Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 52

52
1Amka, amka, ee Sayuni,
jivike nguvu.
Vaa mavazi yako ya fahari,
ee Yerusalemu, mji mtakatifu.
Asiyetahiriwa na aliye najisi
hataingia kwako tena.
2Jikung’ute mavumbi yako,
inuka, uketi kwenye kiti cha utawala, ee Yerusalemu.
Jifungue minyororo iliyo shingoni mwako,
ee Binti Sayuni uliye mateka.
3Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Mliuzwa pasipo malipo,
nanyi mtakombolewa bila fedha.”
4Kwa maana hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:
“Hapo kwanza watu wangu walishuka Misri kuishi,
hatimaye, Ashuru wakawadhulumu.
5“Basi sasa nina nini hapa?” asema Mwenyezi Mungu.
“Kwa kuwa watu wangu wamechukuliwa pasipo malipo,
nao wale wanaowatawala wanawadhihaki,”
asema Mwenyezi Mungu.
“Mchana kutwa
jina langu limetukanwa bila kikomo.
6Kwa hiyo watu wangu watalijua Jina langu;
kwa hiyo katika siku ile watajua
kwamba ndimi niliyetangulia kulisema.
Naam, ni mimi.”
7Tazama jinsi miguu ya wale waletao habari njema
ilivyo mizuri juu ya milima,
wale wanaotangaza amani,
wanaoleta habari njema,
wanaotangaza wokovu,
wauambiao Sayuni,
“Mungu wako anatawala!”
8Sikiliza! Walinzi wako wanapaza sauti zao,
pamoja wanapaza sauti zao kwa furaha.
Mwenyezi Mungu atakaporejea Sayuni,
wataliona kwa macho yao wenyewe.
9Pazeni sauti ya nyimbo za furaha pamoja,
enyi magofu ya Yerusalemu,
kwa maana Mwenyezi Mungu amewafariji watu wake,
ameikomboa Yerusalemu.
10Mkono mtakatifu wa Mwenyezi Mungu umefunuliwa
machoni pa mataifa yote,
nayo miisho yote ya dunia itaona
wokovu wa Mungu wetu.
11Ondokeni, ondokeni, tokeni huko!
Msiguse kitu chochote kilicho najisi!
Tokeni kati yake mwe safi,
ninyi mchukuao vyombo vya Mwenyezi Mungu.
12Lakini hamtaondoka kwa haraka,
wala hamtaenda kwa kukimbia;
kwa maana Mwenyezi Mungu atatangulia mbele yenu,
Mungu wa Israeli atakuwa mlinzi nyuma yenu.
Mateso na utukufu wa mtumishi
13Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa hekima;
atatukuzwa, na kuinuliwa juu, na kukwezwa sana.
14Kama walivyokuwa wengi
walioshangazwa naye,
kwani uso wake ulikuwa umeharibiwa sana
zaidi ya mtu yeyote
na umbo lake kuharibiwa
zaidi ya mfano wa mwanadamu:
15hivyo atayashangaza mataifa mengi,
nao wafalme watafunga vinywa vyao kwa sababu yake.
Kwa kuwa yale ambayo hawakuambiwa, watayaona,
nayo yale wasiyoyasikia, watayafahamu.

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 52: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia