Mwanzo 40:5-19
Mwanzo 40:5-19 NENO
kila mmoja wa hao wawili waliokuwa wamewekwa gerezani, yaani mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, waliota ndoto usiku mmoja, na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti. Yusufu alipowajia asubuhi yake, akawaona kwamba walikuwa na huzuni. Ndipo Yusufu akawauliza maafisa hao wa Farao waliokuwa chini ya ulinzi pamoja naye nyumbani mwa bwana wake hivi, “Mbona nyuso zenu zimejaa huzuni leo?” Wakamjibu, “Sisi sote tumeota ndoto, lakini hakuna wa kuzifasiri.” Ndipo Yusufu akawaambia, “Je, kufasiri ndoto si ni kazi ya Mungu? Niambieni ndoto zenu.” Basi mkuu wa wanyweshaji akamweleza Yusufu ndoto yake. Akamwambia, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu, nao mzabibu ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua, maua yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu zilizoiva. Kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu. Nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, na nikaweka kikombe mkononi mwake.” Yusufu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Matawi matatu ni siku tatu. Baada ya siku tatu, Farao atakutoa gerezani na kukurudisha kwenye nafasi yako, nawe utaweka kikombe cha Farao mkononi mwake, jinsi ulivyofanya ulipokuwa mnyweshaji wake awali. Lakini mambo yako yatakapokuwa mazuri, unikumbuke, unifanyie wema. Useme mema kunihusu kwa Farao ili unitoe huku gerezani. Kwa maana nilichukuliwa kwa nguvu kutoka nchi ya Waebrania, na hata hapa nilipo sikufanya lolote linalostahili niwekwe gerezani.” Yule mwokaji mkuu alipoona kuwa Yusufu amefasiri vizuri, akamwambia Yusufu, “Mimi pia niliota ndoto. Kichwani mwangu kulikuwa vikapu vitatu vya mikate. Katika kikapu cha juu kulikuwa na aina zote za vyakula vilivyookwa kwa ajili ya Farao, lakini ndege walikuwa wakivila kutoka kikapu nilichobeba kichwani.” Yusufu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Vikapu vitatu ni siku tatu. Baada ya siku tatu, Farao atakata kichwa chako na kukutundika juu ya mti. Nao ndege watakula nyama ya mwili wako.”