Yohana 11:1-23
Yohana 11:1-23 NEN
Basi mtu mmoja jina lake Lazaro alikuwa mgonjwa. Yeye alikuwa akiishi Bethania kijiji cha Maria na Martha dada zake. Huyu Maria, ambaye Lazaro kaka yake alikuwa mgonjwa, ndiye yule ambaye alimpaka Bwana mafuta na kuifuta miguu yake kwa nywele zake. Hivyo hawa dada wawili walituma ujumbe kwa Yesu kumwambia, “Bwana, yule umpendaye ni mgonjwa.” Lakini Yesu aliposikia hayo, akasema, “Ugonjwa huu hautaleta mauti bali umetokea ili kudhihirisha utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu apate kutukuzwa kutokana na ugonjwa huu.” Pamoja na hivyo, ingawa Yesu aliwapenda Martha, Maria na Lazaro ndugu yao, baada ya kusikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, aliendelea kukawia huko alikokuwa kwa siku mbili zaidi. Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Haya, turudi Uyahudi.” Wanafunzi wake wakamwambia, “Rabi, Wayahudi walikuwa wanataka kukupiga mawe, nawe unataka kurudi huko?” Yesu akawajibu, “Si kuna saa kumi na mbili za mchana katika siku moja? Wala watembeao mchana hawawezi kujikwaa kwa maana wanaona nuru ya ulimwengu huu. Lakini wale watembeao usiku hujikwaa kwa sababu hakuna nuru ndani yao.” Baada ya kusema haya, Yesu akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini naenda kumwamsha.” Wanafunzi wakamwambia, “Bwana, kama amelala usingizi ataamka.” Hata hivyo, Yesu alikuwa anazungumzia kuwa Lazaro amekufa, lakini wanafunzi wake hawakuelewa, walidhani kwamba anasema Lazaro amelala usingizi tu. Kwa hiyo Yesu akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa. Hata hivyo nafurahi kwa kuwa sikuwepo huko kabla ya Lazaro kufa, ili mpate kuamini. Lakini sasa twendeni kwake.” Tomaso aliyeitwa Pacha akawaambia wanafunzi wenzake, “Sisi nasi twendeni tukafe pamoja naye.” Yesu alipowasili huko alikuta Lazaro amekuwa kaburini siku nne. Basi Bethania ulikuwa karibu na Yerusalemu umbali wa karibu maili mbili, na Wayahudi wengi walikuwa wamekuja kuwafariji Martha na Maria kwa ajili ya kufiwa na ndugu yao. Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alitoka kwenda kumlaki, ila Maria alibaki nyumbani. Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini sasa ninajua kuwa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa.” Yesu akamwambia, “Ndugu yako atafufuka.”