Yeremia 21
21
Mwenyezi Mungu anakataa ombi la Sedekia
1Neno lilimjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu wakati Mfalme Sedekia alipowatuma Pashuri mwana wa Malkiya, na kuhani Sefania mwana wa Maaseya kwake, kusema: 2“Tuulizie sasa kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu Nebukadneza mfalme wa Babeli anatushambulia. Labda Mwenyezi Mungu atatenda maajabu kwa ajili yetu kama nyakati zilizopita, ili Nebukadneza atuondokee.”
3Lakini Yeremia akawajibu, “Mwambieni Sedekia, 4‘Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemalo: Ninakaribia kuwageuzia silaha za vita zilizo mikononi mwenu, ambazo mnatumia kupigana na mfalme wa Babeli na Wakaldayo walio nje ya ukuta wakiwazingira kwa jeshi. Nami nitawakusanya ndani ya mji huu. 5Mimi mwenyewe nitapigana dhidi yenu kwa mkono wangu ulionyooshwa na mkono wa nguvu, kwa hasira na ghadhabu kali na ukali mwingi. 6Nitawaangamiza wakaaji wa mji huu, watu na wanyama, nao watauawa kwa tauni ya kutisha. 7Baada ya hayo, nitamtia Sedekia mfalme wa Yuda, maafisa wake na watu wa mji huu ambao walinusurika tauni, upanga na njaa, mkononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, na kwa adui zao wale wanaotafuta uhai wao. Atawaua kwa upanga; hatakuwa na rehema juu yao au huruma wala kuwasikitikia,’ asema Mwenyezi Mungu.
8“Zaidi ya hayo, waambie watu hawa, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Tazama, naweka mbele yenu njia ya uzima, na njia ya mauti. 9Yeyote atakayekaa katika mji huu atakufa kwa upanga, njaa au tauni. Lakini yeyote atakayeenda na kujisalimisha kwa Wakaldayo, ambao wameuzingira mji huu kwa jeshi, atanusurika, naye ataishi. 10Nimekusudia kuufanyia mji huu jambo baya, wala si jema. Utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteketeza kwa moto, asema Mwenyezi Mungu.’
11“Zaidi ya hayo, iambie nyumba ya mfalme ya Yuda, ‘Sikia neno la Mwenyezi Mungu, 12Ewe nyumba ya Daudi, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“ ‘Hukumuni kwa haki kila asubuhi,
mwokoeni mikononi mwa mdhalimu
yeye aliyetekwa nyara,
la sivyo ghadhabu yangu italipuka
na kuwaka kama moto
kwa sababu ya uovu mlioufanya:
itawaka na hakuna wa kuizima.
13Niko kinyume nawe, ee Yerusalemu,
wewe uishiye juu ya bonde hili
kwenye uwanda wa juu wa miamba,
asema Mwenyezi Mungu,
wewe usemaye, “Ni nani awezaye kuja kinyume chetu?
Nani ataingia mahali pa kimbilio letu?”
14Nitawaadhibu kama istahilivyo matendo yenu,
asema Mwenyezi Mungu.
Nitawasha moto katika misitu yenu
ambao utateketeza kila kitu kinachowazunguka.’ ”
Iliyochaguliwa sasa
Yeremia 21: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.