Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 4

4
1“Ikiwa utataka kurudi, ee Israeli,
nirudie mimi,”
asema Mwenyezi Mungu.
“Ikiwa utaondoa sanamu zako za kuchukiza mbele ya macho yangu
na usiendelee kutangatanga,
2ikiwa utaapa katika kweli, kwa haki na kwa unyofu,
‘Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo,’
ndipo mataifa yatakapobarikiwa naye,
na ndani yake watajitukuza.”
3Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kwa watu wa Yuda na kwa Yerusalemu:
“Vunjeni mabonge kwenye mashamba yenu,
wala msipande katikati ya miiba.
4Jitahirini katika Mwenyezi Mungu,
tahirini mioyo yenu,
enyi wanaume wa Yuda
na watu wa Yerusalemu,
la sivyo ghadhabu yangu itatoka kwa nguvu
na kuwaka kama moto
kwa sababu ya uovu mliotenda,
ikiwaka pasipo wa kuizima.
Maafa kutoka kaskazini
5“Tangaza katika Yuda
na upige mbiu katika Yerusalemu, useme:
‘Piga tarumbeta katika nchi yote!’
Piga kelele na kusema:
‘Kusanyikeni pamoja!
Tukimbilie katika miji yenye ngome!’
6Inueni ishara ili kwenda Sayuni!
Kimbilieni usalama pasipo kuchelewa!
Kwa kuwa ninaleta maafa kutoka kaskazini,
maangamizi ya kutisha.”
7Simba ametoka nje ya pango lake,
mwangamizi wa mataifa amejipanga.
Ametoka mahali pake
ili aangamize nchi yenu.
Miji yenu itakuwa magofu
pasipo mtu wa kuishi humo.
8Hivyo vaeni magunia,
ombolezeni na kulia kwa huzuni,
kwa kuwa hasira kali ya Mwenyezi Mungu
haijaondolewa kwetu.
9“Katika siku ile,” asema Mwenyezi Mungu
“mfalme na maafisa watakata tamaa,
makuhani watafadhaika,
na manabii watashangazwa mno.”
10Ndipo niliposema, “Aa, Bwana Mungu Mwenyezi, hakika umewadanganya watu hawa na Yerusalemu kwa kusema, ‘Mtakuwa na amani,’ wakati upanga uko kooni!”
11Wakati huo watu hawa na Yerusalemu wataambiwa, “Upepo wa moto kutoka miinuko iliyo kame jangwani unavuma kuelekea kwa watu wangu, lakini sio upepo wa kupepeta na kutakasa; 12upepo wenye nguvu sana kuliko wa kupepeta na kutakasa utakuja kwa amri yangu. Sasa natangaza hukumu zangu dhidi yao.”
13Tazama! Anakuja kama mawingu,
magari yake ya vita yanakuja kama upepo wa kisulisuli,
farasi wake wana mbio kuliko tai.
Ole wetu! Tunaangamia!
14Ee Yerusalemu, usafishe uovu
kutoka moyoni mwako, uokolewe.
Utaendelea kuficha mawazo yako potovu hadi lini?
15Sauti inatangaza kutoka Dani,
ikipiga mbiu ya maafa kutoka vilima vya Efraimu.
16“Waambie mataifa jambo hili,
piga mbiu hii dhidi ya Yerusalemu:
‘Jeshi la kuzingira linakuja kutoka nchi ya mbali,
likipiga kelele za vita dhidi ya miji ya Yuda.
17Wamemzunguka kama watu walindao shamba,
kwa sababu amefanya uasi dhidi yangu,’ ”
asema Mwenyezi Mungu.
18“Mwenendo wako na matendo yako mwenyewe
vimeleta haya juu yako.
Hii ndiyo adhabu yako.
Tazama jinsi ilivyo chungu!
Tazama jinsi inavyochoma moyo!”
19Ee mtima wangu, mtima wangu!
Ninagaagaa kwa maumivu.
Ee maumivu makuu ya moyo wangu!
Moyo wangu umefadhaika ndani yangu,
siwezi kunyamaza,
kwa sababu nimesikia sauti ya tarumbeta;
nimesikia kelele za vita.
20Maafa baada ya maafa,
nchi yote imekuwa magofu.
Kwa ghafula mahema yangu yameangamizwa,
makazi yangu kwa muda mfupi.
21Hata lini nitaendelea kuona bendera ya vita
na kusikia sauti za tarumbeta?
22“Watu wangu ni wapumbavu,
hawanijui mimi.
Ni watoto wasio na akili,
hawana ufahamu.
Ni hodari kutenda mabaya,
hawajui kutenda yaliyo mema.”
23Niliitazama dunia,
nayo haikuwa na umbo tena ni tupu;
niliziangalia mbingu,
mianga ilikuwa imetoweka.
24Niliitazama milima, nayo ilikuwa ikitetemeka,
vilima vyote vilikuwa vikiyumbayumba.
25Nilitazama, wala hapakuwa na watu;
kila ndege wa angani alikuwa ameruka zake.
26Nilitazama, nayo nchi iliyokuwa imestawi vizuri
imekuwa jangwa,
miji yake yote ilikuwa magofu
mbele za Mwenyezi Mungu,
mbele ya hasira yake kali.
27Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu:
“Nchi yote itaharibiwa,
ingawa sitaiangamiza kabisa.
28Kwa hiyo dunia itaomboleza
na mbingu zilizo juu zitakuwa giza,
kwa sababu nimesema nami sitarudi nyuma,
nimeamua na wala sitageuka.”
29Kwa sauti ya wapanda farasi na wapiga upinde
kila mji unakimbia.
Baadhi wanakimbilia vichakani,
baadhi wanapanda juu ya miamba.
Miji yote imeachwa,
hakuna aishiye ndani yake.
30Unafanya nini, ewe uliyeharibiwa?
Kwa nini unajivika vazi jekundu
na kuvaa vito vya dhahabu?
Kwa nini unapaka macho yako wanja?
Unajipamba bure.
Wapenzi wako wanakudharau,
wanautafuta uhai wako.
31Nasikia kilio kama cha mwanamke
katika uchungu wa kuzaa,
kilio cha uchungu kama cha anayemzaa
mtoto wake wa kwanza:
kilio cha Binti Sayuni akitweta ili aweze kupumua,
akiinua mikono yake, akisema,
“Ole wangu! Ninazimia;
maisha yangu yamekabidhiwa kwa wauaji.”

Iliyochaguliwa sasa

Yeremia 4: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia