Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 42:29-38

Mwanzo 42:29-38 Biblia Habari Njema (BHN)

Walipowasili nchini Kanaani kwa baba yao Yakobo, walimsimulia yote yaliyowapata, wakamwambia, “Mkuu wa nchi ile alisema nasi kwa ukali, na kutushuku kwamba sisi ni wapelelezi nchini mwake. Lakini sisi tulimweleza kuwa sisi ni watu waaminifu, na wala si wapelelezi. Tulimweleza kuwa sisi tuko ndugu kumi na wawili wa baba mmoja, na kwamba mmoja wetu ni marehemu na yule mdogo yuko nyumbani nchini Kanaani pamoja na baba yetu. Ndipo mkuu wa nchi hiyo akatuambia, ‘Hivi ndivyo nitakavyotambua kama kweli nyinyi ni watu waaminifu: Mwacheni kwangu ndugu yenu mmoja, nanyi wengine mpeleke nafaka nyumbani kwa jamaa zenu wenye njaa. Kisha mleteni kwangu huyo ndugu yenu mdogo, na hapo nitajua kuwa nyinyi si wapelelezi, ila ni watu waaminifu. Mkifanya hivyo nitamwacha huru ndugu yenu, nanyi mtaruhusiwa kufanya biashara katika nchi hii.’” Walipokuwa wanamimina nafaka kutoka magunia yao, walishangaa kuona kila mmoja wao amerudishiwa kifuko chake na fedha ndani ya gunia lake. Walipoona hayo, wote pamoja na baba yao, wakashikwa na hofu. Baba yao Yakobo, akawaambia, “Mnanipokonya watoto wangu! Yosefu hayuko; Simeoni hayuko; sasa mnataka kumchukua na Benyamini. Yote hayo yamenipata!” Hapo Reubeni akamwambia baba yake, “Nisipomrudisha Benyamini, waue wanangu wawili. Mwache Benyamini mikononi mwangu, nami nitamlinda na kumrudisha kwako.” Lakini baba yake akamjibu, “Mwanangu hatakwenda nanyi; ndugu yake amekwisha fariki, naye peke yake ndiye aliyebaki. Mimi ni mzee mwenye mvi ikiwa kijana huyu atapatwa na madhara yoyote katika safari mtakayofanya basi, mtaniua kwa huzuni.”

Shirikisha
Soma Mwanzo 42

Mwanzo 42:29-38 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Walipofika kwa Yakobo baba yao katika nchi ya Kanaani, wakamweleza mambo yote yaliyowapata. Wakasema, “Huyo mtu ambaye ndiye bwana katika nchi hiyo alisema nasi kwa ukali, akatutendea kana kwamba sisi tulikuwa tunaipeleleza nchi. Lakini tulimwambia, ‘Sisi ni watu waaminifu, sio wapelelezi. Tulizaliwa ndugu kumi na wawili, wana wa baba mmoja. Mmoja alikufa, na mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu huko Kanaani.’ “Ndipo huyo mtu aliye bwana katika nchi hiyo alipotuambia, ‘Hivi ndivyo nitafahamu kuwa ninyi ni watu waaminifu: Mwacheni mmoja wa ndugu zenu pamoja nami hapa, kisha nendeni mpeleke chakula kwa ajili ya jamaa yenu inayoteseka kwa njaa. Lakini mleteni huyo ndugu yenu mdogo kwangu, ndipo nitajua kuwa ninyi sio wapelelezi, ila ni watu waaminifu. Kisha nitamrudisha ndugu yenu, nanyi mtaweza kufanya biashara katika nchi hii.’ ” Walipokuwa wanamimina nafaka kutoka kwenye magunia yao, ndani ya gunia la kila mtu kulikuwa na mfuko wa fedha! Wakati wao na baba yao walipoona mifuko ya fedha, wakaogopa. Yakobo baba yao akawaambia, “Ninyi mmenipokonya watoto wangu. Yosefu hayupo na Simeoni hayupo tena na sasa mnataka kumchukua Benyamini. Kila kitu ni kinyume nami!” Ndipo Reubeni akamwambia baba yake, “Waweza kuwaua wanangu wote wawili, ikiwa sitamrudisha Benyamini kwako. Mkabidhi Benyamini katika uangalizi wangu, nami nitamrudisha.” Lakini Yakobo akasema, “Mwanangu hatashuka huko pamoja nanyi; ndugu yake amekufa naye ndiye peke yake aliyebaki. Ikiwa atapatwa na madhara katika safari mnayoiendea, mtashusha kichwa changu chenye mvi kaburini kwa masikitiko.”

Shirikisha
Soma Mwanzo 42