Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 13

13
Unabii dhidi ya Babeli
1Neno la unabii kuhusu Babeli ambalo Isaya mwana wa Amozi aliliona:
2Twekeni bendera juu ya mlima usio na kitu,
wapazieni sauti,
wapungieni mkono waingie
katika malango ya wenye heshima.
3Nimewaamuru watakatifu wangu;
nimewaita mashujaa wangu waitimize hasira yangu:
wale wanaoshangilia ushindi wangu.
4Sikilizeni kelele juu ya milima,
kama ile ya umati mkubwa wa watu!
Sikilizeni, makelele katika falme,
kama mataifa yanayokusanyika pamoja!
Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni anakusanya
jeshi kwa ajili ya vita.
5Wanakuja kutoka nchi za mbali sana,
kutoka miisho ya mbingu,
Mwenyezi Mungu na silaha za ghadhabu yake,
kuangamiza nchi yote.
6Ombolezeni, kwa maana siku ya Mwenyezi Mungu i karibu,
itakuja kama uharibifu kutoka kwa Mwenyezi#13:6 Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania..
7Kwa sababu ya hili, mikono yote italegea,
moyo wa kila mtu utayeyuka.
8Hofu itawakamata,
uchungu na maumivu makali yatawashika,
watagaagaa kama mwanamke aliye na uchungu wa kuzaa.
Watatazamana kwa hofu kila mtu na mwenzake,
nyuso zao zikiwaka kama moto.
9Tazameni, siku ya Mwenyezi Mungu inakuja,
siku katili, yenye ghadhabu na hasira kali,
kuifanya nchi kuwa ukiwa,
na kuwaangamiza wenye dhambi waliomo.
10Nyota za mbinguni na makundi ya nyota
havitatoa mwanga wake.
Jua linalochomoza litatiwa giza
na mwezi hautatoa nuru yake.
11Nitauadhibu ulimwengu kwa ajili ya uovu wake,
waovu kwa ajili ya dhambi zao.
Nitakomesha majivuno ya wenye kiburi,
na nitakishusha kiburi cha watu wakatili.
12Nitawafanya wanadamu kuwa adimu kuliko dhahabu safi,
watakuwa wachache sana kuliko dhahabu ya Ofiri.
13Kwa hiyo nitazifanya mbingu zitetemeke,
nayo dunia itatikisika kutoka mahali pake
katika ghadhabu ya Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni,
katika siku ya hasira yake iwakayo.
14Kama paa awindwaye,
kama kondoo wasio na mchungaji,
kila mmoja atarudi kwa watu wake mwenyewe,
kila mmoja atakimbilia nchi yake ya kuzaliwa.
15Yeyote atakayetekwa atapasuliwa tumbo,
wote watakaokamatwa watauawa kwa upanga.
16Watoto wao wachanga watavunjwa vipande vipande
mbele ya macho yao;
nyumba zao zitatekwa,
na wake zao watanajisiwa.
17Tazama, nitawachochea Wamedi dhidi yao,
ambao hawajali fedha
wala hawafurahii dhahabu.
18Mishale yao itawaangusha vijana,
hawatakuwa na huruma kwa watoto wachanga
wala hawataangalia watoto kwa huruma.
19Babeli, johari ya falme,
utukufu wa kiburi cha Wababeli#13:19 yaani Wakaldayo,
utaangushwa na Mungu
kama Sodoma na Gomora.
20Hautakaliwa na watu kamwe,
wala watu hawataishi humo kwa vizazi vyote.
Hakuna Mwarabu atakayepiga hema lake huko,
hakuna mchungaji atakayepumzisha makundi yake huko.
21Lakini viumbe wa jangwani watalala huko,
mbweha watajaza nyumba zake,
bundi wataishi humo
nao mbuzi-mwitu watarukaruka humo.
22Fisi watalia ndani ya ngome zake,
mbweha ndani ya majumba yake ya kifahari.
Wakati wake umewadia,
na siku zake hazitaongezwa.

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 13: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia