Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 7:25-36

Yohane 7:25-36 Biblia Habari Njema (BHN)

Baadhi ya watu wa Yerusalemu walisema, “Je, yule mtu wanayemtafuta wamuue si huyu? Tazameni sasa! Anawaonya hadharani, wala hakuna mtu anayemwambia hata neno. Je, yawezekana kuwa viongozi wametambua kweli kwamba huyu ndiye Kristo? Kristo atakapokuja hakuna mtu atakayejua mahali alikotoka, lakini sisi tunajua alikotoka mtu huyu!” Basi, Yesu alipokuwa anafundisha hekaluni alipaza sauti na kusema, “Ati mnanijua; hata nilikotoka mnakujua! Hata hivyo, sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe; ila yeye aliyenituma mimi ni wa kweli, nanyi hamumjui. Lakini mimi namjua kwa sababu nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.” Basi, watu wakataka kumtia nguvuni, lakini hakuna mtu aliyethubutu kumkamata kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado. Wengi katika ule umati wa watu walimwamini, wakasema, “Je, Kristo akija atafanya ishara kubwa zaidi kuliko alizozifanya huyu?” Mafarisayo waliwasikia watu wakinongona maneno hayo juu ya Yesu. Basi, wao pamoja na makuhani wakuu wakawatuma walinzi wamtie nguvuni. Yesu akasema, “Bado niko nanyi kwa muda mfupi, kisha nitamwendea yule aliyenituma. Mtanitafuta lakini hamtaniona, na pale nitakapokuwa nyinyi hamwezi kufika.” Viongozi wa Wayahudi wakasema wao kwa wao, “Mtu huyu atakwenda wapi ambapo hatutaweza kumpata? Atakwenda kwa Wayahudi waliotawanyika kati ya Wagiriki, na kuwafundisha Wagiriki? Ana maana gani anaposema: ‘Mtanitafuta lakini hamtanipata, na pale nitakapokuwa nyinyi hamwezi kufika?’”

Shirikisha
Soma Yohane 7

Yohane 7:25-36 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Ndipo baadhi ya watu wa Yerusalemu wakawa wanasema, “Tazameni, huyu si yule mtu wanayetaka kumuua? Mbona yuko hapa anazungumza hadharani, na wala hawamwambii neno lolote? Je, inawezekana viongozi wanafahamu kuwa huyu ndiye Al-Masihi? Tunafahamu huyu mtu anakotoka, lakini Al-Masihi atakapokuja, hakuna yeyote atakayejua atokako.” Ndipo Isa, akaendelea kufundisha Hekaluni, akisema, “Ninyi mnanifahamu na kujua nitokako. Mimi sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, bali yeye aliyenituma ni wa kweli na ninyi hammjui. Mimi namjua kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye alinituma.” Ndipo wakatafuta kumkamata, lakini hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumshika kwa sababu saa yake ilikuwa bado haijawadia. Nao watu wengi wakamwamini, wakasema, “Je, Al-Masihi atakapokuja, atafanya miujiza mikuu kuliko aliyoifanya mtu huyu?” Mafarisayo wakasikia watu wakinong’ona mambo kama hayo kuhusu Isa, ndipo wao pamoja na viongozi wa makuhani wakatuma walinzi wa Hekalu waende kumkamata. Isa akasema, “Mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo, kisha nitarudi kwake yeye aliyenituma. Mtanitafuta lakini hamtaniona, nami niliko ninyi hamwezi kuja.” Wayahudi wakaulizana wao kwa wao, “Huyu mtu anataka kwenda wapi ambako hatuwezi kumfuata? Je, anataka kwenda kwa Wayunani ambako baadhi ya watu wetu wametawanyikia, akawafundishe Wayunani? Yeye ana maana gani anaposema, ‘Mtanitafuta lakini hamtaniona,’ na, ‘nami niliko ninyi hamwezi kuja’?”

Shirikisha
Soma Yohane 7