Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 47:23-31

Mwanzo 47:23-31 NENO

Yusufu akawaambia watu, “Kwa vile nimewanunua ninyi pamoja na nchi yenu leo kuwa mali ya Farao, hapa kuna mbegu kwa ajili yenu ili mweze kuziotesha. Lakini wakati mazao yatakapokuwa tayari, mpeni Farao sehemu ya tano. Sehemu hizo nne zitakazobaki mtaziweka kama mbegu kwa ajili ya mashamba, na kwa ajili ya chakula chenu wenyewe, na cha watu wa nyumbani mwenu na watoto wenu.” Wakamwambia, “Umeokoa maisha yetu. Basi na tupate kibali mbele ya macho ya bwana wetu; tutakuwa watumwa wa Farao.” Basi Yusufu akaiweka iwe sheria ya ardhi katika nchi ya Misri, ambayo inatumika hata leo, kwamba sehemu ya tano ya mazao ni mali ya Farao. Ni ardhi ya makuhani tu ambayo haikuwa ya Farao. Basi Waisraeli wakaishi Misri katika nchi ya Gosheni. Wakapata mali huko, wakastawi na kuongezeka kwa idadi. Yakobo akaishi Misri miaka kumi na saba, nayo miaka ya maisha yake ilikuwa mia moja na arobaini na saba (147). Wakati ulipokaribia wa Israeli kufa, akamwita mwanawe Yusufu na kumwambia, “Kama nimepata kibali machoni pake, weka mkono wako chini ya paja langu na uniahidi kuwa utanifanyia fadhili na uaminifu. Usinizike Misri, lakini nitakapopumzika na baba zangu, unichukue kutoka Misri, ukanizike walipozikwa.” Yusufu akamwambia, “Nitafanya kama unavyosema.” Akamwambia, “Niapie.” Ndipo Yusufu akamwapia, naye Israeli akaabudu akiwa ameegemea juu ya kichwa cha fimbo yake.