Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 37

37
Yeremia gerezani
1Sedekia mwana wa Yosia akafanywa kuwa mfalme wa Yuda na Nebukadneza mfalme wa Babeli, naye akatawala mahali pa Yehoyakini#37:1 au Yekonia, Konia mwana wa Yehoyakimu. 2Lakini sio Sedekia, wala watumishi wake, wala watu wa nchi walisikiliza maneno ya Mwenyezi Mungu aliyonena kupitia kwa nabii Yeremia.
3Hata hivyo, Mfalme Sedekia akamtuma Yehukali mwana wa Shelemia, pamoja na kuhani Sefania mwana wa Maaseya kwa nabii Yeremia na ujumbe huu: “Tafadhali utuombee kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.”
4Wakati huu Yeremia alikuwa huru kuingia na kutoka katikati ya watu, kwa sababu alikuwa bado hajatiwa gerezani. 5Jeshi la Farao lilikuwa limetoka Misri, nao Wakaldayo waliokuwa wameuzingira Yerusalemu kwa majeshi waliposikia taarifa kuhusu jeshi hilo walijiondoa Yerusalemu.
6Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia nabii Yeremia kusema: 7“Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Mwambie mfalme wa Yuda aliyekutuma uniulize mimi, ‘Jeshi la Farao lililokuja kukusaidia litarudi katika nchi yake yenyewe, yaani Misri. 8Kisha Wakaldayo watarudi na kushambulia mji huu, watauteka na kuuchoma moto.’
9“Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Msijidanganye wenyewe mkifikiri, ‘Hakika Wakaldayo watatuacha na kwenda zao.’ Hakika hawatawaacha! 10Hata kama mngelishinda jeshi lote la Wakaldayo linalowashambulia ninyi, na wakawa ni watu waliojeruhiwa tu waliobaki kwenye mahema yao, wangetoka na kuuchoma mji huu moto.”
11Baada ya jeshi la Wakaldayo kujiondoa kutoka Yerusalemu kwa sababu ya jeshi la Farao, 12Yeremia akaondoka mjini kwenda nchi ya Benyamini ili akapate huko sememu yake ya milki miongoni mwa watu. 13Lakini alipofika kwenye Lango la Benyamini, mkuu wa walinzi aliyeitwa Iriya mwana wa Shelemia, mwana wa Hanania, akamkamata Yeremia na kusema, “Wewe unaenda kujiunga na Wakaldayo!”
14Yeremia akasema, “Hiyo si kweli, mimi sijiungi na Wakaldayo.” Lakini Iriya hakumsikiliza; badala yake, akamkamata Yeremia na kumpeleka kwa maafisa. 15Wakamkasirikia Yeremia, wakaamuru apigwe, na akafungwa katika nyumba ya Yonathani mwandishi waliyokuwa wameifanya kuwa gereza.
16Yeremia akawekwa kwenye chumba kilichofukuliwa chini, kilichojengwa kwa zege ndani ya gereza chini ya ngome, akakaa huko kwa muda mrefu. 17Kisha Mfalme Sedekia akatumana aletwe katika jumba la kifalme, mahali alipomuuliza kwa siri, “Je, kuna neno lolote kutoka kwa Mwenyezi Mungu?”
Yeremia akajibu, “Ndiyo, utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli.”
18Kisha Yeremia akamwambia Mfalme Sedekia, “Nimefanya kosa gani dhidi yako na maafisa wako au watu hawa, hata ukanifunga gerezani? 19Wako wapi manabii wako waliokutabiria wakisema, ‘Mfalme wa Babeli hatakushambulia wewe wala nchi hii’? 20Lakini sasa, bwana wangu mfalme, tafadhali sikiliza. Niruhusu nilete maombi yangu mbele yako, usinirudishe kwenye nyumba ya Yonathani mwandishi, nisije nikafia humo.”
21Ndipo Mfalme Sedekia akatoa maagizo Yeremia awekwe katika ua wa walinzi, na apewe mkate kutoka mitaa ya waokaji kila siku hadi mikate yote katika mji itakapokwisha. Kwa hiyo Yeremia akabaki katika ua wa walinzi.

Iliyochaguliwa sasa

Yeremia 37: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia