Isaya 19:18-25
Isaya 19:18-25 NENO
Katika siku hiyo miji mitano ya Misri, itazungumza lugha ya Kanaani, na kuapa kumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. Mji mmoja utaitwa Mji wa Uharibifu. Katika siku hiyo patakuwa na madhabahu ya Mwenyezi Mungu katikati ya Misri na mnara wa kumbukumbu kwa Mwenyezi Mungu kwenye mpaka wa Misri. Itakuwa alama na ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni katika nchi ya Misri. Watakapomlilia Mwenyezi Mungu kwa sababu ya watesi wao, Mungu atawapelekea mwokozi na mtetezi, naye atawaokoa. Hivyo Mwenyezi Mungu atajijulisha mwenyewe kwa Wamisri, nao katika siku hiyo watamkubali Mwenyezi Mungu. Wataabudu kwa kumtolea dhabihu na sadaka za nafaka, watamwekea Mwenyezi Mungu nadhiri na kuzitimiza. Mwenyezi Mungu ataipiga Misri kwa tauni; atawapiga na kuwaponya. Watamgeukia Mwenyezi Mungu, naye atayasikia maombi yao na kuwaponya. Katika siku hiyo kutakuwa na njia kuu kutoka Misri hadi Ashuru. Waashuru wataenda Misri, na Wamisri wataenda Ashuru. Wamisri na Waashuru wataabudu pamoja. Katika siku hiyo Israeli itakuwa ya tatu, pamoja na Misri na Ashuru, nao watakuwa baraka kwa dunia. Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni atawabariki, akisema, “Baraka iwe kwa Misri watu wangu, kwa Ashuru kazi ya mikono yangu, na kwa Israeli urithi wangu.”