Yohane 11:1-23
Yohane 11:1-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Mtu mmoja aitwaye Lazaro, mwenyeji wa Bethania, alikuwa mgonjwa. (Kijiji cha Bethania kilikuwa mahali walipokaa Maria na Martha, dada yake. Maria ndiye yule aliyempaka Bwana marashi na kumpangusa kwa nywele zake. Lazaro, kaka yake, ndiye aliyekuwa mgonjwa). Basi, hao dada wakatuma ujumbe huu kwa Yesu: “Bwana, rafiki yako ni mgonjwa!” Yesu aliposikia hivyo, akasema, “Ugonjwa huo hautaleta kifo, ila ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu; ameugua ili kwa njia hiyo Mwana wa Mungu atukuzwe.” Yesu aliwapenda Martha, dada yake na Lazaro. Alipopata habari kwamba Lazaro ni mgonjwa, Yesu aliendelea kukaa mahali hapo alipokuwa kwa siku mbili zaidi. Kisha akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni tena Yudea!” Wanafunzi wakamwambia, “Mwalimu! Muda mfupi tu umepita tangu Wayahudi walipotaka kukuua kwa mawe, nawe unataka kwenda huko tena?” Yesu akajibu, “Je, saa za mchana si kumi na mbili? Basi, mtu akitembea mchana hawezi kujikwaa kwa kuwa anauona mwanga wa ulimwengu huu. Lakini mtu akitembea usiku atajikwaa kwa maana mwanga haumo ndani yake.” Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini mimi nitakwenda kumwamsha.” Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, ikiwa amelala, basi atapona.” Wao walidhani kwamba alikuwa amesema juu ya kulala usingizi, kumbe alikuwa amesema juu ya kifo cha Lazaro. Basi, Yesu akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa; lakini nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini. Haya, twendeni kwake.” Thoma (aitwaye Pacha) akawaambia wanafunzi wenzake, “Twendeni nasi tukafe pamoja naye!” Yesu alipofika huko alikuta Lazaro amekwisha kaa kaburini kwa siku nne. Kijiji cha Bethania kilikuwa karibu na Yerusalemu, umbali upatao kilomita tatu. Wayahudi wengi walikuwa wamefika kwa Martha na Maria kuwafariji kwa kifo cha kaka yao. Basi, Martha aliposikia kwamba Yesu alikuwa anakuja, akaenda kumlaki; lakini Maria alibaki nyumbani. Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa! Lakini najua kwamba hata sasa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa.” Yesu akamwambia, “Kaka yako atafufuka.”
Yohane 11:1-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi mtu mmoja alikuwa mgonjwa, Lazaro wa Bethania, mwenyeji wa mji wa Mariamu na Martha, dada yake. Ndiye Mariamu yule aliyempaka Bwana marhamu, akamfuta miguu kwa nywele zake, ambaye Lazaro nduguye alikuwa mgonjwa. Basi wale dada wakatuma ujumbe kwake wakisema, Bwana, yeye umpendaye ni mgonjwa. Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo. Naye Yesu alimpenda Martha na dada yake na Lazaro. Basi aliposikia ya kwamba ni mgonjwa, bado alikaa siku mbili pale pale alipokuwapo. Kisha, baada ya hayo, akawaambia wanafunzi wake, Twendeni Yudea tena. Wale wanafunzi wakamwambia, Rabi, juzi juzi tu Wayahudi walikuwa wakitafuta kukupiga kwa mawe, nawe unakwenda huko tena? Yesu akajibu, Je! Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu akienda mchana hajikwai; kwa sababu aiona nuru ya ulimwengu huu. Bali akienda usiku hujikwaa; kwa sababu nuru haimo ndani yake. Aliyasema hayo; kisha, baada ya hayo, akawaambia, Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha. Basi wale wanafunzi wakamwambia, Bwana, ikiwa amelala, atapona. Lakini Yesu alikuwa amenena habari ya mauti yake; nao walidhania ya kuwa ananena habari ya kulala usingizi. Basi hapo Yesu akawaambia waziwazi, Lazaro amekufa. Nami nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini; lakini na twendeni kwake. Basi Tomaso, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe, Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye. Basi Yesu alipofika, alimkuta amekwisha kuwamo kaburini yapata siku nne. Na Bethania ilikuwa karibu na Yerusalemu, kadiri ya maili mbili hivi; na watu wengi katika Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu, ili kuwafariji kwa ajili ya ndugu yao. Basi Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; na Mariamu alikuwa akikaa nyumbani. Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yoyote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka.
Yohane 11:1-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi mtu mmoja alikuwa hawezi, Lazaro wa Bethania, mwenyeji wa mji wa Mariamu na Martha, dada yake. Ndiye Mariamu yule aliyempaka Bwana marhamu, akamfuta miguu kwa nywele zake, ambaye Lazaro nduguye alikuwa hawezi. Basi wale maumbu wakatuma ujumbe kwake wakisema, Bwana, yeye umpendaye hawezi. Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo. Naye Yesu alimpenda Martha na umbu lake na Lazaro. Basi aliposikia ya kwamba hawezi, alikaa bado siku mbili pale pale alipokuwapo. Kisha, baada ya hayo, akawaambia wanafunzi wake, Twendeni Uyahudi tena. Wale wanafunzi wakamwambia, Rabi, juzijuzi tu Wayahudi walikuwa wakitafuta kukupiga kwa mawe, nawe unakwenda huko tena? Yesu akajibu, Je! Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu akienda mchana hajikwai; kwa sababu aiona nuru ya ulimwengu huu. Bali akienda usiku hujikwaa; kwa sababu nuru haimo ndani yake. Aliyasema hayo; kisha, baada ya hayo, akawaambia, Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha. Basi wale wanafunzi wakamwambia, Bwana, ikiwa amelala, atapona. Lakini Yesu alikuwa amenena habari ya mauti yake; nao walidhania ya kuwa ananena habari ya kulala usingizi. Basi hapo Yesu akawaambia waziwazi, Lazaro amekufa. Nami nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini; lakini na twendeni kwake. Basi Tomaso, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe, Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye. Basi Yesu alipofika, alimkuta amekwisha kuwamo kaburini yapata siku nne. Na Bethania ilikuwa karibu na Yerusalemu, kadiri ya maili mbili hivi; na watu wengi katika Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu, ili kuwafariji kwa habari ya ndugu yao. Basi Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; na Mariamu alikuwa akikaa nyumbani. Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yo yote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka.
Yohane 11:1-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi mtu mmoja jina lake Lazaro alikuwa mgonjwa. Yeye alikuwa akiishi Bethania kijiji cha Maria na Martha dada zake. Huyu Maria, ambaye Lazaro kaka yake alikuwa mgonjwa, ndiye yule ambaye alimpaka Bwana mafuta na kuifuta miguu yake kwa nywele zake. Hivyo hawa dada wawili walituma ujumbe kwa Yesu kumwambia, “Bwana, yule umpendaye ni mgonjwa.” Lakini Yesu aliposikia hayo, akasema, “Ugonjwa huu hautaleta mauti bali umetokea ili kudhihirisha utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu apate kutukuzwa kutokana na ugonjwa huu.” Pamoja na hivyo, ingawa Yesu aliwapenda Martha, Maria na Lazaro ndugu yao, baada ya kusikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, aliendelea kukawia huko alikokuwa kwa siku mbili zaidi. Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Haya, turudi Uyahudi.” Wanafunzi wake wakamwambia, “Rabi, Wayahudi walikuwa wanataka kukupiga mawe, nawe unataka kurudi huko?” Yesu akawajibu, “Si kuna saa kumi na mbili za mchana katika siku moja? Wala watembeao mchana hawawezi kujikwaa kwa maana wanaona nuru ya ulimwengu huu. Lakini wale watembeao usiku hujikwaa kwa sababu hakuna nuru ndani yao.” Baada ya kusema haya, Yesu akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini naenda kumwamsha.” Wanafunzi wakamwambia, “Bwana, kama amelala usingizi ataamka.” Hata hivyo, Yesu alikuwa anazungumzia kuwa Lazaro amekufa, lakini wanafunzi wake hawakuelewa, walidhani kwamba anasema Lazaro amelala usingizi tu. Kwa hiyo Yesu akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa. Hata hivyo nafurahi kwa kuwa sikuwepo huko kabla ya Lazaro kufa, ili mpate kuamini. Lakini sasa twendeni kwake.” Tomaso aliyeitwa Pacha akawaambia wanafunzi wenzake, “Sisi nasi twendeni tukafe pamoja naye.” Yesu alipowasili huko alikuta Lazaro amekuwa kaburini siku nne. Basi Bethania ulikuwa karibu na Yerusalemu umbali wa karibu maili mbili, na Wayahudi wengi walikuwa wamekuja kuwafariji Martha na Maria kwa ajili ya kufiwa na ndugu yao. Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alitoka kwenda kumlaki, ila Maria alibaki nyumbani. Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini sasa ninajua kuwa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa.” Yesu akamwambia, “Ndugu yako atafufuka.”