Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 16

16
Hali ya kukata tamaa ya Moabu
1Pelekeni wana-kondoo kama ushuru
kwa mtawala wa nchi,
Kutoka Sela, kupitia jangwani,
hadi mlima wa Binti Sayuni.
2Kama ndege wanaopapatika
waliofukuzwa kutoka kiota,
ndivyo walivyo wanawake wa Moabu
kwenye vivuko vya Mto Arnoni.
3“Tupeni shauri,
toeni uamuzi.
Wakati wa adhuhuri,
fanyeni kivuli chenu kama usiku.
Waficheni watoro,
msisaliti wakimbizi.
4Waacheni watoro wa Moabu wakae pamoja nanyi;
kuweni mahali pao pa salama ili kuepuka mwangamizi.”
Mtesi atafikia mwisho na maangamizi yatakoma,
aletaye vita atatoweka kutoka nchi.
5Kwa upendo kiti cha utawala kitaimarishwa,
kwa uaminifu mtu ataketi juu yake,
yeye atokaye nyumba ya Daudi:
yeye ambaye katika kuhukumu hutafuta haki,
na huhimiza njia ya haki.
6Tumesikia juu ya kiburi cha Moabu:
kiburi chake cha kujivuna na udanganyifu,
kiburi chake na ufidhuli wake,
lakini majivuno yake si kitu.
7Kwa hiyo Wamoabu wanaomboleza,
wanaiombolezea Moabu kwa pamoja.
Wanaomboleza na kuhuzunika
kwa ajili ya watu wa Kir-Haresethi.
8Mashamba ya Heshboni yananyauka,
pia na mizabibu ya Sibma.
Watawala wa mataifa
wamekanyaga mizabibu iliyo mizuri sana,
ambayo ilipata kufika Yazeri
na kuenea kuelekea jangwani.
Machipukizi yake yalienea
yakafika hadi baharini.
9Hivyo ninalia kama Yazeri aliavyo,
kwa ajili ya mizabibu ya Sibma.
Ee Heshboni, ee Eleale,
ninakulowesha kwa machozi!
Shangwe za furaha kwa ajili ya tunda lako lililoiva
na kwa ajili ya mavuno zimekomeshwa.
10Furaha na shangwe zimeondolewa
kutoka mashamba ya matunda;
hakuna yeyote aimbaye wala apazaye sauti
katika mashamba ya mizabibu;
hakuna yeyote akanyagaye zabibu shinikizoni,
kwa kuwa nimekomesha makelele.
11Moyo wangu unaomboleza kwa ajili ya Moabu kama kinubi,
nafsi yangu yote kwa ajili ya Kir-Haresethi.
12Moabu anapojitokeza mahali pake pa juu pa kuabudia,
anajichosha mwenyewe tu;
anapoenda mahali pake pa ibada za sanamu ili kuomba,
haitamfaidi lolote.
13Hili ndilo neno ambalo Mwenyezi Mungu ameshasema kuhusu Moabu. 14Lakini sasa Mwenyezi Mungu anasema: “Katika miaka mitatu, kama vile mtumishi aliyefungwa na mkataba angeihesabu, fahari ya Moabu na watu wake wengi watadharauliwa, nao walionusurika watakuwa wachache sana, tena wanyonge.”

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 16: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia