Mwanzo 47:23-31
Mwanzo 47:23-31 SRUV
Yusufu akawaambia watu, Angalieni, nimewanunua leo, ninyi, na nchi yenu, kuwa mali ya Farao; basi mbegu zenu ni hizi, zipandeni katika nchi. Wakati wa mavuno mtampa Farao sehemu ya tano, na sehemu nne zitakaposalia zitakuwa zenu wenyewe, kuwa mbegu za nchi, na chakula chenu, na chakula chao waliomo nyumbani mwenu, na chakula cha watoto wenu. Wakasema, Umeyaokoa maisha yetu, na tuone kibali machoni pa bwana wetu, nasi tutakuwa watumwa wa Farao. Yusufu akaifanya kuwa sheria ya nchi ya Misri hata leo, ya kwamba sehemu ya tano iwe mali ya Farao. Ila nchi ya makuhani tu haikuwa mali ya Farao. Israeli akakaa katika nchi ya Misri, katika nchi ya Gosheni. Wakapata mali humo, wakaongezeka na kuzidi sana. Yakobo akaishi katika nchi ya Misri miaka kumi na saba, basi umri wake Yakobo ulikuwa miaka mia moja na arubaini na saba. Siku za kufa kwake Israeli zikakaribia; akamwita mwanawe Yusufu, akamwambia, Kama nimeona kibali machoni pako, weka mkono wako chini ya paja langu, ukanifanyie rehema na kweli; nakusihi usinizike katika Misri. Lakini nitakapolala pamoja na baba zangu, unichukue toka Misri, unizike katika kaburi lao. Akasema, Nitafanya kama ulivyosema. Akanena, Niapie. Naye akamwapia. Israeli akajiinamisha kwenye mchago wa kitanda.