko mmoja mwenye kuutafuta utukufu huo, naye ni hakimu. Kweli nawaambieni, anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele.”
Yohane 8:31-51 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru. Wakamjibu, Sisi tu uzao wake Abrahamu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wowote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru? Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Wala mtumwa hakai nyumbani sikuzote; mwana hukaa sikuzote. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. Najua ya kuwa ninyi ni uzao wa Abrahamu lakini mnatafuta kuniua kwa sababu neno langu halimo ndani yenu. Niliyoyaona kwa Baba ndiyo niyanenayo; nanyi vivyo hivyo mliyoyasikia kwa baba yenu ndiyo myatendayo. Wakajibu, wakamwambia, Baba yetu ndiye Abrahamu! Yesu akawaambia, Kama mngekuwa watoto wa Abrahamu, mngezitenda kazi zake Abrahamu. Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli, niliyoisikia kwa Mungu. Abrahamu hakufanya hivyo. Ninyi mnazitenda kazi za baba yenu. Ndipo walipomwambia, Sisi hatukuzaliwa kwa zinaa; sisi tunaye Baba mmoja, yaani, Mungu. Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nilitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma. Mbona hamyafahamu hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamuwezi kulisikia neno langu. Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa uongo. Nami, kwa sababu nasema iliyo kweli, hamnisadiki. Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi? Nami nikisema kweli, mbona ninyi hamnisadiki? Yeye aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu; hivyo ninyi hamsikii kwa sababu ninyi si wa Mungu. Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Je! Sisi hatusemi vema ya kwamba wewe u Msamaria, nawe una pepo? Yesu akajibu, Mimi sina pepo; lakini mimi namheshimu Baba yangu, na ninyi mwanivunjia heshima yangu. Wala mimi siutafuti utukufu wangu; kuna yule autafutaye na ndiye hakimu. Amin, amin, nawaambia, Mtu akilishika neno langu, hataona mauti milele.
Yohane 8:31-51 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru. Wakamjibu, Sisi tu uzao wake Ibrahimu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wo wote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru? Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Wala mtumwa hakai nyumbani sikuzote; mwana hukaa sikuzote. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. Najua ya kuwa ninyi ni uzao wa Ibrahimu lakini mnatafuta kuniua kwa sababu neno langu halimo ndani yenu. Niliyoyaona kwa Baba ndiyo niyanenayo; nanyi vivyo hivyo mliyoyasikia kwa baba yenu ndiyo myatendayo. Wakajibu, wakamwambia, Baba yetu ndiye Ibrahimu! Yesu akawaambia, Kama mngekuwa watoto wa Ibrahimu, mngezitenda kazi zake Ibrahimu. Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli, niliyoisikia kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya hivyo. Ninyi mnazitenda kazi za baba yenu. Ndipo walipomwambia, Sisi hatukuzaliwa kwa zinaa; sisi tunaye Baba mmoja, yaani, Mungu. Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma. Mbona hamyafahamu hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamwezi kulisikia neno langu. Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo. Nami, kwa sababu nasema iliyo kweli, hamnisadiki. Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi? Nami nikisema kweli, mbona ninyi hamnisadiki? Yeye aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu; hivyo ninyi hamsikii kwa sababu ninyi si wa Mungu. Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Je! Sisi hatusemi vema ya kwamba wewe u Msamaria, nawe una pepo? Yesu akajibu, Mimi sina pepo; lakini mimi namheshimu Baba yangu, na ninyi mwanivunjia heshima yangu. Wala mimi siutafuti utukufu wangu; yuko mwenye kutafuta na kuhukumu. Amin, amin, nawaambia, Mtu akilishika neno langu, hataona mauti milele.
Yohane 8:31-51 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkidumu katika maneno yangu, mtakuwa wanafunzi wangu kweli kweli. Ndipo mtaijua kweli nayo kweli itawaweka huru.” Wao wakamjibu, “Sisi tu wazao wa Abrahamu, nasi hatujawa watumwa wa mtu yeyote. Wawezaje kusema kwamba tutawekwa huru?” Yesu akajibu, “Amin, amin nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Mtumwa hakai nyumbani anakotumika siku zote, lakini mwana hukaa nyumbani daima. Hivyo Mwana akiwaweka huru mtakuwa huru kweli kweli. Ninajua ya kuwa ninyi ni wazao wa Abrahamu, lakini mnatafuta wasaa wa kuniua kwa sababu ndani yenu hamna nafasi ya neno langu. Ninasema yale niliyoyaona mbele za Baba yangu, nanyi inawapa kufanya yale mliyosikia kutoka kwa baba yenu.” Wakajibu, “Baba yetu ni Abrahamu.” Yesu akawaambia, “Kama mngekuwa wazao wa Abrahamu mngefanya mambo yale aliyofanya Abrahamu. Lakini sasa ninyi mnatafuta kuniua, mtu ambaye nimewaambia kweli ile niliyosikia kutoka kwa Mungu, Abrahamu hakufanya jambo la namna hii. Ninyi mnafanya mambo afanyayo baba yenu.” Wakamjibu, “Sisi hatukuzaliwa kwa uzinzi. Tunaye Baba mmoja, Mungu pekee.” Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda, kwa maana nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, ila yeye alinituma. Kwa nini hamwelewi ninayowaambia? Ni kwa sababu hamwezi kusikia nisemacho. Ninyi ni watoto wa baba yenu ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli maana hamna kweli ndani yake. Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo. Lakini kwa sababu nimewaambia kweli hamkuniamini! Je, kuna yeyote miongoni mwenu awezaye kunithibitisha kuwa mwenye dhambi? Kama nawaambia yaliyo kweli, mbona hamniamini? Yeye atokaye kwa Mungu husikia kile Mungu asemacho. Sababu ya ninyi kutosikia ni kwa kuwa hamtokani na Mungu.” Wayahudi wakamjibu Yesu, “Je, hatuko sahihi tunaposema ya kwamba wewe ni Msamaria na ya kwamba una pepo mchafu?” Yesu akawajibu, “Mimi sina pepo mchafu, bali ninamheshimu Baba yangu, nanyi mnanidharau. Lakini mimi sitafuti utukufu wangu mwenyewe, bali yuko anayetaka kunitukuza, naye ndiye mwamuzi. Amin, amin nawaambia, mtu yeyote akilitii neno langu hataona mauti milele.”