Yohana 7:25-36
Yohana 7:25-36 NENO
Ndipo baadhi ya watu wa Yerusalemu wakawa wanasema, “Tazameni, huyu si yule mtu wanayetaka kumuua? Mbona yuko hapa anazungumza hadharani, na wala hawamwambii neno lolote? Je, inawezekana viongozi wanafahamu kuwa huyu ndiye Kristo? Tunafahamu huyu mtu anakotoka, lakini Kristo atakapokuja, hakuna yeyote atakayejua atokako.” Ndipo Yesu, akaendelea kufundisha Hekaluni, akisema, “Ninyi mnanifahamu na kujua nitokako. Mimi sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, bali yeye aliyenituma ni wa kweli na ninyi hammjui. Mimi namjua kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye alinituma.” Ndipo wakatafuta kumkamata, lakini hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumshika kwa sababu saa yake ilikuwa bado haijawadia. Nao watu wengi wakamwamini, wakasema, “Je, Kristo atakapokuja, atafanya miujiza mikuu kuliko aliyoifanya mtu huyu?” Mafarisayo wakasikia watu wakinongʼona mambo kama hayo kuhusu Yesu, ndipo wao pamoja na viongozi wa makuhani wakatuma walinzi wa Hekalu waende kumkamata. Yesu akasema, “Mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo, kisha nitarudi kwake yeye aliyenituma. Mtanitafuta lakini hamtaniona, nami niliko ninyi hamwezi kuja.” Wayahudi wakaulizana wao kwa wao, “Huyu mtu anataka kwenda wapi ambako hatuwezi kumfuata? Je, anataka kwenda kwa Wayunani ambako baadhi ya watu wetu wametawanyikia, akawafundishe Wayunani? Yeye ana maana gani anaposema, ‘Mtanitafuta lakini hamtaniona,’ na, ‘nami niliko ninyi hamwezi kuja’?”