Yohana 21
21
Yesu Awatokea Wanafunzi Saba
1 Baada ya haya Yesu akawatokea tena wanafunzi wake kando ya Bahari ya Tiberia.#21:1 Yaani Bahari ya Galilaya. Yeye alijionyesha kwao hivi: 2 Simoni Petro, Tomaso aitwaye Didimasi, yaani Pacha, Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, wana wa Zebedayo na wanafunzi wengine wawili walikuwa pamoja. 3 Simoni Petro akawaambia wenzake, “Mimi naenda kuvua samaki.” Nao wakamwambia, “Tutakwenda pamoja nawe.” Wakatoka, wakaingia ndani ya mashua, lakini usiku ule hawakupata chochote.
4 Mara baada ya kupambazuka, Yesu akasimama ufuoni, lakini wanafunzi hawakumtambua kwamba alikuwa Yesu.
5 Yesu akawaambia, “Wanangu, je, mna samaki wowote?”
Wakamjibu, “La.”
6 Akawaambia, “Shusheni nyavu upande wa kuume wa mashua yenu nanyi mtapata samaki.” Wakashusha nyavu na tazama wakapata samaki wengi mno hata wakashindwa kuvutia zile nyavu zilizojaa samaki ndani ya mashua.
7 Yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, “Huyu ni Bwana!” Simoni Petro aliposikia haya, akajifunga nguo yake kwa kuwa alikuwa uchi, naye akajitosa baharini. 8Wale wanafunzi wengine wakaja kwa ile mashua huku wakikokota ule wavu uliyojaa samaki, maana hawakuwa mbali na nchi kavu, ilikuwa yapata dhiraa 200#21:8 Dhiraa 200 ni kama mita 90. 9 Walipofika ufuoni, wakaona moto wa makaa na samaki wakiokwa juu yake na mikate.
10Yesu akawaambia, “Leteni baadhi ya hao samaki mliovua sasa hivi.”
11Simoni Petro akapanda kwenye mashua na kuukokota ule wavu pwani. Ulikuwa umejaa samaki wakubwa 153. Ingawa samaki walikuwa wengi kiasi hicho, ule wavu haukuchanika. 12 Yesu akawaambia, “Njooni mpate kifungua kinywa.” Hakuna hata mmoja wa wanafunzi aliyethubutu kumuuliza, “Wewe ni nani?” Kwa sababu walijua ya kuwa ni Bwana. 13 Yesu akaja, akachukua ule mkate, akawapa na vivyo hivyo akawagawia pia wale samaki. 14 Hii ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wanafunzi wake baada yake kufufuliwa kutoka kwa wafu.
Yesu Amuuliza Petro Kama Anampenda
15 Walipokwisha kula, Yesu akamuuliza Simoni Petro, “Je, Simoni mwana wa Yohana, unanipenda kweli kuliko hawa?”
Yeye akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”
Yesu akamwambia, “Lisha wana-kondoo wangu.”
16 Yesu akamwambia tena, “Simoni, mwana wa Yohana, wanipenda?”
Petro akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”
Yesu akamwambia, “Chunga kondoo zangu.”
17 Kwa mara ya tatu Yesu akamuuliza Petro, “Simoni mwana wa Yohana, unanipenda?”
Petro akahuzunika sana kwa kuwa Yesu alimuuliza mara ya tatu, “Unanipenda?” Akamjibu, “Bwana, wewe unajua yote, unajua ya kuwa ninakupenda.”
Yesu akamwambia, “Lisha kondoo wangu. 18Amin, amin nakuambia, ulipokuwa kijana ulivaa na kwenda unakotaka, lakini utakapokuwa mzee utanyoosha mikono yako na mtu mwingine atakuvika na kukupeleka usipotaka kwenda.” 19 Yesu alisema haya ili kuashiria ni kifo cha aina gani Petro atakachomtukuza nacho Mungu. Kisha Yesu akamwambia Petro, “Nifuate!”
20 Petro akageuka, akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akiwafuata. (Huyu ndiye yule mwanafunzi aliyeegama kifuani mwa Yesu walipokula naye chakula cha mwisho na kuuliza, “Bwana, ni nani atakayekusaliti?”) 21Petro alipomwona huyo mwanafunzi, akamuuliza Yesu, “Bwana na huyu je?”
22 Yesu akamjibu, “Ikiwa nataka aishi mpaka nitakaporudi, inakuhusu nini? Wewe inakupasa unifuate!” 23 Kwa sababu ya maneno haya ya Yesu, uvumi ukaenea miongoni mwa ndugu kwamba huyu mwanafunzi hangekufa. Lakini Yesu hakusema kuwa hangekufa. Yeye alisema tu kwamba, “Ikiwa nataka aishi mpaka nitakaporudi, inakuhusu nini?”
24 Huyu ndiye yule mwanafunzi anayeshuhudia mambo haya na ndiye ambaye ameandika habari hizi. Nasi tunajua ya kuwa ushuhuda wake ni kweli.
25 Lakini kuna mambo mengine mengi ambayo Yesu alifanya. Kama yote yangeliandikwa, nadhani hata ulimwengu wote usingekuwa na nafasi ya kutosha kuweka vitabu vyote ambavyo vingeandikwa. Amen.
Iliyochaguliwa sasa
Yohana 21: NEN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.