Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 42:29-38

Mwanzo 42:29-38 NEN

Walipofika kwa Yakobo baba yao katika nchi ya Kanaani, wakamweleza mambo yote yaliyowapata. Wakasema, “Huyo mtu ambaye ndiye bwana katika nchi hiyo alisema nasi kwa ukali, akatutendea kana kwamba sisi tulikuwa tunaipeleleza nchi. Lakini tulimwambia, ‘Sisi ni watu waaminifu, sio wapelelezi. Tulizaliwa ndugu kumi na wawili, wana wa baba mmoja. Mmoja alikufa, na mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu huko Kanaani.’ “Ndipo huyo mtu aliye bwana katika nchi hiyo alipotuambia, ‘Hivi ndivyo nitafahamu kuwa ninyi ni watu waaminifu: Mwacheni mmoja wa ndugu zenu pamoja nami hapa, kisha nendeni mpeleke chakula kwa ajili ya jamaa yenu inayoteseka kwa njaa. Lakini mleteni huyo ndugu yenu mdogo kwangu, ndipo nitajua kuwa ninyi sio wapelelezi, ila ni watu waaminifu. Kisha nitamrudisha ndugu yenu, nanyi mtaweza kufanya biashara katika nchi hii.’ ” Walipokuwa wanamimina nafaka kutoka kwenye magunia yao, ndani ya gunia la kila mtu kulikuwa na mfuko wa fedha! Wakati wao na baba yao walipoona mifuko ya fedha, wakaogopa. Yakobo baba yao akawaambia, “Ninyi mmenipokonya watoto wangu. Yosefu hayupo na Simeoni hayupo tena na sasa mnataka kumchukua Benyamini. Kila kitu ni kinyume nami!” Ndipo Reubeni akamwambia baba yake, “Waweza kuwaua wanangu wote wawili, ikiwa sitamrudisha Benyamini kwako. Mkabidhi Benyamini katika uangalizi wangu, nami nitamrudisha.” Lakini Yakobo akasema, “Mwanangu hatashuka huko pamoja nanyi; ndugu yake amekufa naye ndiye peke yake aliyebaki. Ikiwa atapatwa na madhara katika safari mnayoiendea, mtashusha kichwa changu chenye mvi kaburini kwa masikitiko.”