Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 22

22
Hukumu dhidi ya wafalme waovu
1Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Shuka kwenye jumba la kifalme la mfalme wa Yuda, utangaze ujumbe huu huko: 2‘Sikia neno la Mwenyezi Mungu, ee mfalme wa Yuda, wewe uketiye kwenye kiti cha utawala cha Daudi: wewe, wakuu wako na watu wako mnaopitia malango haya. 3Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Tenda haki na adili. Mwokoe mkononi mwa mdhalimu yeye aliyetekwa nyara. Usimtendee mabaya wala ukatili mgeni, yatima au mjane, wala usimwage damu isiyo na hatia mahali hapa. 4Ukiwa mwangalifu kushika maagizo haya, wafalme watakaokalia kiti cha utawala cha Daudi wataingia kupitia malango ya jumba la kifalme wakiwa wamepanda magari na farasi huku wakifuatana na watumishi wao na watu wao. 5Lakini kama hutayatii maagizo haya, asema Mwenyezi Mungu, ninaapa kwa nafsi yangu kwamba jumba hili litakuwa gofu.’ ”
6Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu jumba la kifalme la mfalme wa Yuda:
“Ingawa uko kama Gileadi kwangu,
kama kilele cha Lebanoni,
hakika nitakufanya uwe kama jangwa,
kama miji ambayo haijakaliwa na watu.
7Nitawatuma waharibifu dhidi yako,
kila mtu akiwa na silaha zake,
nao watazikata boriti zako bora za mwerezi
na kuzitupa motoni.
8“Watu kutoka mataifa mengi watapita karibu na mji huu na kuulizana, ‘Kwa nini Mwenyezi Mungu amefanya jambo la namna hii kwa mji huu mkubwa?’ 9Nalo jibu litakuwa: ‘Kwa sababu wameliacha agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wao, na wameabudu na kuitumikia miungu mingine.’ ”
10Usimlilie yeye aliyekufa, wala usimwombolezee;
badala yake, afadhali umlilie kwa uchungu
yule aliyepelekwa uhamishoni,
kwa sababu kamwe hatairudia
wala kuiona tena nchi yake aliyozaliwa.
11Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu Shalumu#22:11 pia anaitwa Yehoahazi mwana wa Yosia, aliyeingia mahali pa baba yake kuwa mfalme wa Yuda, lakini ameondoka mahali hapa: “Yeye kamwe hatarudi tena. 12Atafia huko mahali walipompeleka kuwa mateka; hataiona tena nchi hii.”
13“Ole wake yeye ajengaye jumba lake la kifalme kwa dhuluma,
vyumba vyake vya juu kwa udhalimu,
akiwatumikisha watu wa nchi yake pasipo malipo,
bila kuwalipa kwa utumishi wao.
14Anasema, ‘Nitajijengea jumba kuu la kifalme,
na vyumba vya juu vyenye nafasi kubwa.’
Hivyo anaweka ndani yake madirisha makubwa,
huweka kuta za mbao za mwerezi,
na kuzipaka kwa rangi nyekundu.
15“Je, huko kuongeza idadi ya mierezi
kutakufanya uwe mfalme?
Je, baba yako hakula na kunywa?
Alifanya yaliyo sawa na haki,
naye akafanikiwa kwa yote.
16Aliwatetea maskini na wahitaji,
hivyo yeye akafanikiwa katika yote.
Je, hiyo si ndiyo maana ya kunijua mimi?”
asema Mwenyezi Mungu.
17“Lakini macho yako na moyo wako vimeelekezwa tu
katika mapato ya udhalimu,
kumwaga damu isiyo na hatia,
na katika uonevu na ukatili.”
18Kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda:
“Hawatamwombolezea wakisema:
‘Ole, ndugu yangu! Ole, dada yangu!’
Hawatamwombolezea wakisema:
‘Ole, bwana wangu! Ole, fahari yake!’
19Atazikwa maziko ya punda:
ataburutwa na kutupwa
nje ya malango ya Yerusalemu.”
20“Panda Lebanoni ukapige kelele,
sauti yako na isikike huko Bashani,
piga kelele toka Abarimu,
kwa kuwa wote waliojiunga nawe wameangamizwa.
21Nilikuonya wakati ulipojisikia kwamba uko salama,
lakini ulisema, ‘Mimi sitasikiliza!’
Hii imekuwa kawaida yako tangu ujana wako;
hujanitii mimi.
22Upepo utawaondoa wachungaji wako wote,
na wandani wako wataenda uhamishoni.
Kisha utaaibika na kufedheheka
kwa sababu ya uovu wako wote.
23Wewe uishiye Lebanoni,
wewe uliyetulia kwenye majengo ya mwerezi,
tazama jinsi utakavyoomboleza
maumivu makali yatakapokupata,
maumivu kama ya mwanamke
mwenye uchungu wa kuzaa!
24“Hakika kama niishivyo,” asema Mwenyezi Mungu, “hata kama wewe, Yekonia#22:24 au Konia; pia anaitwa Yehoyakini mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, ungekuwa pete yangu ya muhuri katika mkono wangu wa kuume, bado ningekung’oa hapo. 25Nitakutia mikononi mwa wanaoutafuta uhai wako, wale unaowaogopa, yaani Nebukadneza mfalme wa Babeli na kwa Wakaldayo. 26Nitakutupa mbali wewe na mama aliyekuzaa mwende katika nchi nyingine, ambayo hakuna hata mmoja wenu aliyezaliwa huko, nanyi mtafia huko. 27Kamwe hamtarudi katika nchi mliyotamani kuirudia.”
28Je, huyu mtu Yekonia ni chungu kilichodharauliwa,
chungu kilichovunjika,
chombo kisichotakiwa na mtu yeyote?
Kwa nini yeye na watoto wake watupwe nje kwa nguvu,
na kutupwa kwenye nchi wasioijua?
29Ee nchi, nchi, nchi,
sikia neno la Mwenyezi Mungu!
30Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Mwandike huyu mtu kama asiye na mtoto,
mtu ambaye hatafanikiwa maisha yake yote,
kwa maana hakuna mzao wake atakayefanikiwa,
wala kukaa kwenye kiti cha utawala cha Daudi
wala kuendelea kutawala katika Yuda.”

Iliyochaguliwa sasa

Yeremia 22: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia