Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 40:5-19

Mwanzo 40:5-19 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, usiku mmoja, yule mtunza vinywaji mkuu na yule mwoka mikate mkuu wa mfalme wa Misri, waliota ndoto humo gerezani, kila mmoja na ndoto yake tofauti. Yosefu alipokwenda kwao asubuhi na kuwaona, wote wawili walikuwa wenye wasiwasi. Basi, Yosefu akawauliza maofisa hao wa Farao waliokuwa kifungoni pamoja naye nyumbani mwa bwana wake, “Mbona leo mna nyuso za huzuni?” Wakamjibu, “Tuna huzuni kwa kuwa tumeota ndoto na hakuna awezaye kututafsiria ndoto zetu.” Yosefu akawaambia, “Je, kutafsiri ndoto si kazi ya Mungu? Basi, niambieni ndoto zenu.” Mtunza vinywaji mkuu wa mfalme akamsimulia Yosefu ndoto yake, akisema, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu, nao ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua majani, maua yake yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu mbivu. Mkononi mwangu nilikuwa na kikombe cha Farao, basi, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe hicho, nikampa Farao.” Yosefu akamwambia huyo mtumishi, “Tafsiri ya ndoto yako ni hii: Yale matawi matatu ni siku tatu. Baada ya siku tatu Farao atakunyanyua kutoka gerezani na kukurudisha tena katika cheo chako. Utaweza tena kumpa Farao kikombe mkononi kama ulivyokuwa unafanya hapo awali. Lakini tafadhali usinisahau wakati mambo yatakapokwendea vema; unifanyie fadhili na kunitaja mbele ya Farao, nipate kutoka humu gerezani. Maana mimi nilitoroshwa kutoka nchi ya Waebrania, na hapa Misri sijafanya chochote kinachostahili nitiwe gerezani.” Yule mwoka mikate mkuu alipoona kwamba tafsiri ile ni nzuri, akamwambia Yosefu, “Hata mimi niliota ndoto! Katika ndoto yangu nilikuwa nimechukua kichwani nyungo tatu za mikate. Katika ungo wa juu, kulikuwa na vyakula mbalimbali vilivyookwa kwa ajili ya Farao. Lakini, ndege walikuwa wakivila kutoka ungo huo kichwani pangu!” Yosefu akamwambia, “Tafsiri ya ndoto yako ni hii: Zile nyungo tatu ni siku tatu. Baada ya siku tatu Farao atakunyanyua kutoka gerezani, atakiinua kichwa chako akutundike mtini, nao ndege wataula mwili wako.”

Shirikisha
Soma Mwanzo 40

Mwanzo 40:5-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Wakaota ndoto wote wawili, kila mtu ndoto yake usiku mmoja, kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri waliofungwa gerezani. Yusufu akawajia asubuhi, akawaona wamefadhaika. Akawauliza hao maofisa wa Farao, waliokuwa pamoja naye katika kifungo, nyumbani mwa bwana wake, akisema, Mbona nyuso zenu zimekunjamana leo? Wakamwambia, Tumeota ndoto wala hapana awezaye kuifasiri. Yusufu akawaambia, Nawaomba mniambie, kufasiri si ni kazi ya Mungu? Mnyweshaji mkuu akamhadithia Yusufu ndoto yake; akamwambia, Katika ndoto yangu nimeota, uko mzabibu mbele yangu. Na katika mzabibu mlikuwa na matawi matatu, nao ulikuwa kana kwamba unamea, unachanua maua, vishada vyake vikatoa zabibu zilizoiva. Na kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, nikampa Farao kikombe mkononi mwake. Yusufu akamwambia, Tafsiri yake ndiyo hii. Matawi matatu ni siku tatu. Baada ya siku tatu Farao atakiinua kichwa chako, atakurudisha katika kazi yako; nawe utampa Farao kikombe mkononi mwake, kama desturi ya kwanza, ulipokuwa mnyweshaji wake. Ila unikumbuke mimi, utakapopata mema, ukanifanyie fadhili, nakuomba, ukanitaje kwa Farao, na kunitoa katika nyumba hii. Kwa sababu hakika niliibwa kutoka nchi ya Waebrania, wala hapa sikutenda jambo lolote hata wanitie gerezani. Mkuu wa waokaji alipoona ya kwamba hiyo tafsiri ni ya mema, akamwambia Yusufu, Mimi kadhalika nilikuwa katika ndoto yangu, na tazama, ziko nyungo tatu za mikate myeupe juu ya kichwa changu. Na katika ungo wa juu, mlikuwa na kila namna ya chakula kwa Farao, kazi za mwokaji; ndege wakavila katika ungo juu ya kichwa changu. Yusufu akajibu, akasema, Tafsiri yake ndiyo hii Nyungo tatu ni siku tatu. Baada ya siku tatu Farao atakiinua na kukuondolea kichwa chako, na kukutundika juu ya mti, na ndege watakula nyama yako.

Shirikisha
Soma Mwanzo 40

Mwanzo 40:5-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Wakaota ndoto wote wawili, kila mtu ndoto yake usiku mmoja, kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri waliofungwa gerezani. Yusufu akawajia asubuhi, akawaona wamefadhaika. Akawauliza hao maakida wa Farao, waliokuwa pamoja naye katika kifungo, nyumbani mwa bwana wake, akisema, Mbona nyuso zenu zimekunjamana leo? Wakamwambia, Tumeota ndoto wala hapana awezaye kuifasiri. Yusufu akawaambia, Kufasiri si kazi ya Mungu? Tafadhalini mniambie. Mnyweshaji mkuu akamhadithia Yusufu ndoto yake; akamwambia, Katika ndoto yangu nimeota, uko mzabibu mbele yangu. Na katika mzabibu mlikuwa na matawi matatu, nao ulikuwa kana unamea, unachanua maua, vishada vyake vikatoa zabibu zilizoiva. Na kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, nikampa Farao kikombe mkononi mwake. Yusufu akamwambia, Tafsiri yake ndiyo hii. Matawi matatu ni siku tatu. Baada ya siku tatu Farao atakiinua kichwa chako, atakurudisha katika kazi yako; nawe utampa Farao kikombe mkononi mwake, kama desturi ya kwanza, ulipokuwa mnyweshaji wake. Ila unikumbuke mimi, utakapopata mema, ukanifanyie fadhili, nakuomba, ukanitaje kwa Farao, na kunitoa katika nyumba hii. Kwa sababu hakika naliibiwa kutoka nchi ya Waebrania, wala hapa sikutenda neno lo lote hata wanitie gerezani. Mkuu wa waokaji alipoona ya kwamba hiyo tafsiri ni ya mema, akamwambia Yusufu, Mimi kadhalika nilikuwa katika ndoto yangu, na tazama, ziko nyungo tatu za mikate myeupe juu ya kichwa changu. Na katika ungo wa juu, mlikuwa na kila namna ya chakula kwa Farao, kazi za mwokaji; ndege wakavila katika ungo juu ya kichwa changu. Yusufu akajibu, akasema, Tafsiri yake ndiyo hii Nyungo tatu ni siku tatu. Baada ya siku tatu Farao atakiinua na kukuondolea kichwa chako, na kukutundika juu ya mti, na ndege watakula nyama yako.

Shirikisha
Soma Mwanzo 40

Mwanzo 40:5-19 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

kila mmoja wa hao wawili waliokuwa wamewekwa gerezani, yaani mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, waliota ndoto usiku mmoja, na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti. Yusufu alipowajia asubuhi yake, akawaona kwamba walikuwa na huzuni. Ndipo Yusufu akawauliza maafisa hao wa Farao waliokuwa chini ya ulinzi pamoja naye nyumbani mwa bwana wake hivi, “Mbona nyuso zenu zimejaa huzuni leo?” Wakamjibu, “Sisi sote tumeota ndoto, lakini hakuna wa kuzifasiri.” Ndipo Yusufu akawaambia, “Je, kufasiri ndoto si ni kazi ya Mungu? Niambieni ndoto zenu.” Basi mkuu wa wanyweshaji akamweleza Yusufu ndoto yake. Akamwambia, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu, nao mzabibu ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua, maua yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu zilizoiva. Kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu. Nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, na nikaweka kikombe mkononi mwake.” Yusufu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Matawi matatu ni siku tatu. Baada ya siku tatu, Farao atakutoa gerezani na kukurudisha kwenye nafasi yako, nawe utaweka kikombe cha Farao mkononi mwake, jinsi ulivyofanya ulipokuwa mnyweshaji wake awali. Lakini mambo yako yatakapokuwa mazuri, unikumbuke, unifanyie wema. Useme mema kunihusu kwa Farao ili unitoe huku gerezani. Kwa maana nilichukuliwa kwa nguvu kutoka nchi ya Waebrania, na hata hapa nilipo sikufanya lolote linalostahili niwekwe gerezani.” Yule mwokaji mkuu alipoona kuwa Yusufu amefasiri vizuri, akamwambia Yusufu, “Mimi pia niliota ndoto. Kichwani mwangu kulikuwa vikapu vitatu vya mikate. Katika kikapu cha juu kulikuwa na aina zote za vyakula vilivyookwa kwa ajili ya Farao, lakini ndege walikuwa wakivila kutoka kikapu nilichobeba kichwani.” Yusufu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Vikapu vitatu ni siku tatu. Baada ya siku tatu, Farao atakata kichwa chako na kukutundika juu ya mti. Nao ndege watakula nyama ya mwili wako.”

Shirikisha
Soma Mwanzo 40