Mwanzo 4:1-16
Mwanzo 4:1-16 NENO
Adamu akakutana kimwili na mkewe Hawa, naye akapata mimba, akamzaa Kaini. Hawa akasema, “Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu nimemzaa mtoto wa kiume.” Baadaye akamzaa Habili ndugu yake. Basi Habili akawa mfugaji, na Kaini akawa mkulima. Baada ya muda, Kaini akaleta baadhi ya mazao ya shamba ikiwa sadaka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini Habili akaleta fungu nono kutoka baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo yake. Mwenyezi Mungu akamkubali Habili pamoja na sadaka yake, lakini Mungu hakumkubali Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa hiyo Kaini akakasirika sana, uso wake ukawa na huzuni. Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika? Kwa nini uso wako una huzuni? Ukifanya lililo sawa, je, hutakubalika? Lakini usipofanya lililo sawa, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, ikikutamani wewe, lakini inakupasa uishinde.” Basi Kaini akamwambia ndugu yake Habili, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Habili ndugu yake, akamuua. Kisha Mwenyezi Mungu akamuuliza Kaini, “Ndugu yako Habili yuko wapi?” Akamjibu, “Sijui. Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” Mwenyezi Mungu akasema, “Umefanya nini? Sikiliza! Damu ya ndugu yako inanililia mimi kutoka ardhini. Sasa umelaaniwa na umehamishwa kutoka ardhi, ambayo imefungua kinywa chake na kupokea damu ya ndugu yako kutoka mkononi mwako. Utakapoilima ardhi, haitakupa tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga duniani bila utulivu.” Kaini akamwambia Mwenyezi Mungu, “Adhabu yangu ni zaidi ya ninavyoweza kustahimili. Leo unanifukuza kutoka nchi, nami nitafichwa mbali na uwepo wako. Nitakuwa mtu wa kutangatanga duniani bila utulivu, na yeyote anionaye ataniua.” Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia, “La, sivyo! Ikiwa mtu yeyote atamuua Kaini, atalipizwa kisasi mara saba.” Kisha Mwenyezi Mungu akamwekea Kaini alama ili yeyote angemwona asimuue. Kwa hiyo Kaini akaondoka mbele za Mwenyezi Mungu, akaenda kuishi katika nchi ya Nodi, mashariki mwa Edeni.