Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waamuzi 9:22-57

Waamuzi 9:22-57 NEN

Baada ya Abimeleki kutawala Israeli kwa muda wa miaka mitatu, Mungu akaruhusu roho mbaya kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu, nao watu wa Shekemu wakamtendea Abimeleki kwa hila. Hili lilitokea ili ule ukatili waliotendewa hao wana sabini wa Yerub-Baali upatilizwe, na damu yao iwe juu ya Abimeleki ndugu yao aliyewaua, na pia iwe juu ya watu wa Shekemu, ambao walimsaidia kuua ndugu zake. Hivyo, kutokana na uadui juu yake watu wa Shekemu wakaweka watu wa kumvizia katika vilele vya milima. Wakawanyangʼanya watu wote waliopita karibu nao, nayo haya yakaarifiwa kwa Abimeleki. Basi Gaali mwana wa Ebedi akaenda pamoja na ndugu zake wakaingia Shekemu, nao watu wa huko wakamtumainia yeye. Wakaenda mashambani mwao kuvuna zabibu na kuzisindika hizo zabibu, wakafanya sikukuu katika hekalu la mungu wao. Wakati wakila na kunywa, wakamlaani Abimeleki. Gaali mwana wa Ebedi akasema, “Abimeleki ni nani, na Shekemu ni nani, hata tumtumikie? Je, yeye si mwana wa Yerub-Baali? Naye Zebuli si ndiye msaidizi wake? Basi watumikieni watu wa Hamori, babaye Shekemu. Kwa nini tumtumikie Abimeleki? Laiti watu hawa wangekuwa chini ya amri yangu! Basi mimi ningemwondoa huyo Abimeleki. Ningemwambia Abimeleki, ‘Ondoa jeshi lako lote.’ ” Zebuli aliyekuwa mtawala wa mji aliposikia aliyosema Gaali mwana wa Ebedi, akakasirika sana. Akatuma ujumbe uende kwa Abimeleki kwa siri na kusema, “Gaali mwana wa Ebedi na ndugu zake wamekuja Shekemu, na wanauchochea mji huu kinyume chako. Sasa, basi, usiku huu wewe uondoke na watu wako ili mje kuwavizia mashambani. Kisha asubuhi wakati wa kuchomoza jua, amka mapema na ujipange dhidi ya huo mji. Wakati yeye na jeshi lililo pamoja naye watakapotoka kukabiliana nanyi, mwaweza kuwatendea kwa kadiri mnavyoweza.” Kwa hiyo Abimeleki pamoja na jeshi lake lote wakaondoka usiku na kujificha karibu na Shekemu wakiwa vikosi vinne. Basi Gaali mwana wa Ebedi alikuwa ametoka nje akawa amesimama katika ingilio la mji wakati ule ule ambao Abimeleki na watu wake walipokuwa wanatoka sehemu zao za maficho. Gaali alipowaona, akamwambia Zebuli, “Tazama, watu wanashuka kutoka kwenye vilele vya milima!” Zebuli akajibu, “Wewe unaona vivuli vya milima kana kwamba ni watu.” Lakini Gaali akasema tena, “Tazama, watu wanashuka kutoka katikati ya nchi na kikosi kimoja kinakuja kutoka Tabur-Ezeri na kikosi kingine kutoka upande wa Elon-Meonenimu.” Ndipo Zebuli akamwambia, “Kuko wapi kujivuna kwako sasa, wewe uliyesema, ‘Huyo Abimeleki ni nani hata tumtumikie?’ Hawa si wale watu uliowadharau? Toka nje sasa ukapigane nao!” Basi Gaali akatoka akawaongoza watu wa Shekemu kupigana na Abimeleki. Abimeleki akamfukuza, watu wengi wakajeruhiwa katika kukimbia huko, njia nzima hadi kwenye ingilio la lango. Abimeleki akakaa Aruma, naye Zebuli akawafukuza Gaali na ndugu zake watoke Shekemu. Kesho yake watu wa Shekemu wakatoka wakaenda mashambani, Abimeleki akaambiwa juu ya jambo hili. Hivyo akawachukua watu wake, akawagawanya katika vikosi vitatu na kuwaweka waviziao huko mashambani. Alipowaona watu wanatoka kwenda nje ya mji, akainuka dhidi yao na kuwashambulia. Abimeleki pamoja na vile vikosi wakaharakisha kwenda mbele kwenye nafasi, mahali pa ingilio la lango la mji. Vile vikosi viwili vikawawahi wale waliokuwa mashambani na kuwaua. Siku hiyo nzima Abimeleki akazidisha mashambulizi yake dhidi ya mji hadi akawa ameuteka na kuwaua watu wa huo mji. Kisha akauangamiza mji na kusambaza chumvi juu yake. Kwa kusikia jambo hili watu wote katika mnara wa Shekemu, wakaingia kwenye ngome ya hekalu la El-Berithi. Abimeleki aliposikia kuwa wamekusanyika huko, yeye na watu wake wote wakakwea kwenye Mlima Salmoni. Abimeleki akachukua shoka, akakata baadhi ya matawi, ambayo aliyachukua mabegani. Akawaagiza wale watu waliokuwa pamoja naye kuwa, “Fanyeni kile mlichoona mimi nikifanya!” Basi watu wote wakakata matawi na kumfuata Abimeleki. Wakayakusanya hayo matawi juu ya ngome na kuitia moto ili kuwachoma wale watu wote waliokuwa ndani yake. Hivyo watu wote katika mnara wa Shekemu, karibia watu 1,000 waume kwa wake, pia wakafa. Baadaye Abimeleki akaenda Thebesi na kuuzingira kwa jeshi na kuuteka. Hata hivyo, ndani ya huo mji kulikuwa na mnara imara, ambako watu wote wa mji wanaume na wanawake, watu wote wa mji, walikimbilia ndani yake. Wakajifungia ndani yake na kupanda juu ya paa la mnara. Abimeleki akaja kwenye ule mnara na kuushambulia, lakini alipokaribia kwenye ingilio la mnara ili kuuchoma kwa moto, mwanamke mmoja akaangusha sehemu ya juu ya jiwe la kusagia juu ya kichwa cha Abimeleki, likapasua fuvu la kichwa chake. Akamwita kwa haraka kijana yule aliyechukua silaha zake, na kumwambia, “Chukua upanga wako na uniue, watu wasije wakasema kwamba, ‘Mwanamke amemuua.’ ” Basi yule kijana akamchoma upanga, naye akafa. Waisraeli walipoona kuwa Abimeleki amekufa, kila mtu akaenda nyumbani kwake. Hivyo ndivyo Mungu alivyolipiza uovu ule ambao Abimeleki alikuwa ameutenda kwa baba yake kwa kuwaua ndugu zake sabini. Mungu akawapatiliza watu wa Shekemu uovu wao juu ya vichwa vyao, na juu yao ikaja laana ya Yothamu mwana wa Yerub-Baali.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha