Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 6:32-59

Yohana 6:32-59 NEN

Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, si Mose aliyewapa mikate kutoka mbinguni, bali Baba yangu ndiye anawapa mkate wa kweli kutoka mbinguni. Kwa maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.” Wakamwambia, “Bwana, kuanzia sasa tupatie huo mkate siku zote.” Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uzima. Yeye ajaye kwangu, hataona njaa kamwe na yeye aniaminiye, hataona kiu kamwe. Lakini kama nilivyowaambia, mmeniona lakini bado hamwamini. Wale wote anipao Baba watakuja kwangu na yeyote ajaye kwangu, sitamfukuzia nje kamwe. Kwa kuwa nimeshuka kutoka mbinguni si ili kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake yeye aliyenituma. Haya ndiyo mapenzi yake yeye aliyenituma, kwamba, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho. Kwa maana mapenzi ya Baba yangu ni kwamba kila mmoja amtazamaye, Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele, nami nitawafufua siku ya mwisho.” Wayahudi wakaanza kunungʼunika kwa kuwa alisema, “Mimi ndimi mkate ulioshuka kutoka mbinguni.” Wakasema, “Huyu si Yesu, mwana wa Yosefu, ambaye baba yake na mama yake tunawajua? Anawezaje basi sasa kusema, ‘Nimeshuka kutoka mbinguni’?” Hivyo Yesu akawaambia, “Acheni kunungʼunikiana ninyi kwa ninyi. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu kama asipovutwa na Baba aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho. Imeandikwa katika Manabii, ‘Wote watafundishwa na Mungu.’ Yeyote amsikilizaye Baba na kujifunza kutoka kwake, huyo huja kwangu. Hakuna mtu yeyote aliyemwona Baba isipokuwa yeye atokaye kwa Mungu, yeye ndiye peke yake aliyemwona Baba. Amin, amin nawaambia, yeye anayeamini anao uzima wa milele. Mimi ni mkate wa uzima. Baba zenu walikula mana jangwani, lakini wakafa. Lakini hapa kuna mkate utokao mbinguni, ambao mtu yeyote akiula, hatakufa. Mimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni. Mtu yeyote akiula mkate huu, ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu, ambao nitautoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.” Ndipo Wayahudi wakaanza kuhojiana vikali wao kwa wao wakisema, “Mtu huyu awezaje kutupatia mwili wake tuule?” Hivyo Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, msipoula mwili wa Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Mtu yeyote aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, anao uzima wa milele. Nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Yeyote alaye mwili wangu na kunywa damu yangu, atakaa ndani yangu nami nitakaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, na kama nami ninavyoishi kwa sababu ya Baba, hivyo anilaye mimi ataishi kwa sababu yangu. Huu ndio mkate ushukao kutoka mbinguni, si kama ule mkate baba zenu waliokula nao wakafa. Lakini yeye aulaye mkate huu ataishi milele.” Yesu alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika sinagogi huko Kapernaumu.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Yohana 6:32-59