Isaya 41:1-16
Isaya 41:1-16 NENO
“Nyamazeni kimya mbele zangu, enyi visiwa! Mataifa na wafanye upya nguvu zao! Wao na wajitokeze, kisha waseme, tukutane pamoja mahali pa hukumu. “Ni nani aliyemchochea mmoja kutoka mashariki, akimwita katika haki kwa utumishi wake? Huyatia mataifa mkononi mwake, na kuwatiisha wafalme mbele zake. Huwafanya kuwa mavumbi kwa upanga wake, huwafanya makapi yapeperushwayo na upepo kwa upinde wake. Huwafuatia na kuendelea salama, katika njia ambayo miguu yake haijawahi kupita. Ni nani aliyefanya jambo hili na kulitimiliza, akiita vizazi tangu mwanzo? Mimi, Mwenyezi Mungu, ni wa kwanza, nami nitakuwa pamoja na wa mwisho: Mimi ndiye.” Visiwa vimeliona na kuogopa, miisho ya dunia inatetemeka. Wanakaribia na kuja mbele, kila mmoja humsaidia mwingine na kusema kwa ndugu yake, “Uwe hodari!” Fundi humtia moyo sonara, yeye alainishaye kwa nyundo humhimiza yeye agongeaye kwenye fuawe. Humwambia yeye aunganishaye, “Ni kazi njema.” Naye huikaza sanamu kwa misumari ili isitikisike. “Lakini wewe, ee Israeli, mtumishi wangu, Yakobo, niliyemchagua, ninyi wazao wa Ibrahimu rafiki yangu, nilikuchukua toka miisho ya dunia, nilikuita kutoka pembe zake za mbali. Nilisema, ‘Wewe ni mtumishi wangu’; nimekuchagua, wala sikukukataa. Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako. Nitakutia nguvu na kukusaidia; nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu. “Wote walioona hasira dhidi yako hakika wataaibika na kutahayarika, wale wakupingao watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia. Ingawa utawatafuta adui zako, hutawaona. Wale wanaopigana vita dhidi yako watakuwa kama vile si kitu kabisa. Kwa maana Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, nikushikaye mkono wako wa kuume na kukuambia, Usiwe na hofu, nitakusaidia. Usiogope, ee Yakobo uliye mdudu, ee Israeli uliye mdogo, kwa kuwa Mimi mwenyewe nitakusaidia,” asema Mwenyezi Mungu, Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli. “Tazama, nitakufanya chombo cha kupuria, kipya na chenye makali, chenye meno mengi. Utaipura milima na kuiponda na kuvifanya vilima kuwa kama makapi. Utaipepeta, nao upepo utaichukua, dhoruba itaipeperushia mbali. Bali wewe utajifurahisha katika Mwenyezi Mungu na katika utukufu wa yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.