Yohana 21:1-12
Yohana 21:1-12 NEN
Baada ya haya Yesu akawatokea tena wanafunzi wake kando ya Bahari ya Tiberia. Yeye alijionyesha kwao hivi: Simoni Petro, Tomaso aitwaye Didimasi, yaani Pacha, Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, wana wa Zebedayo na wanafunzi wengine wawili walikuwa pamoja. Simoni Petro akawaambia wenzake, “Mimi naenda kuvua samaki.” Nao wakamwambia, “Tutakwenda pamoja nawe.” Wakatoka, wakaingia ndani ya mashua, lakini usiku ule hawakupata chochote. Mara baada ya kupambazuka, Yesu akasimama ufuoni, lakini wanafunzi hawakumtambua kwamba alikuwa Yesu. Yesu akawaambia, “Wanangu, je, mna samaki wowote?” Wakamjibu, “La.” Akawaambia, “Shusheni nyavu upande wa kuume wa mashua yenu nanyi mtapata samaki.” Wakashusha nyavu na tazama wakapata samaki wengi mno hata wakashindwa kuvutia zile nyavu zilizojaa samaki ndani ya mashua. Yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, “Huyu ni Bwana!” Simoni Petro aliposikia haya, akajifunga nguo yake kwa kuwa alikuwa uchi, naye akajitosa baharini. Wale wanafunzi wengine wakaja kwa ile mashua huku wakikokota ule wavu uliyojaa samaki, maana hawakuwa mbali na nchi kavu, ilikuwa yapata dhiraa 200 Walipofika ufuoni, wakaona moto wa makaa na samaki wakiokwa juu yake na mikate. Yesu akawaambia, “Leteni baadhi ya hao samaki mliovua sasa hivi.” Simoni Petro akapanda kwenye mashua na kuukokota ule wavu pwani. Ulikuwa umejaa samaki wakubwa 153. Ingawa samaki walikuwa wengi kiasi hicho, ule wavu haukuchanika. Yesu akawaambia, “Njooni mpate kifungua kinywa.” Hakuna hata mmoja wa wanafunzi aliyethubutu kumuuliza, “Wewe ni nani?” Kwa sababu walijua ya kuwa ni Bwana.