Mwanzo 47
47
Yakobo ambariki Farao
1Yusufu akaenda na kumwambia Farao, “Baba yangu na ndugu zangu wamekuja kutoka nchi ya Kanaani wakiwa na makundi yao ya kondoo, mbuzi na ng’ombe, pamoja na kila kitu walicho nacho, nao sasa wako Gosheni.” 2Akawachagua ndugu zake watano na kuwapeleka mbele ya Farao.
3Farao akawauliza hao ndugu zake, “Kazi yenu ni nini?”
Wakamjibu, “Watumishi wako ni wafugaji, kama baba zetu walivyokuwa.” 4Pia wakamwambia Farao, “Tumekuja kukaa huku kwa muda mfupi, kwa sababu njaa ni kali huko Kanaani, na mifugo ya watumishi wako haina malisho. Kwa hiyo sasa, tafadhali uruhusu watumishi wako wakae huko Gosheni.”
5Farao akamwambia Yusufu, “Baba yako na ndugu zako wamekuja kwako, 6nayo nchi ya Misri ipo mbele yako; wakalishe baba yako na ndugu zako katika sehemu iliyo bora kupita zote katika nchi. Na waishi Gosheni. Kama unawafahamu walio na uwezo maalum miongoni mwao, wafanye kuwa wasimamizi wa mifugo yangu.”
7Ndipo Yusufu akamleta Yakobo baba yake na kumtambulisha mbele ya Farao. Baada ya Yakobo kumbariki Farao, 8Farao akamuuliza, “Je, una umri gani?”
9Naye Yakobo akamwambia Farao, “Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni miaka mia moja na thelathini. Miaka yangu imekuwa michache na ya taabu, wala haikufikia miaka ya maisha ya baba zangu.” 10Yakobo akambariki Farao, kisha akaondoka mbele yake.
11Ndipo Yusufu akawakalisha baba yake na ndugu zake katika nchi ya Misri, akawapa milki katika sehemu bora sana ya nchi, ile wilaya ya Ramesesi, kama Farao alivyoelekeza. 12Pia Yusufu akampa baba yake, na ndugu zake, na wote wa nyumbani mwa baba yake vyakula, kulingana na hesabu ya watoto wao.
Uongozi wa Yusufu wakati wa njaa
13Hata hivyo, hapakuwa na chakula katika eneo lote; kwa kuwa njaa ilikuwa kali sana; Misri na Kanaani zote zikaharibiwa kwa sababu ya njaa. 14Yusufu akakusanya fedha zote zilizopatikana kutoka mauzo ya nafaka huko Misri na Kanaani, akazileta kwenye jumba la kifalme la Farao. 15Fedha za watu wa Misri na Kanaani zilipokwisha, Wamisri wote wakamjia Yusufu na kumwambia, “Tupatie chakula. Kwa nini tufe mbele ya macho yako? Fedha zetu zimekwisha.”
16Yusufu akawaambia, “Basi leteni mifugo yenu. Nitawauzia chakula kwa kubadilisha na mifugo yenu, kwa kuwa fedha zenu zimekwisha.” 17Kwa hiyo wakaleta mifugo yao kwa Yusufu, naye akawapa chakula kwa kubadilishana na farasi, kondoo na mbuzi, ng’ombe, na punda wao. Katika mwaka huo wote Yusufu akawapa chakula kwa kubadilishana na mifugo yao yote.
18Mwaka ule ulipokwisha, wakamjia mwaka uliofuata na kumwambia, “Hatuwezi kuficha ukweli mbele za bwana wetu kwamba, kwa kuwa fedha zetu zimekwisha na wanyama wetu ni mali yako, sasa hakuna chochote kilichosalia kwa ajili ya bwana wetu isipokuwa miili yetu na ardhi yetu. 19Kwa nini tuangamie mbele ya macho yako, sisi pamoja na nchi yetu? Tununue sisi pamoja na ardhi yetu ili kubadilishana kwa chakula. Nasi pamoja na nchi yetu tutakuwa watumwa wa Farao. Tupe sisi mbegu ili tuweze kuishi wala tusife, nchi yetu isije ikawa ukiwa.”
20Kwa hiyo Yusufu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri. Wamisri, mmoja baada ya mwingine, waliuza mashamba yao, kwa sababu njaa ilikuwa kali sana kwao. Nchi ikawa mali ya Farao, 21naye Yusufu akawafanya watu watumike kama watumwa, kuanzia upande mmoja wa Misri hadi upande mwingine. 22Hata hivyo hakununua nchi ya makuhani, kwa sababu walipokea mgawo wao wa kawaida kutoka kwa Farao, nao walikuwa na chakula cha kuwatosha kutokana na mgawo waliopewa na Farao. Hii ndiyo sababu hawakuuza ardhi yao.
23Yusufu akawaambia watu, “Kwa vile nimewanunua ninyi pamoja na nchi yenu leo kuwa mali ya Farao, hapa kuna mbegu kwa ajili yenu ili mweze kuziotesha. 24Lakini wakati mazao yatakapokuwa tayari, mpeni Farao sehemu ya tano. Sehemu hizo nne zitakazobaki mtaziweka kama mbegu kwa ajili ya mashamba, na kwa ajili ya chakula chenu wenyewe, na cha watu wa nyumbani mwenu na watoto wenu.”
25Wakamwambia, “Umeokoa maisha yetu. Basi na tupate kibali mbele ya macho ya bwana wetu; tutakuwa watumwa wa Farao.”
26Basi Yusufu akaiweka iwe sheria ya ardhi katika nchi ya Misri, ambayo inatumika hata leo, kwamba sehemu ya tano ya mazao ni mali ya Farao. Ni ardhi ya makuhani tu ambayo haikuwa ya Farao.
27Basi Waisraeli wakaishi Misri katika nchi ya Gosheni. Wakapata mali huko, wakastawi na kuongezeka kwa idadi.
28Yakobo akaishi Misri miaka kumi na saba, nayo miaka ya maisha yake ilikuwa mia moja na arobaini na saba (147). 29Wakati ulipokaribia wa Israeli kufa, akamwita mwanawe Yusufu na kumwambia, “Kama nimepata kibali machoni pake, weka mkono wako chini ya paja langu na uniahidi kuwa utanifanyia fadhili na uaminifu. Usinizike Misri, 30lakini nitakapopumzika na baba zangu, unichukue kutoka Misri, ukanizike walipozikwa.”
Yusufu akamwambia, “Nitafanya kama unavyosema.”
31Akamwambia, “Niapie.” Ndipo Yusufu akamwapia, naye Israeli akaabudu akiwa ameegemea juu ya kichwa cha fimbo yake.
Iliyochaguliwa sasa
Mwanzo 47: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.