Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waamuzi 9:22-57

Waamuzi 9:22-57 Biblia Habari Njema (BHN)

Abimeleki alitawala juu ya Israeli kwa muda wa miaka mitatu. Kisha Mungu akaleta roho ya uadui kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu, nao wakamwasi. Ndivyo walivyoadhibiwa watu wa Shekemu pamoja na ndugu yao Abimeleki kwa ukatili waliowafanyia wana sabini wa Yerubaali. Adhabu ya mauaji hayo iliwapata maana Abimeleki aliwaua akisaidiwa na hao watu wa Shekemu. Watu wa Shekemu waliweka washambulizi wamwotee Abimeleki kutoka vilele vya mlima. Watu hao waliwanyanganya mali zao wote waliopita huko. Abimeleki akaambiwa mambo hayo. Siku moja Gaali, mwana wa Ebedi, pamoja na ndugu zake alikwenda kukaa Shekemu. Watu wa Shekemu wakawa na imani naye. Wakatoka na kwenda kwenye mashamba yao ya mizabibu, wakachuma zabibu halafu wakazisindika, wakatengeneza divai wakafanya sikukuu. Wakaingia kwenye nyumba ya mungu wao wakala na kunywa; kisha wakamtukana Abimeleki. Gaali, mwana wa Ebedi, akasema, “Abimeleki ni nani? Sisi hapa Shekemu ni watu wa aina gani hata tumtumikie Abimeleki? Gideoni na Zebuli ofisa wake walimtumikia Hamori baba wa Shekemu, lakini kwa nini basi, sisi tumtumikie Abimeleki? Kama watu hawa wangekuwa chini yangu, ningemwondoa Abimeleki. Ningemwambia Abimeleki, ‘Ongeza jeshi lako, kisha, njoo hadharani tupigane.’” Zebuluni, mtawala wa mji, aliposikia maneno ya Gaali mwana wa Ebedi, alikasirika sana. Basi akampelekea ujumbe Abimeleki huko Torma akasema, “Gaali, mwana wa Ebedi, pamoja na ndugu zake wameingia mjini Shekemu na kuchochea uasi dhidi yako. Basi, rudi wewe na watu ulio nao, wakati wa usiku, uvizie mashambani karibu na mji. Mara jua litakapotoka wakati wa asubuhi, ushambulie mji. Gaali akitoka pamoja na watu wake kuja kukukabili, uwatendee ifaavyo.” Abimeleki aliondoka na watu waliokuwa pamoja naye kuja Shekemu wakati wa usiku. Aliwagawa watu wake katika vikosi vinne na kuvizia huko karibu na mji. Gaali, mwana wa Ebedi, akatoka nje na kusimama kwenye lango la mji, wakati huo Abimeleki na watu wake walitoka mahali walipokuwa wanavizia. Gaali alipomwona akamwambia Zebuli, “Tazama, watu wanashuka kutoka vilele vya mlima.” Zebuli akamwambia, “Wewe unaona vivuli vya milima kana kwamba ni watu.” Gaali akasema tena, “Tazama! Watu wanashuka katikati ya nchi na kikosi kingine kinatoka upande wa Mwaloni wa Waaguzi.” Kisha Zebuli akamwambia, “Majivuno yako yako wapi sasa? Si ni wewe uliyesema, ‘Abimeleki ni nani? Kwa nini tumtumikie?’ Sasa, hao ndio watu uliowadharau; nenda ukapigane nao.” Gaali akatoka akiwaongoza watu wa Shekemu na kupigana na Abimeleki. Gaali akashindwa na kukimbia, huku anafuatiwa na Abimeleki. Watu wengi walijeruhiwa na kuanguka njiani hadi kwenye lango la mji. Abimeleki akakaa Aruma na Zebuli akamfukuza Gaali na ndugu zake kutoka mji wa Shekemu. Siku iliyofuata, Abimeleki alipata habari kwamba watu wa Shekemu wametoka mjini na kwenda mashambani. Akachukua watu wake akawagawa katika vikosi vinne, ili waende kuvizia mashambani. Alipowaona watu wanatoka mjini, akatoka alikojificha akawaua. Abimeleki na kundi lake wakaenda mbio kwenda kulinda lango la mji. Makundi yake mawili mengine yaliwashambulia wale waliokuwa mashambani na kuwaua. Abimeleki alipigana na wakazi wa mji huo siku nzima. Akauteka mji na kuwaua watu wote waliokuwamo humo. Akauteketeza mji kwa moto na kuutia chumvi. Watu wote waliokuwa katika mnara wa Shekemu waliposikia habari hizo, walikimbilia kwenye ngome ya nyumba ya mungu aliyeitwa El-berithi. Abimeleki akaambiwa kuwa watu wote waliokuwa kwenye mnara wa Shekemu wamejikusanya pamoja. Abimeleki na watu wake wakaenda mlimani Salmoni, akachukua shoka akakata tawi la mti na kuliweka begani mwake. Halafu akawaambia wale watu aliokuwa nao waharakishe kufanya kama alivyofanya. Kila mmoja akakata tawi kama lile la Abimeleki. Wakachukua matawi yao na kuyaegemeza kwenye kuta za ngome, wakayatia moto na kuichoma ngome; watu wote wanaume na wanawake wapatao 1,000 waliokuwa katika mnara wa Shekemu wakafa. Kisha Abimeleki akaenda Thebesi, akauzingira na kuuteka. Lakini kulikuwa na mnara imara katikati ya mji. Basi, wakazi wote wa mji huo wanaume na wanawake wakakimbilia humo na kujifungia ndani. Wakapanda kwenye paa la mnara huo. Abimeleki aliufikia mnara na kuushambulia, kisha, aliukaribia mlango wa mnara autie moto. Naye mwanamke mmoja akatupa jiwe la juu la kusagia, akamponda Abimeleki kichwa. Kisha Abimeleki akamwita haraka kijana wake aliyembebea silaha akamwambia, “Chukua upanga wako uniue, wasije watu wakasema kuwa niliuawa na mwanamke.” Kijana akachukua upanga wake, akamchoma na kumuua. Waisraeli walipoona kwamba Abimeleki amekufa, wakaondoka na kurudi kila mmoja nyumbani kwake. Hivyo ndivyo Mungu alivyomwadhibu Abimeleki kwa kosa lake dhidi ya baba yake kwa kuwaua ndugu zake sabini. Vilevile Mungu aliwafanya watu wa Shekemu waadhibiwe kwa uovu wao walioufanya. Hivyo, laana ya Yothamu mwana wa Yerubaali ikawapata.

Shirikisha
Soma Waamuzi 9

Waamuzi 9:22-57 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Abimeleki alitawala juu ya Israeli kwa muda wa miaka mitatu. Kisha Mungu akatuma roho mbaya kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu; nao watu wa Shekemu wakamtendea Abimeleki kwa udanganyifu; ili kwamba huo udhalimu waliotendewa hao wana sabini wa Yerubaali ulipizwe, ili damu yao iwe juu ya Abimeleki ndugu yao, aliyewaua, na juu ya watu wa Shekemu, waliomtia nguvu mikono yake ili awaue hao nduguze. Basi watu wa Shekemu wakaweka watu kumvizia juu ya vilele vya milima, ambao waliwapora watu wote waliopita njia hiyo karibu nao; naye Abimeleki aliarifiwa. Kisha Gaali, mwana wa Ebedi, akaenda pamoja na nduguze, wakavuka na kufika Shekemu; na watu wa Shekemu wakawa na imani naye. Nao wakatoka kwenda mashambani, wakavuna mashamba yao ya mizabibu, na kuzishindika hizo zabibu, na kufanya sikukuu, kisha wakaingia nyumbani mwa mungu wao, wakala na kunywa na kumlaani huyo Abimeleki. Naye Gaali mwana wa Ebedi akasema, Abimeleki ni nani, na sisi wa Shekemu ni nani, hata tukamtumikie yeye? Je, huyu mwana wa Yerubaali na Zebuli afisa wake hawakuwatumikia watu wa Hamori babaye Shekemu? Basi, kwa nini tumutumikie? Laiti watu hawa wangekuwa chini ya mkono wangu! Hapo basi mimi ningemuondoa huyo Abimeleki. Kisha akamwambia Abimeleki, Haya, ongeza jeshi lako, utokeze. Basi hapo Zebuli, aliyekuwa mkuu wa mji, alipoyasikia hayo maneno ya Gaali mwana wa Ebedi, hasira zake zikamwaka. Naye akatuma wajumbe waende kwa Abimeleki kwa siri, akasema, Tazama, Gaali, mwana wa Ebedi, na ndugu zake wamekuja Shekemu; na wanaufitinisha mji huu kinyume chako. Basi sasa, inuka wewe, usiku, wewe na watu walio pamoja nawe, mvizie mashambani; kisha asubuhi na mapema, mara tu baada ya jua kuchomoza, inuka na uushambulie mji huo; na Gaali na wale watu walio pamoja naye watakapotokeza nje kupigana nawe, ndipo utakapowatenda kama utakavyoweza. Basi Abimeleki na watu wote waliokuwa pamoja naye wakaondoka usiku na kuuvizia Shekemu kwa vikosi vinne. Huyo Gaali mwana wa Ebedi akatoka nje, akasimama penye maingilio ya lango la mji; naye Abimeleki na hao watu waliokuwa pamoja naye wakainuka kutoka mahali pale walipokuwa wanavizia. Basi Gaali alipowaona hao watu, akamwambia Zebuli, Tazama, watu washuka kutoka katika vilele vya milima. Zebuli akamwambia, Ni kivuli cha milima unachokiona kama ndio watu. Kisha Gaali akasema mara ya pili, akanena, Angalia, watu washuka katikati ya nchi, na kikosi kimoja kinakuja kwa njia ya mwaloni wa Meonenimu. Ndipo Zebuli akamwambia, Je! Kinywa chako sasa kiko wapi, hata ukasema, Huyo Abimeleki ni nani, hata inatupasa kumtumikia yeye? Je! Hawa sio majeshi hao uliowadharau wewe? Haya, toka nje sasa, tafadhali, upigane nao. Basi Gaali akatokeza mbele ya watu wa Shekemu, akapigana na Abimeleki. Lakini Abimeleki akamkimbiza, naye akakimbia mbele yake, wengi walijeruhiwa na kuanguka hadi kufikia maingilio ya lango la mji. Abimeleki akakaa Aruma; naye Zebuli akawatoa Gaali na ndugu zake, wasikae katika Shekemu. Ikawa siku ya pili yake, watu wakatoka waende mashambani; naye Abimeleki alipoambiwa. Akawatwaa watu wake, na kuwagawanya katika vikosi vitatu, nao wakavizia mashambani; naye akaangalia, alipoona watu wakitoka nje ya mji, aliwashambulia na kuwaua. Abimeleki, na vile vikosi vilivyokuwa pamoja naye, wakafululiza, wakasimama penye maingilio ya lango la mji, na vile vikosi viwili vikawarukia hao wote waliokuwa mashambani, na kuwaua. Abimeleki akapigana na huo mji mchana kutwa; akautwaa mji, akawaua watu waliokuwamo ndani yake; kisha akauteketeza mji, na kuutia chumvi. Kisha watu wote waliokaa katika ule mnara wa Shekemu waliposikia habari hiyo wakaingia ndani ya ngome ya nyumba ya El-berithi. Abimeleki aliambiwa ya kuwa watu hao wote wa mnara wa Shekemu wamekusanyika pamoja. Basi Abimeleki akakwea kwenda katika kilima cha Salmoni, yeye na wote waliokuwa pamoja naye; naye Abimeleki akashika shoka mkononi mwake, akakata tawi moja katika miti, akalishika na kujitwika begani mwake; akawaambia hao watu waliokuwa pamoja naye, “Haya, kile mlichoona nikifanya, nanyi fanyeni vivyo hivyo haraka”. Basi watu hao wote wakakata kila mtu tawi lake, wakamfuata Abimeleki, wakayaweka hayo matawi pale ngomeni, na kuiteketeza moto hiyo ngome juu yao; ndipo watu wote wa huo mnara wa Shekemu wakafa, watu wapatao elfu moja, wanaume kwa wanawake. Ndipo Abimeleki alipokwenda Thebesi, akauzingira na kuutwaa. Lakini ndani ya huo mji palikuwa na mnara wenye nguvu, na watu wote wanaume na wanawake wakakimbilia huko, na watu wote wa mji, nao wakajifungia ndani, wakapanda paa la mnara. Abimeleki akauendea huo mnara na kupigana nao; naye akaukaribia mlango wa mnara ili auteketeze. Na mwanamke mmoja akabwaga jiwe la kusagia la juu, nalo likampiga Abimeleki kichwani, na kulivunja fuvu la kichwa chake. Ndipo akamwita kwa haraka huyo kijana aliyekuwa anamchukulia silaha zake, na kumwambia, Futa upanga wako, uniue, ili watu wasiseme juu yangu, Aliuawa na mwanamke. Basi huyo kijana wake akamchoma upanga, naye akafa. Basi hapo watu wa Israeli walipoona ya kuwa Abimeleki amekufa, wakaondoka wakaenda kila mtu mahali pake. Kwa hiyo, Mungu akalipiza kisasi juu ya uovu wa Abimeleki aliomtenda baba yake, kwa kuwaua hao nduguze watu sabini; uovu wote wa watu wa Shekemu Mungu alilipiza juu ya vichwa vyao; na hiyo laana ya Yothamu mwana wa Yerubaali ikawajia juu yao.

Shirikisha
Soma Waamuzi 9

Waamuzi 9:22-57 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Abimeleki alitawala juu ya Israeli muda wa miaka mitatu. Kisha Mungu akapeleka roho mbaya kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu; nao watu wa Shekemu wakamtendea Abimeleki kwa udanganyifu; ili kwamba huo udhalimu waliotendewa hao wana sabini wa Yerubaali uje, tena kwamba damu yao iandikwe juu ya Abimeleki ndugu yao, aliyewaua, na juu ya watu wa Shekemu, waliomtia nguvu mikono yake ili awaue hao nduguze. Basi watu wa Shekemu wakaweka watu kumvizia juu ya vilele vya milima, ambao waliwanyang’anya vitu vyao watu wote waliopita njia hiyo karibu nao; naye Abimeleki aliambiwa. Kisha Gaali, mwana wa Ebedi, akaenda pamoja na nduguze, wakavuka na kufika Shekemu; na watu wa Shekemu wakamtumaini yeye. Nao wakatoka kwenda mashambani, wakavuna mashamba yao ya mizabibu, na kuzishindika hizo zabibu, na kufanya sikukuu, kisha wakaingia nyumbani mwa mungu wao, wakala na kunywa na kumlaani huyo Abimeleki. Naye Gaali mwana wa Ebedi akasema, Abimeleki ni nani, na Shekemu ni nani, hata tukamtumikie yeye? Yeye, je! Si mwana wa Yerubaali? Na Zebuli siye akida wake? Haya, ninyi watumikieni hao watu wa Hamori, babaye Shekemu; Lakini sisi je! Tumtumikie kwa sababu gani? Laiti watu hawa wangekuwa chini ya mkono wangu! Hapo basi mimi ningemwondoa huyo Abimeleki. Kisha akamwambia Abimeleki, Haya, ongeza askari zako, utoke nje. Basi hapo Zebuli, aliyekuwa liwali wa mji, alipoyasikia hayo maneno ya Gaali mwana wa Ebedi, hasira zake zikamwaka. Naye akatuma wajumbe waende kwa Abimeleki kwa siri, akasema, Tazama, Gaali, mwana wa Ebedi, na ndugu zake wamekuja Shekemu; na tazama waufitinisha mji huu kinyume chako. Basi sasa, inuka wewe, usiku, wewe na watu walio pamoja nawe, mvizie mashambani; kisha itakuwa, asubuhi, mara litakapokucha jua, wewe utaamka asubuhi na mapema, na kuushambulia mji huo; tena, angalia, hapo yeye na wale watu walio pamoja naye watakapokutokea nje kupigana nawe, ndipo utapata kuwatenda kama utakavyopata nafasi. Basi Abimeleki akainuka na watu wote waliokuwa pamoja naye, usiku nao wakauvizia Shekemu kwa vikosi vinne. Huyo Gaali mwana wa Ebedi akatoka nje, akasimama penye maingilio ya lango la mji; naye Abimeleki na hao watu waliokuwa pamoja naye wakainuka kutoka mahali pale walipokuwa wanavizia. Basi Gaali alipowaona hao watu, akamwambia Zebuli, Tazama, watu washuka kutoka katika vilele vya milima. Zebuli akamwambia, Ni kivuli cha milima unachokiona kama ndio watu. Kisha Gaali akasema mara ya pili, akanena, Angalia, watu washuka katikati ya nchi, na kikosi kimoja kinakuja kwa njia ya mwaloni wa Meonenimu. Ndipo Zebuli akamwambia, Je! Kinywa chako sasa ki wapi, hata ukasema Huyo Abimeleki ni nani, hata inatupasa kumtumikia yeye? Je! Hawa sio watu hao uliowadharau wewe? Haya, toka nje sasa, tafadhali, upigane nao. Basi Gaali akatoka nje mbele ya watu wa Shekemu, akapigana na Abimeleki. Lakini Abimeleki akamkimbiza, naye akakimbia mbele yake, wengi wakaanguka waliojeruhiwa hata kufikilia maingilio ya hilo lango. Abimeleki akakaa Aruma; naye Zebuli akawatoa Gaali na ndugu zake, wasikae katika Shekemu. Ikawa siku ya pili yake, watu wakatoka waende mashambani; naye Abimeleki aliambiwa. Naye akawatwaa watu wake, na kuwagawanya wawe vikosi vitatu, nao wakavizia mashambani; naye akaangalia, na tazama, watu walikuwa watoka humo mjini; basi akainuka na kupigana nao, akawapiga. Abimeleki, na vile vikosi vilivyokuwa pamoja naye, wakafuliza kwenda mbele, wakasimama penye maingilio ya lango la mji, na vile vikosi viwili vikawarukia hao wote waliokuwa mashambani, na kuwapiga. Abimeleki akapigana na huo mji mchana kutwa; akautwaa mji, akawaua watu waliokuwamo ndani yake; kisha akaupomosha mji, na kuutia chumvi. Kisha watu wote waliokaa katika ile buruji ya Shekemu waliposikia habari hiyo wakaingia ndani ya ngome ya nyumba ya El-berithi. Abimeleki aliambiwa ya kuwa watu hao wote wa buruji ya Shekemu wamekutana pamoja. Basi Abimeleki akakwea kwenda kilima cha Salmoni, yeye na wote waliokuwa pamoja naye; naye Abimeleki akashika shoka mkononi mwake, akakata tawi moja katika miti, akalishika na kujitweka fuzini mwake; akawaambia hao watu waliokuwa pamoja naye, Haya, mliyoniona mimi kufanya, fanyeni upesi vivyo, kama nilivyofanya mimi. Basi watu hao wote vivyo wakakata kila mtu tawi lake, wakamwandama Abimeleki, wakayaweka hayo matawi pale ngomeni, na kuiteketeza moto hiyo ngome juu yao; basi hivyo watu wote wa hiyo buruji ya Shekemu wakafa, walipata kama watu elfu, waume kwa wake. Ndipo Abimeleki alipokwenda Thebesi, akapanga kinyume cha Thebesi na kuutwaa. Lakini ndani ya huo mji palikuwa na buruji yenye nguvu, na watu wote waume na wake wakakimbilia huko, na watu wote wa mji, nao wakajifungia ndani, wakapanda paa la buruji. Abimeleki akaiendea hiyo buruji na kupigana nayo; naye akaukaribia mlango wa buruji ili auteketeze kwa moto. Na mwanamke mmoja akabwaga jiwe la kusagia la juu, nalo likampiga Abimeleki kichwani, na kulivunja fuvu la kichwa chake. Ndipo akamwita kwa haraka huyo kijana aliyekuwa anamchukulia silaha zake, na kumwambia, Futa upanga wako, uniue, ili watu wasiseme juu yangu Aliuawa na mwanamke. Basi huyo kijana wake akamchoma upanga, naye akafa. Basi hapo watu wa Israeli walipoona ya kuwa Abimeleki amekufa, wakaondoka wakaenda kila mtu mahali pake. Basi hivyo Mungu akalipiza kisasi juu ya uovu wa Abimeleki aliomtenda baba yake, katika kuwaua hao nduguze watu sabini; uovu wote wa watu wa Shekemu Mungu alilipiza juu ya vichwa vyao; na hiyo laana ya Yothamu mwana wa Yerubaali ikawajilia juu yao.

Shirikisha
Soma Waamuzi 9

Waamuzi 9:22-57 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya Abimeleki kutawala Israeli kwa muda wa miaka mitatu, Mungu akaruhusu roho mbaya kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu, nao watu wa Shekemu wakamtendea Abimeleki kwa hila. Hili lilitokea ili ule ukatili waliotendewa hao wana sabini wa Yerub-Baali upatilizwe, na damu yao iwe juu ya Abimeleki ndugu yao aliyewaua, na pia iwe juu ya watu wa Shekemu, ambao walimsaidia kuua ndugu zake. Hivyo, kutokana na uadui juu yake watu wa Shekemu wakaweka watu wa kumvizia katika vilele vya milima. Wakawanyangʼanya watu wote waliopita karibu nao, nayo haya yakaarifiwa kwa Abimeleki. Basi Gaali mwana wa Ebedi akaenda pamoja na ndugu zake wakaingia Shekemu, nao watu wa huko wakamtumainia yeye. Wakaenda mashambani mwao kuvuna zabibu na kuzisindika hizo zabibu, wakafanya sikukuu katika hekalu la mungu wao. Wakati wakila na kunywa, wakamlaani Abimeleki. Gaali mwana wa Ebedi akasema, “Abimeleki ni nani, na Shekemu ni nani, hata tumtumikie? Je, yeye si mwana wa Yerub-Baali? Naye Zebuli si ndiye msaidizi wake? Basi watumikieni watu wa Hamori, babaye Shekemu. Kwa nini tumtumikie Abimeleki? Laiti watu hawa wangekuwa chini ya amri yangu! Basi mimi ningemwondoa huyo Abimeleki. Ningemwambia Abimeleki, ‘Ondoa jeshi lako lote.’ ” Zebuli aliyekuwa mtawala wa mji aliposikia aliyosema Gaali mwana wa Ebedi, akakasirika sana. Akatuma ujumbe uende kwa Abimeleki kwa siri na kusema, “Gaali mwana wa Ebedi na ndugu zake wamekuja Shekemu, na wanauchochea mji huu kinyume chako. Sasa, basi, usiku huu wewe uondoke na watu wako ili mje kuwavizia mashambani. Kisha asubuhi wakati wa kuchomoza jua, amka mapema na ujipange dhidi ya huo mji. Wakati yeye na jeshi lililo pamoja naye watakapotoka kukabiliana nanyi, mwaweza kuwatendea kwa kadiri mnavyoweza.” Kwa hiyo Abimeleki pamoja na jeshi lake lote wakaondoka usiku na kujificha karibu na Shekemu wakiwa vikosi vinne. Basi Gaali mwana wa Ebedi alikuwa ametoka nje akawa amesimama katika ingilio la mji wakati ule ule ambao Abimeleki na watu wake walipokuwa wanatoka sehemu zao za maficho. Gaali alipowaona, akamwambia Zebuli, “Tazama, watu wanashuka kutoka kwenye vilele vya milima!” Zebuli akajibu, “Wewe unaona vivuli vya milima kana kwamba ni watu.” Lakini Gaali akasema tena, “Tazama, watu wanashuka kutoka katikati ya nchi na kikosi kimoja kinakuja kutoka Tabur-Ezeri na kikosi kingine kutoka upande wa Elon-Meonenimu.” Ndipo Zebuli akamwambia, “Kuko wapi kujivuna kwako sasa, wewe uliyesema, ‘Huyo Abimeleki ni nani hata tumtumikie?’ Hawa si wale watu uliowadharau? Toka nje sasa ukapigane nao!” Basi Gaali akatoka akawaongoza watu wa Shekemu kupigana na Abimeleki. Abimeleki akamfukuza, watu wengi wakajeruhiwa katika kukimbia huko, njia nzima hadi kwenye ingilio la lango. Abimeleki akakaa Aruma, naye Zebuli akawafukuza Gaali na ndugu zake watoke Shekemu. Kesho yake watu wa Shekemu wakatoka wakaenda mashambani, Abimeleki akaambiwa juu ya jambo hili. Hivyo akawachukua watu wake, akawagawanya katika vikosi vitatu na kuwaweka waviziao huko mashambani. Alipowaona watu wanatoka kwenda nje ya mji, akainuka dhidi yao na kuwashambulia. Abimeleki pamoja na vile vikosi wakaharakisha kwenda mbele kwenye nafasi, mahali pa ingilio la lango la mji. Vile vikosi viwili vikawawahi wale waliokuwa mashambani na kuwaua. Siku hiyo nzima Abimeleki akazidisha mashambulizi yake dhidi ya mji hadi akawa ameuteka na kuwaua watu wa huo mji. Kisha akauangamiza mji na kusambaza chumvi juu yake. Kwa kusikia jambo hili watu wote katika mnara wa Shekemu, wakaingia kwenye ngome ya hekalu la El-Berithi. Abimeleki aliposikia kuwa wamekusanyika huko, yeye na watu wake wote wakakwea kwenye Mlima Salmoni. Abimeleki akachukua shoka, akakata baadhi ya matawi, ambayo aliyachukua mabegani. Akawaagiza wale watu waliokuwa pamoja naye kuwa, “Fanyeni kile mlichoona mimi nikifanya!” Basi watu wote wakakata matawi na kumfuata Abimeleki. Wakayakusanya hayo matawi juu ya ngome na kuitia moto ili kuwachoma wale watu wote waliokuwa ndani yake. Hivyo watu wote katika mnara wa Shekemu, karibia watu 1,000 waume kwa wake, pia wakafa. Baadaye Abimeleki akaenda Thebesi na kuuzingira kwa jeshi na kuuteka. Hata hivyo, ndani ya huo mji kulikuwa na mnara imara, ambako watu wote wa mji wanaume na wanawake, watu wote wa mji, walikimbilia ndani yake. Wakajifungia ndani yake na kupanda juu ya paa la mnara. Abimeleki akaja kwenye ule mnara na kuushambulia, lakini alipokaribia kwenye ingilio la mnara ili kuuchoma kwa moto, mwanamke mmoja akaangusha sehemu ya juu ya jiwe la kusagia juu ya kichwa cha Abimeleki, likapasua fuvu la kichwa chake. Akamwita kwa haraka kijana yule aliyechukua silaha zake, na kumwambia, “Chukua upanga wako na uniue, watu wasije wakasema kwamba, ‘Mwanamke amemuua.’ ” Basi yule kijana akamchoma upanga, naye akafa. Waisraeli walipoona kuwa Abimeleki amekufa, kila mtu akaenda nyumbani kwake. Hivyo ndivyo Mungu alivyolipiza uovu ule ambao Abimeleki alikuwa ameutenda kwa baba yake kwa kuwaua ndugu zake sabini. Mungu akawapatiliza watu wa Shekemu uovu wao juu ya vichwa vyao, na juu yao ikaja laana ya Yothamu mwana wa Yerub-Baali.

Shirikisha
Soma Waamuzi 9

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha