Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Habakuki 3

3
Maombi ya Habakuki
1Sala ya nabii Habakuki iliyoimbwa kwa shigionothi#3:1 Ni kifaa cha uimbaji chenye nyuzi; pia maombi kutumia kifaa hiki..
2Mwenyezi Mungu, nimezisikia sifa zako;
nami naogopa kwa matendo yako, Ee Mwenyezi Mungu.
Fufua kazi yako katika siku hizi zetu,
tangaza habari yako wakati huu wetu;
katika ghadhabu kumbuka rehema.
3Mungu alitoka Temani,
yeye Aliye Mtakatifu kutoka Mlima Parani.
Utukufu wake ulifunika mbingu,
na sifa zake zikaifunika dunia.
4Mng’ao wake ulikuwa kama jua linapochomoza;
miali ilimulika kutoka mkononi mwake,
ambako nguvu zake zilifichwa.
5Tauni ilimtangulia;
maradhi ya kuambukiza yalifuata nyayo zake.
6Alisimama, akaitikisa dunia;
alitazama, na kuyafanya mataifa yatetemeke.
Milima ya zamani iligeuka mavumbi
na vilima vilivyozeeka vikaanguka.
Njia zake ni za milele.
7Niliona watu wa Kushani katika dhiki,
na makazi ya Midiani katika maumivu makali.
8Ee Mwenyezi Mungu, uliikasirikia mito?
Je, ghadhabu yako ilikuwa dhidi ya vijito?
Je, ulighadhibikia bahari
ulipoendesha farasi wako
na magari yako ya vita ili ushinde?
9Uliufunua upinde wako
na kuitisha mishale mingi.
Uliigawa dunia kwa mito;
10milima ilikuona ikatetemeka.
Mafuriko ya maji yakapita huko;
vilindi vilinguruma
na kuinua mawimbi yake juu.
11Jua na mwezi vilisimama kimya mbinguni
katika mng’ao wa mishale yako inayoruka,
na katika mng’ao wa mkuki wako umeremetao.
12Kwa ghadhabu ulipitia kwenye dunia,
na katika hasira ulikanyaga mataifa.
13Ulikuja kuwaokoa watu wako,
kumwokoa uliyempaka mafuta.
Ulimponda kiongozi wa nchi ya uovu,
ukamvua toka kichwani hadi wayo.
14Kwa mkuki wake mwenyewe ulitoboa kichwa chake
wakati mashujaa wake walifurika nje kwa kishindo kututawanya,
wakifurahi kama walio karibu kutafuna
wale wanyonge waliokuwa mafichoni.
15Ulikanyaga bahari kwa farasi wako,
ukisukasuka maji makuu.
16Nilisikia na moyo wangu ukagonga kwa nguvu,
midomo yangu ikatetemeka kwa hofu niliposikia sauti;
uchakavu ukanyemelea mifupa yangu,
na miguu yangu ikatetemeka.
Hata hivyo nitasubiri kwa uvumilivu siku ya maafa
kuyajilia mataifa yaliyotuvamia.
17Ingawa mtini hauchanui maua
na hakuna zabibu juu ya mizabibu,
ingawaje mzeituni hauzai,
na hata mashamba hayatoi chakula,
iwapo hakuna kondoo katika banda,
wala ng’ombe katika zizi,
18hata hivyo nitashangilia katika Mwenyezi Mungu,
nitamfurahia Mungu Mwokozi wangu.
19Bwana Mungu Mwenyezi ni nguvu yangu;
huifanya miguu yangu kama miguu ya ayala,
huniwezesha kupita juu ya vilima.
Kwa kiongozi wa uimbaji. Kwa vinanda vyangu vya nyuzi.

Iliyochaguliwa sasa

Habakuki 3: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia