Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 41:9-36

Mwanzo 41:9-36 NENO

Ndipo mnyweshaji mkuu alimwambia Farao, “Leo nimekumbushwa kosa langu. Farao alipowakasirikia watumishi wake, alinifunga mimi na mwokaji mkuu katika nyumba ya mkuu wa walinzi. Katika usiku mmoja, kila mmoja wetu aliota ndoto, na kila ndoto ilikuwa na maana yake. Basi kuna kijana Mwebrania aliyekuwa pamoja nasi huko, mtumishi wa mkuu wa walinzi. Tulimweleza ndoto zetu, naye akatufasiria, akitupatia kila mtu tafsiri ya ndoto yake. Nayo mambo yakawa jinsi alivyotufasiria ndoto zetu: Mimi nilirudishwa kazini mwangu, naye huyo mwingine akaangikwa.” Basi, Farao akatuma Yusufu aitwe, naye akatolewa kifungoni haraka. Baada ya kunyoa na kubadilisha nguo zake, akaenda mbele ya Farao. Farao akamwambia Yusufu, “Nimeota ndoto, wala hakuna mtu hata mmoja anayeweza kuifasiri. Lakini nimesikia habari yako kwamba unapoelezwa ndoto unaweza kuifasiri.” Yusufu akamjibu Farao, “Siwezi kuifasiri, lakini Mungu atampa Farao jibu analolihitaji.” Kisha Farao akamwambia Yusufu, “Katika ndoto yangu nilikuwa nimesimama ukingoni mwa Mto Naili. Nikawaona ng’ombe saba, wazuri na wanono, wakijitokeza kutoka mtoni, wakaja kujilisha kwenye matete. Baada ya hao, ng’ombe wengine saba wadhaifu wakatokea, wabaya sana na waliokonda. Kamwe sikuwahi kuona ng’ombe wabaya jinsi hiyo katika nchi yote ya Misri. Hao ng’ombe waliokonda na wabaya sana wakawala wale ng’ombe saba walionona waliojitokeza kwanza. Lakini hata baada ya kuwala, hakuna mtu ambaye angeweza kusema kwamba wamekula, bado walionekana wabaya kama mwanzoni. Kisha nikaamka kutoka usingizini. “Pia katika ndoto zangu niliona masuke saba ya nafaka, yamejaa na mazuri, yanakua katika bua moja. Baada ya hayo, masuke mengine saba yakachipua, yaliyonyauka, membamba na yamekaushwa na upepo wa mashariki. Yale masuke membamba ya nafaka yakayameza yale masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka. Nimewaeleza waaguzi, wala hakuna yeyote aliyeweza kunifasiria.” Ndipo Yusufu akamwambia Farao, “Ndoto za Farao ni ndoto hiyo hiyo moja. Mungu amemfunulia Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. Ng’ombe saba wazuri ni miaka saba, nayo masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka ni miaka saba; ni ndoto hiyo hiyo moja. Ng’ombe saba waliokonda na wabaya waliojitokeza baadaye ni miaka saba, vivyo hivyo masuke saba ya ngano yaliyodhoofika na kukaushwa na upepo wa mashariki: Ni miaka saba ya njaa. “Ni kama nilivyomwambia Farao. Mungu amemwonesha Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. Miaka saba ya shibe inakuja katika nchi yote ya Misri, lakini itafuata miaka saba ya njaa. Ndipo shibe yote ya Misri itasahaulika na njaa itaikumba nchi. “Shibe iliyokuwa katika nchi haitakumbukwa, kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno. Sababu ya ndoto kumjia Farao kwa namna mbili ni kwamba jambo hilo Mungu ameshaamua kwa hakika, naye Mungu atalifanya karibuni. “Basi sasa Farao na atafute mtu mwenye akili na hekima ili amweke kuwa msimamizi wa nchi ya Misri. Farao na aweke wasimamizi nchini kote, wakusanye sehemu ya tano ya mavuno ya Misri katika miaka hii saba ya shibe. Wakusanye chakula chote katika miaka hii saba ya neema inayokuja na kuhifadhi nafaka chini ya mamlaka ya Farao, iwe akiba ya chakula katika miji. Chakula hiki kitakuwa akiba ya tahadhari kwa ajili ya nchi, ili kitumike katika ile miaka saba ya njaa itakayokuja Misri, ili nchi isiharibiwe na njaa.”