Isaya 3
3
Hukumu kwa Yerusalemu na Yuda
1Tazama sasa, Bwana,
Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,
yu karibu kuwaondolea Yerusalemu na Yuda
upatikanaji wa mahitaji na misaada,
upatikanaji wote wa chakula na tegemeo lote la maji,
2shujaa na mtu wa vita,
mwamuzi na nabii,
mwaguzi na mzee,
3jemadari wa kikosi cha watu hamsini
na mtu mwenye cheo, mshauri,
fundi stadi na msihiri mjanja.
4Nitawafanya wavulana wawe viongozi wao;
watoto ndio watakaowatawala.
5Watu watadhulumiana:
mtu dhidi ya mtu, na jirani dhidi ya jirani yake.
Kijana atainuka dhidi ya mzee,
mtu mnyonge dhidi ya mtu mwenye heshima.
6Mtu atamkamata mmoja wa ndugu zake
katika nyumba ya baba yake na kusema,
“Unalo joho, sasa uwe kiongozi wetu,
tawala lundo hili la magofu!”
7Lakini siku hiyo atapiga kelele akisema,
“Sina msaada.
Sina chakula wala mavazi katika nyumba yangu,
msinifanye niwe kiongozi wa watu.”
8Yerusalemu inapepesuka,
Yuda inaanguka;
maneno yao na matendo yao ni kinyume na Mwenyezi Mungu,
wakiudharau uwepo wake uliotukuka.
9Nyuso zao zinavyoonekana zinashuhudia dhidi yao,
hujivunia dhambi yao kama Sodoma,
wala hawaifichi.
Ole wao!
Wamejiletea maafa juu yao wenyewe.
10Waambie wanyofu itakuwa heri kwao,
kwa kuwa watafurahia tunda la matendo yao.
11Ole kwa watu waovu! Maafa yapo juu yao!
Watalipwa kwa ajili ya yale mikono yao iliyotenda.
12Vijana wanawatesa watu wangu,
wanawake wanawatawala.
Enyi watu wangu, viongozi wenu wanawapotosha,
wanawapoteza njia.
13Mwenyezi Mungu anachukua nafasi yake mahakamani,
anasimama kuhukumu watu.
14Mwenyezi Mungu anaingia katika hukumu
dhidi ya wazee na viongozi wa watu wake:
“Ninyi ndio mlioharibu shamba langu la mizabibu,
mali iliyonyang’anywa maskini imo nyumbani mwenu.
15Mnamaanisha nini kuwaponda watu wangu
na kuzisaga nyuso za maskini?”
asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
16Mwenyezi Mungu asema,
“Wanawake wa Sayuni wana kiburi,
wanatembea na shingo ndefu,
wakikonyeza kwa macho yao,
wanatembea kwa hatua za madaha,
wakiwa na mapambo ya njuga kwenye vifundo vya miguu yao.
17Kwa hiyo Bwana ataleta majipu kwenye vichwa vya wanawake wa Sayuni;
Mwenyezi Mungu atazifanya ngozi za vichwa vyao kuwa vipara.”
18Katika siku ile Bwana atawanyang’anya uzuri wao: bangili, tepe za kichwani, mikufu yenye alama za mwezi mwandamo, 19vipuli, vikuku, shela, 20vilemba, mikufu ya vifundo vya miguu, mshipi, chupa za manukato na hirizi, 21pete zenye muhuri, pete za puani, 22majoho mazuri, mitandio, mavazi, kifuko cha kutilia fedha, 23vioo, mavazi ya kitani, taji na shali.
24Badala ya harufu ya manukato kutakuwa na uvundo;
badala ya mishipi, ni kamba;
badala ya nywele zilizotengenezwa vizuri, ni upara;
badala ya mavazi mazuri, ni magunia;
badala ya uzuri, ni alama ya aibu kwa chuma cha moto.
25Wanaume wako watauawa kwa upanga,
nao mashujaa wako watauawa vitani.
26Malango ya Sayuni yataomboleza na kulia,
ataketi mavumbini akiwa fukara.
Iliyochaguliwa sasa
Isaya 3: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.