Isaya 41:1-16
Isaya 41:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Mungu asema hivi: “Enyi wakazi wa mbali nyamazeni mnisikilize! Enyi mataifa jipeni nguvu; jitokezeni mkatoe hoja zenu, na tuje pamoja kwa hukumu. “Nani, ila mimi, aliyemwita shujaa toka mashariki, mtu ambaye hupata ushindi popote aendako? Mimi huyatia mataifa makuchani mwake, naye huwaponda wafalme chini ya miguu yake! Upanga wake huwafanya kuwa kama vumbi, kwa upinde wake huwapeperusha kama makapi. Yeye huwafuatia na kupita salama; huenda kasi kana kwamba hagusi chini. Nani aliyefanya yote haya yatendeke? Ni nani aliyepanga wakati wa kila tukio? Mimi Mwenyezi-Mungu nipo tangu mwanzo, mimi nitakuwapo hata milele. “Wakazi wa mbali wameona niliyotenda, wakaogopa; dunia yote inatetemeka kwa hofu. Watu wote wamekusanyika, wakaja. Kila mmoja anamhimiza mwenzake akisema, ‘Haya! Jipe moyo!’ Fundi anamhimiza mfua dhahabu, naye alainishaye sanamu kwa nyundo, anamhimiza anayeiunga kwa misumari. Wote wanasema, ‘Imeungika vizuri sana!’ Kisha wanaifunga kwa misumari isitikisike. “Sikiliza ewe Israeli, mtumishi wangu, wewe, Yakobo ambaye nimekuchagua, wewe mzawa wa Abrahamu, rafiki yangu; wewe niliyekuleta toka miisho ya dunia, wewe niliyekuambia: ‘Wewe u mtumishi wangu; mimi sikukutupa, bali nilikuchagua.’ Basi, usiogope, mimi nipo pamoja nawe. Usifadhaike, mimi ni Mungu wako. Nitakuimarisha na kukusaidia; nitakulinda kwa mkono wangu wa ushindi. “Naam! Wote waliokuwakia hasira, wataaibishwa na kupata fedheha. Wote wanaopingana nawe, watakuwa si kitu na kuangamia. Utawatafuta hao wanaopingana nawe, lakini watakuwa wameangamia. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ndimi ninayetegemeza mkono wako. Mimi ndimi ninayekuambia: ‘Usiogope, nitakusaidia.’” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Enyi watu wa Yakobo dhaifu kama mdudu, enyi Waisraeli, msiogope! Mimi Mwenyezi-Mungu nasema nitawasaidia. Mimi ni Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli. Nitawafanya muwe kama chombo cha kupuria, chenye meno mapya na makali. Mtaipura milima na kuipondaponda; vilima mtavisagasaga kama makapi. Mtaipepeta milima hiyo, nao upepo utaipeperushia mbali, naam, dhoruba itaitawanya huko na huko. Nanyi mtafurahi kwa sababu yangu Mwenyezi-Mungu; mtaona fahari kwa sababu yangu Mungu Mtakatifu wa Israeli.
Isaya 41:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nyamazeni mbele zangu, enyi visiwa, na mataifa wajipatie nguvu mpya; na waje karibu wakanene; na tukaribiane pamoja kwa hukumu. Ni nani aliyemwinua mmoja atokaye mashariki, ambaye katika haki amemwita mguuni pake? Ampa mataifa mbele yake, na kumtawaza juu ya wafalme; awatoa wawe kama mavumbi kwa upanga wake, kama makapi yaliyopeperushwa kwa upinde wake. Awafuatia, apita salama hata kwa njia asiyoikanyaga kamwe kwa miguu yake. Ni nani aliyetenda na kufanya jambo hilo, aviitaye vizazi tangu mwanzo? Mimi, BWANA, wa kwanza na wa mwisho, mimi ndiye. Visiwa vimeona, vikaogopa; ncha za dunia zilitetemeka; walikaribia, walikuja. Wakasaidiana, kila mtu na mwenzake, kila mtu akamwambia ndugu yake; Jipe moyo. Seremala akamtia moyo mfua dhahabu, na yeye alainishaye kwa nyundo akamhimiza yule apigaye fuawe, akiisifu kazi ya kuunga, akisema, Ni kazi njema; naye akaikaza kwa misumari isitikisike. Nawe, Israeli, mtumishi wangu; Yakobo, niliyekuchagua; mzao wa Abrahamu, rafiki yangu; wewe niliyekushika toka miisho ya dunia, na kukuita toka pembe zake, nikikuambia, Wewe u mtumishi wangu; nimekuchagua wala sikukutupa; usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kulia wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kulia, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia. Usiogope, Yakobo uliye mdudu, nanyi watu wa Israeli; mimi nitakusaidia, asema BWANA, na mkombozi wako ni Mtakatifu wa Israeli. Tazama, nitakufanya kuwa chombo kikali kipya cha kupuria, chenye meno; utaifikicha milima, na kuisaga; nawe utafanya vilima kuwa kama makapi. Utawapepeta, na upepo utawapeperusha; upepo wa kisulisuli utawatawanya; nawe utamfurahia BWANA, utajitukuza katika Mtakatifu wa Israeli.
Isaya 41:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nyamazeni mbele zangu, enyi visiwa, na mataifa wajipatie nguvu mpya; na waje karibu wakanene; na tukaribiane pamoja kwa hukumu. Ni nani aliyemwinua mmoja atokaye mashariki, ambaye katika haki amemwita mguuni pake? Ampa mataifa mbele yake, na kumtawaza juu ya wafalme; awatoa wawe kama mavumbi kwa upanga wake, kama makapi yaliyopeperushwa kwa upinde wake. Awafuatia, apita salama hata kwa njia asiyoikanyaga kamwe kwa miguu yake. Ni nani aliyetenda na kufanya jambo hilo, aviitaye vizazi tangu mwanzo? Mimi, BWANA, wa kwanza na wa mwisho, mimi ndiye. Visiwa vimeona, vikaogopa; ncha za dunia zilitetemeka; walikaribia, walikuja. Wakasaidiana, kila mtu na mwenzake, kila mtu akamwambia ndugu yake; Uwe na moyo mkuu. Seremala akamtia moyo mfua dhahabu, na yeye alainishaye kwa nyundo akamhimiza yule apigaye fuawe, akiisifu kazi ya kuunga, akisema, Ni kazi njema; naye akaikaza kwa misumari isitikisike. Nawe, Israeli, mtumishi wangu; Yakobo, niliyekuchagua; mzao wa Ibrahimu, rafiki yangu; wewe niliyekushika toka miisho ya dunia, na kukuita toka pembe zake, nikikuambia, Wewe u mtumishi wangu; nimekuchagua wala sikukutupa; usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia. Usiogope, Yakobo uliye mdudu, nanyi watu wa Israeli; mimi nitakusaidia, asema BWANA, na mkombozi wako ni Mtakatifu wa Israeli. Tazama, nitakufanya kuwa chombo kikali kipya cha kupuria, chenye meno; utaifikicha milima, na kuisaga; nawe utafanya vilima kuwa kama makapi. Utawapepeta, na upepo utawapeperusha; upepo wa kisulisuli utawatawanya; nawe utamfurahia BWANA, utajitukuza katika Mtakatifu wa Israeli.
Isaya 41:1-16 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Nyamazeni kimya mbele zangu, enyi visiwa! Mataifa na wafanye upya nguvu zao! Wao na wajitokeze, kisha waseme, tukutane pamoja mahali pa hukumu. “Ni nani aliyemchochea mmoja kutoka mashariki, akimwita katika haki kwa utumishi wake? Huyatia mataifa mkononi mwake, na kuwatiisha wafalme mbele zake. Huwafanya kuwa mavumbi kwa upanga wake, huwafanya makapi yapeperushwayo na upepo kwa upinde wake. Huwafuatia na kuendelea salama, katika njia ambayo miguu yake haijawahi kupita. Ni nani aliyefanya jambo hili na kulitimiliza, akiita vizazi tangu mwanzo? Mimi, Mwenyezi Mungu, ni wa kwanza, nami nitakuwa pamoja na wa mwisho: Mimi ndiye.” Visiwa vimeliona na kuogopa, miisho ya dunia inatetemeka. Wanakaribia na kuja mbele, kila mmoja humsaidia mwingine na kusema kwa ndugu yake, “Uwe hodari!” Fundi humtia moyo sonara, yeye alainishaye kwa nyundo humhimiza yeye agongeaye kwenye fuawe. Humwambia yeye aunganishaye, “Ni kazi njema.” Naye huikaza sanamu kwa misumari ili isitikisike. “Lakini wewe, ee Israeli, mtumishi wangu, Yakobo, niliyemchagua, ninyi wazao wa Ibrahimu rafiki yangu, nilikuchukua toka miisho ya dunia, nilikuita kutoka pembe zake za mbali. Nilisema, ‘Wewe ni mtumishi wangu’; nimekuchagua, wala sikukukataa. Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako. Nitakutia nguvu na kukusaidia; nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu. “Wote walioona hasira dhidi yako hakika wataaibika na kutahayarika, wale wakupingao watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia. Ingawa utawatafuta adui zako, hutawaona. Wale wanaopigana vita dhidi yako watakuwa kama vile si kitu kabisa. Kwa maana Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako, nikushikaye mkono wako wa kuume na kukuambia, Usiwe na hofu, nitakusaidia. Usiogope, ee Yakobo uliye mdudu, ee Israeli uliye mdogo, kwa kuwa Mimi mwenyewe nitakusaidia,” asema Mwenyezi Mungu, Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli. “Tazama, nitakufanya chombo cha kupuria, kipya na chenye makali, chenye meno mengi. Utaipura milima na kuiponda na kuvifanya vilima kuwa kama makapi. Utaipepeta, nao upepo utaichukua, dhoruba itaipeperushia mbali. Bali wewe utajifurahisha katika Mwenyezi Mungu na katika utukufu wa yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.